Habari za Punde

Balozi Seif apiga kura leo skuli ya sekondari Kitope jimbo la Mahonda


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kati kati akitumbukiza karatasi za kupigia Kura baada ya kuwachanguwa Viongozi aliyoridhika nao kufuatia Kampeni zilizokuwa zimeshamiri Nchini na kudumu ndani ya Siku 45 kwa Zanzibar na siku 61 kwa upande wa Muungano.

Balozi Seif alipiga kura hiyo kwenye kituo chake cha kawaida Chumba Nambari Mbili katika Skuli ya Sekondari ya Kitope Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR


Jumatano ya Oktoba Mwaka 2020 ambayo Watanzania walikuwa wakiisubiri kutoa maamuzi ya kwa kutumbukiza Kura ili kukipa dhamana Chama kilichonadi vyema Ilani na Sera zake na kukubalika imewadia.

Watanzania hao wamepata fursa ya kutimiza haki yao ya Kidemokrasia ya kuwachagua Viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha Miaka Mitano ndani ya Mfumo wa Vyama vingi vya Kisiasa ulioanza Mnamo Mwaka 1995 takriban Chaguzi ya Sita sasa.

Wapiga Kura wa upande wa Tanzania Bara waliokuwa chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi {NEC} wamewajibika kupiga kura kwa nafasi Tatu za Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ubunge na Udiwani wakati wale wa Zanzibar wamepiga Kura kwa nafasi Tano za Urais wa Muungano, Ubunge, Urais wa Zanzibar, Uwakilishi pamoja na Udiwani.

Moja kati ya jambo lililoleta faraja ndani ya vituo vya Wapiga Kura Mjini na Vijijini ni ile hali ya Amani na usalama iliyotanda ambayo ilikuwa ikisisitizwa kulindwa na kudumishwa wakati wa Kampeni za Uchaguzi zilizochukuwa takriban Siku 61 kwa Tanzania Bara na Siku 45 kwa upande wa Zanzibar.

Maelfu ya Wananchi pamoja na Viongozi wa Kitaifa, Waandamizi wale wa Kiserikali na Vyama vya Siasa wamejitokeza mapema asubuhi kupiga Kura na kutimiza ile kiu yao iliyowashika tokea kuanza kwa zoezi la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,Kura za Maoni, Kampeni hadi upigaji kura wenyewe.

Misururu mirefu ya Wananchi iliyowekwa kwa mujibu wa mfumo wa Majina ya Wapiga Kura ilianza mapema alfajiri mara tu baada ya wale waumini wa Dini ya Kiislamu kutoka Misikitini Ibada ya sala la Asubuhi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi walitumia Haki yao ya Kidemokrasia ya Kupiga Kura katika Kituo chao kiliopo Skuli ya Sekondari ya Kitope Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja mnamo saa 3.00 Asubuhi.

Balozi Seif Ali Iddi mwaka huu ameamua kustaafu kugombea Nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo lake la Mahonda baada ya kulitumikia kwa kipindi cha Miaka Mitano kwa Tiketi ya Chama cha Mapinduzi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kupiga Kura Balozi Seif Ali Iddi alisema zoezi zima lililoanza mapema asubuhi limempa faraja  kutokana na utulivu uliotanda Vituoni ambapo Wananchi mbali mbali wameshatumia haki yao ya kupiga kura na kurejea Nyumbani kuendelea na shughuli zao za kila Siku.

Alisema Serikali kupitia Vyombo vyake vya Dola vitaendelea kulinda usalama wa Wananchi na pale itakapobaini ishara au dalili za uvunjiufu wa Amani haitasita kuwashughulikia mara moja wale wote watakaohusika na vurugu zozote bila ya kujali cheo cha Mtu au Kiongozi.

Balozi Seif aliendelea kuwatahadharisha Wanasiasa wenye uchu wa madaraka kujiepusha na kitendo cha kujitangazia Ushindi, kwani jukumu hilo linasimamiwa na Mamalaka zilizopewa dhamana kwa mujibu wa shaeria ambazo ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } na ile ya Taifa ya Tanzania {NEC }.

Makamu wa Pili wa Zanzibar alibainisha kwamba Kiongozi ndie mwenye dhamana ya kumsimamia Mwanachana au Mwananchi wake mahali popote pale wakielewa kwamba huo ndio wajibu wao wa kuhakikisha Maisha ya Jamii yanaendelea kubakia salama na Amani.

Mmoja kati ya Wapiga Kura katika Kituo cha Skuli ya Sekondari cha Kitope ambae alikataa kutaja jina lake alisema ameridhika na maandalizi mazima yaliyofanywa na Tume zote mbili za Uchaguzi Tanzania Bara na Zanzibar na kuwapa fursa Wananchi kutekeleza haki yao katika misingi ya utulivu na bila ya usumbufu.

Alisema Mtu atakayefikia maamuzi ya kutaka kuzilaumu Tumeza Uchaguzi ajijue kwamba ana mapungufu ya akili kwa vile fursa iliyotolewa mapema kwa Wananchi kuangalia majina yao kwa karibu siku Nne kabla ya Uchaguzi na kupewa nafasi ya kutoa Taarifa ili afanyiwe marekebisho endapo jina lake hakuliona.

Katika kuimarisha misingi ya Sheria, Utawala Bora na Demokrasia Tanzania imeridhia kuingia katika mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vyingi vya Kisiasa vugu vugu  lake lilianzia mnamo Mwaka 1992 na Uchaguzi wa mwanzo ukaanza Mwaka 1995.

Uchaguzi huo wa Vyama vingi vya Kisiasa ulimuwezesha Dr. Salim Amour wa Chama cha Mapinduzi kuongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka Mitano na kwa upande wa Tanzania Marehemu Bendjamin William Mkapa akashika kijiti cha Kuiongozi Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo yeye alibahatika vipindi viwili vya Miaka Mitano Mitano.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.