PICHA NA FAUZIA MUSSA /MAELEZO ZANZIBAR.
NA MIZA KONA MAELEZO/ZANZIBAR
WAZIRI WA Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka wanafunzi waliomaliza kada ya Uuguzi na Ukunga kuyatekeleza kwa vitendo mafunzo waliyoyapata kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Syrus Castico katika hafla ya Kuwaaga wanafuzi walinaomaliza Kada ya Uuguzi na Ukunga wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba huko Ukumbi wa SUZA Vuga,
Amesema wauguzi na wakunga wana umuhimu mkubwa kwa jamii katika kutoa huduma ya Afya na kuwa watetezi wakuu kwa wanawake na watoto katika kupinga vitendo vya udhalilishaji.
Amewasisitiza kufuata kanuni za maadili ya uuguzi na Ukunga kwa kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa na kutoa mashirikiano na upendo katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ili kuweza kutoa huduma nzuri na kupata mafanikio katika fani yao hiyo.
Waziri Castico amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kukiunganisha na kukipa hadhi Chuo cha Afya kuwa na hadhi ya chuo Kikuu cha Taifa pamoja na kutekeleza kwa vitendo shabaha ya Mapinduzi ya kutoa elimu kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.
aidha Waziri huyo alimkabidhi zawadi maalum Mhadhiri Mkuu Idara ya Ukunga na Uuguzi Dk.Rukia Rajab Bakar mara baada ya kuhitimu masomo yake katika ngazi ya uzamivu wa Afya ya jamii.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo wa hicho Dk. Zakia Mohamed Abubakar amesema fani ya uuguzi na ukunga ni sekta inayohitajika sana katika kuboresha maisha ya wananchi na kupata Taifa bora na lililoimara.
Mapema Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Profesa Amina Abdulkadir amewahimiza wahitimu hao kufuata sheria na maadili ya fani hiyo katika kutekeleza majukumu yao ili kupata mafaniko na maendeleo zaidi.
Ameeleza mashirikiano ya pamoja baina ya wauguzi wa zamani na waliopata eluimu ya sasa ndio yatayoweza kusaidia kukuza taaluma hiyo na kuboresha utoaji mzuri wa hudunma
“Tunawapima wanafunzi wetu kwa kutumia H 3, H ya kwanza ni kichwa na H ya pili ni Mikono na H ya tatu ni moyo. Hizi H tatu mkizitumia vizuri mtafanikiwa katika kuwahudumia wagonjwa na kutoa huduma kwa upendo na uadilifu”, alifahamisha Bi Amina.
Bi Amina amewasisitiza wahitimu hao kujiendeleza kielimu kwa dhamira ya kupata ujuzi zaidi ili kuweza kufanyakazi kwa ufanisi mkubwa katika kuimarisha huduma ya afya nchini.
Akisoma risala mwanafunzi Rashid Hilal Mohamed amesema wanakabiliwa na changamoto ya kukosa wasimazi kutoka chuoni wanapokwenda kujifunza kwa vitendo katika vituo vya afya kwani wafanyakazi wa vituo hivyo hukabiliwa na majukumu yao mengine jambo linalopelekea kukosa maelekezo mazuri ya vitendo.
Aidha wameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuwafundisha na kuwapa mafunzo mazuri na kupata mafanikio katika fani yao hiyo na kuweza kufaulu bila ya usumbufu.
No comments:
Post a Comment