Habari za Punde

Zaidi ya Watoto Elfu 20 Walio Chini ya Miaka Mitano Wasajaliwa na Kupatiwa Vyeti Vya Kuzaliwa

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WATOTO wapatao 20342 sawa na asilimia 54 walio na umri chini ya miaka mitano katika wilaya ya Tanga wamefikiwa na kuandikishwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa katika kipindi cha siku 12 za awali katika mpango wa kusajili watoto walio na umri huo katika mkoa wa Tanga.

Mpango huo ulioandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kwa wilaya ya Tanga ililenga kuwafikia watoto wapatao 37,755 katika kipindi cha siku 12 za awali, zoezi ambalo lilianza Agost 8 na linatrajiwa kumalizika kesho Agost 19.

Akiongea na Nipashe ofisini kwake jana Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga Charles Mkombe alisema kuwa idadi ya watoto walioandikishwa na kupatiwa vyeti ni kubwa kwani baadhi yao wameandikishwa lakini taarifa zao hazikuweza kuingizwa rasmi kwenye mfumo wa takwimu.

"Kwa wilaya ya Tanga na Jiji kwa ujumla tulilenga kuwafikia na kuwapatia vyeti watoto 37,755 lakini mpaka kufikia leo tumefanikiwa kuandikisha watoto 20,342 ambao taarifa zao zimeingizwa kwenye mfumo, naweza kusema tumewafikia watoto wengi zaidi na sasa tumeweka kambi maalumu ili wale ambao taarifa zao hazijaingizwa ziweze kuingizwa" alisema Mkombe.

Aidha alieleza kwamba katika wilaya hiyo vituo 56 vya kutolea huduma za afya pamoja Kata zote vilitumika katika kufanikishia zoezi la kusajili watoto hao na kuongeza kuwa kwa watoto ambao taarifa zao hazikuweza kuingizwa ilitokana na changamoto ya mfumo ambao ulisumbua kutokana na uwingi wa usajili uliokuwa ukiendelea katika maeneo mbalimbali.

"Changamoto iliyokuwepo wakati wa usajili ni mfumo ulikuwa unasumbua kwakuwa halmashauri zote pamoja na mkoa wa Kilimanjaro walikuwa wakitumia mfumo huo kwa wakati mmoja hivyo kuleta ugumu kidogo katika zoezi hilo" aliongeza.

Hata hivyo Mkombe alitoa pongezi kwa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na kuonyesha ushirikiano wa halo ya juu katika kufanikisha zoezi hill ambalo aliongeza lilifanyika vizuri katika kila kituo na muitikio ulikuwa mkubwa tofauti na ilivyotarajiwa awali.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa alieleza kwamba mafanikio yaliyopatikana kwenye kampeni hiyo yamekuwa chachu kwa serikali kwani imeonyesha ni jinsi gani wananchi wamepata hanasa ya kuitikia kupigania haki za msingi kwa watoto hao.

Mwilapwa alibainisha kwamba kampeni hiyo ilikuwa ni mpango wa kuwaweka sawa wananchi na kwamba zoezi hilo ni endelevu kwa nchi nzima ili kuhakikisha kula mtoto aliye na huo anapatiwa cheti cha kuzaliwa bila malipo na baada ya kumalizika siku 12 kutaandaliwa mpango mwengine wa siku 90 utakaoanza mara tu baada ya kesho kumalizika zoezi la awali.

"Kwanza niwapongeze wale wote waliofanikiwa kuwaandikisha watoto wao kwa ajili ya kupatiwa vyeti lakini pia nitoe wito kwa wananchi wa wilaya ya Tanga, zoezi hili ni endelevu hivyo kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kuwaandikisha watoto wao na wale wanaoendelea kujifungua popote walipo wafike kwenye vituo vya kuandikisha watoto" alieleza Mwilapwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.