Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Ali Mohamed Shein Shein Amewataka Wananchi Kujitokeza Kwa Wingi Kupiga Kura.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,.Dk.Ali Mohamed Shein akipiga kura yake katika Kituo cha kupigia kura cha Skuli ya Bungi Wilaya ya Kati Unguja, wakati wa  zoezi la upigaji kura kwa Tanzania nzima uliofanyika leo 28/10/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka na wala wasiwe na hofu kwani Serikali yao imewawekea ulinzi wa kutosha.

Hayo aliyasema leo wakati alipofanya mahojiano na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali mara baada ya kumaliza zoezi la kupiga kura huko katika kituo cha kupiga kura Bungi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo Rais Dk. Shein alitimiza haki yake hiyo ya msingi mapema subuhi mnamo majira ya saa mbili kasorobo.

Rais Dk. Shein alifika kituoni hapo akiwa amefuatana na mkewe mama  Mwanamwema Shein na mara baada ya kufika wote kwa pamoja walifuata taratibu zote za kupiga kura wakiwa wameanza kwa kupanga foleni katika mistari maalum iliyopangwa.

Katika mahojiano hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa yeye amepiga kura na kuchukua muda mfupi sana kutokana na taratibu zilizopangwa na kuwataka wananchi kwenda mapema ili na wao wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka baada ya kusikiliza kampeni za vyama vya siasa na kueleza imani yake kwamba anaamini tayari wameshafanya uamuzi.

Alisisitiza kwamba hali ya ulinzi ni nzuri na hali iko shuwari sana hivyo waliwataka wananchi wasiwe na hofu na wala wasiogope kwani leo ndio siku yao ya kufanya maamuzi wanayoyataka.

Aliongeza kuwa wananchi hawatakiwi kuwa na hofu kwani wako nchini mwao na wako huru na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Serikali yao kwani wana wajibu wa kuwachagua  viongozi wengine wapya baada ya wao kumaliza madaraka.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mtu hatakiwi kuwa na hofu wakati akiwa nchini mwake kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imewathibitishia wananchi kwamba imewawekea  ulinzi wa kutosha.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kutochelea kwenda kupiga kura na kuwasisitiza kwamba waende wakapige kura kwa azma ya kutekeleza jukumu lao la msingi huku akisisitiza kwamba ni lazima kila mmoja aende akachague kiongozi anaemtaka.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi waende kupiga kura na wasiwe na dhana zaidi kuliko ukweli na kuwataka wasisikilize hadidthi nyengine zisiso na ukweli kuhuhusu ukweli uliopo.

“Isijefika wakati mtu akaja kujuta na kubaki akisema mimi sikwenda ninge ninge, ningejua, kwani ninge haiisaidii na badala yake waende katika vituo vyao wakapinge kura”, alisisitiza Dk. Shein.

Akitoa nasaha zake kwa mgombea atakaeshinda, katika nafasi zote zinazogombewa, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa mgombea kuzingatia katiba ya nchi kwani nchi hii inaongozwa kwa Katiba, Sheria na taratibu zilizowekwa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.