Habari za Punde

DC -Handeni Amewataka Viongozi Nendeni Mkasikilize na Kutatua Kero za Wananchi Vijijini .

Na. Hamida Kamchalla, HANDENI.
VIONGOZI wa Taasisi zote zinazohusika na shuhuli mbalimbali za serikali kwenye wilaya ziwe pamoja kusikiliza na kutatua kero za wananchi badala ya kuwaacha wananchi hao kupeleka kero zao kwenye ofisi za wahusika.

Kauli hiyo ilitolewa mwanzoni mwa wiki na Mkuu wa wilaya ya Handeni Toba Nguvila wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kwamsisi, Kata ya Kwamsisi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kukumbana na kero ya migogoro ya ardhi na mipaka.

Nguvila alisema kuwa viongozi wanatakiwa kuwafuata wananchi na kusikiliza na kutatua kero zao kwani bila kufanya hivyo itakuwa vigumu kumaliza kero hizo kutokana na kwamba kila mmoja atafika kwenye ofisi husika na kupeleka kero zake kwa wakati wake.

"Haiwezekani tukawa tupo ofisini halafu huku kuna kero za wananchi nyingi, leo atakuja mmoja, kesho mmoja haiwezekani kumaliza kero kwa staili hiyo, ni lazima taasisi zote zinazohusika na utendaji wa shuhuli mbalimbali za serikali katika wilaya tuwe pamoja tusikilize tutatue" alisema. 

Aidha Nguvila aliwataka wananchi hao kuwa wawazi na kueleza kero zao katika mkutano huo wa hadhara ili kupatiwa majibu kwani kila kwenye dhamana yake alikuwepo eneo la tukio hivyo ni mahala lake kila mmoja kuwajibika katika dhamana yake.

"Vikero vimelimbikizwa vidogo vidogo, sio sawa wenye dhamana tupo hapa ni lazima watoe majawabu hapa hapa na mimi ndio mkuu wa wilaya kwa hiyo sitaki wananchi wangu muondoke hapa na kero zenu, ziwe ni kero za mipaka au umedhulumiwa kiwanja sema, kero za hospitali sema, wapo wote hapa, kero zozote hapa leo ziishe" alisistiza Nguvila.

Kwa upande wao wananchi walitoa malalamiko yao mbalimbali yakiwemo ya migogoro ya ardhi, afya, mifugo, miundombinu ambapo baadhi ya hayo yalipatiwa majibu hapa hapo huku mengine yakichukuliwa kufanyiwa uhakiki zaidi.

Walieleza kwamba katika kijiji hicho kuna mgogoro wa mipaka kati yao na kijiji cha Kwedikabu, Kitumbi pamoja mgogoro wa ardhi baina ya yao na shamba la Sasumuwa ambayo ni ya muda mrefu na ilishafikishwa kwa viongozi mbalimbali wa ardhi akiwemo Waziri mwenye dhamana lakini tatizo bado halijatatuliwa.

"Kero hiyo tuliifikisha kwa waziri wa ardhi alipokuja wilayani Handeni na yeye akawaagiza viongozi wa wilaya wakiwemo wa idara ya ardhi, alikuja kaimu mkuu wa wilaya na mkurugenzi kipindi kile Gondwe hakuwepo, tukasomewa waraka tukaambiwa yule mwekezaji amepewa notsi ambayo ingekwisha tarehe 30 mwezi wa 3 kwamba alipewa siku 90" alieleza mwanakiji aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Luhezi.

"Lakini walitupa na muelekeo kwamba baada ya notisi hiyo kwisha halmashauri ya wilaya itakaa halafu itapeleka mapendekezo yake kunakohusika na mwisho wa mapendekezo na notisi hiyo kwisha tutafuatilia, lakini mpaka leo hii tunaona kimya" alifafanua Luhezi.

Hata hivyo wananchi hao wametakiwa kuwa na uvumilivu wakati suala lao likifanyiwa kazi na kupatiwa majibu sahihi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.