Habari za Punde

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo amali afungua semina ya maandalizi ya kujiunga na Vyuo vikuu


Na mwandishi wetu


NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Simai Mohammed Said amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imeiongezea  bajeti  Wizara ya Elimu ili kuhakikisha wananchi wote  wanapata Elimu Kama  walivyoanzisha waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.



Akizungumza wakati alipofungua semina ya maandalizi ya kujiunga na Vyuo vikuu iliotayarishwa na jumuia ya 'Afrika moja movement' katika ukumbi wa kariakoo Mjini Unguja amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu inaendelea  kuifanyia kazi falsafa za waasisi  ili kuhakikisha Zanzibar inazalisha wataalam wanaoendena na soko la ajira.



Alisema  ipo haja kwa Wanafunzi kupatiwa taaluma juu ya kujiunga na Elimu ya juu na namna ya kupata mikopo ili kuepusha usumbufu kwa Wanafunzi na kuepuka kujiunga na vyuo visivyo sahihi kwao.



Said  aliwaomba Wanafunzi watakaopata nafasi ya masomo nje ya nchi kua wazalendo  kwa kurejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo na kusimamia Mila, utamaduni  na silka  za nchi yao kwa kipindi chote wanapokuwa masomoni.



Aidha Simai  aliwanasihi Wanafunzi kusoma kwa bidii ili kulinda heshima ya Taifa la Tanzania na kuwataka wanafunzi kutumia haki yao ya Kikatiba kwa kwenda  kupiga kura wakati utakapofika na kuhakikisha wanadumisha amani ya nchi yao pamoja na kuwataka kuepukana  vurugu zinazoashiria uvunjifu wa amani.



Nae Mratibu Mkuu wa Africa Moja Movement Unguja Eshe Mtumwa Said ameeleza kuwa Jumuiya yao inaendesha pragam za kuwajengea uwezo vijana wa Kiafrika na kuwaunganisha vijana wa Afrika katika nyanja za
kiuchumi, kiutamaduni na kiitikadi.



Alifahamisha kuwa  wanatoa program za kuwasaidia vijana katika makundi mbali mbali kama vile mayatima, wazee na hata watu wenye ulemavu.



Alisema  kuwa changamato kubwa ambayo inawakumba Wanafunzi wa Sekondari na hata wale wa Sekondari ya Juu kushindwa kujua fani wanazotaka kusoma hali  inayopelekea kuchagua fani zisozokuwa na soko.



Aliwasihi wanafunzi kusikiliza kwa makini maelezo watakayo patiwa ili kuweza kufanya maamuzi mazuri katika uchaguzi wa fani ambazo watakwenda kusoma huko Vyuoni.



Kwa upande wake Afisa NACTE  Twaha Twaha amewataka Wanafunzi kusoma kutokana na malengo yao na sio kufuata mkumbo kwani hakutaweza kutimiza ndoto zao na kusema NACTE imejipanga kuhakikisha  Vyuo
vinatoa fani ambazo zina Walimu waliobobea ili kuondosha usumbufu kwa wahitimu, huku akiwataka Wanafunzi kuhakisha wanasoma fani walizokuwa na wanasifa nazo kutokana na alama zao za ufaulu.



Katika semina hiyo ya siku moja mada mbali mbali zilijadiliwa ikiwemo huduma za Mikopo  Zanzibar na Tanzania Bara pamoja na mada ya kazi za NACTE.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.