Habari za Punde

Wananchi Waingie Katika Utaratibu wa Kuuza Biashara Kwa Njia za Kisasa Zaidi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akikata utepe kulifungua Jengo Jipya la Maduka ya Kisasa la Michezani Mall leo 5/10/2020, akiwa na Viongozi mbalimbali (kushoto kwke) Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Mhe.Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa cRais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, Rais Mstaaf wa Tanzania Mhe.Ali Hassan Mwinyi na Mkurugenzi Muendeshaji wa ZSSF.Bi. Sabra Issa Machano na (kulia kwa Rais) Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa, wakiwa wameshika utepe wakati wa hafla hiyo ya ug\ufunguzi wa Michezani Mall leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali imejenga  jengo la biashara la “Michenzani Mall” ili wananchi waingie katika utaratibu wa kuuza biashara kwa njia za kisasa zaidi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa jengo jipya la biashara la “Michenzani Mall”, liliopo Michezani Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia, ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Katibu Mkuu wa CCM Taifa Bashiru Ali Kakurwa na viongozi wengine  wa ndani na nje ya Zanzibar pamoja na wananchi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa majengo ya biashara kama hayo hayajengwi kwa ajili ya shughuli za kuuza na kununua vitu peke yake bali yanajumuisha huduma mbali mbali za kijamii zinazohusiana na elimu, afya, urembo, manukato, burudani na kadhalika.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa ndani ya jengo hilo mna maduka, sehemu za mazoezi ya viungo, sinema, sehemu za kucheza kwa watoto na shughuli kadhaa za kijamii ukiwemo ukumbi wa harusi na chumba maalum kwa kumpambia bi harusi, mikahawa, sehemu za vyakula na vinywaji, saluni za nywele na sehemu nyenginezo.

Aliongeza kuwa eneo hilo kabla palijaa makontena ya biashara ambayo hayakuwa na mpangilio maalum ndipo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba ilipofikiria kuwawekea wananchi wake mazingira bora ya ya kuvutia ya kufanya biashara.

Rais Dk. Shein alisema kuwa sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi na sekta hiyo ina uwiano mkubwa na sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo huunganisha watu kutoka vijijini na mijini, kanda za Kitaifa na Kimataifa.

Kutokana na hilo, ndio maana Serikali yake anayoiongoza ya Awamu ya Saba iliivalia njuga kazi ya uimarishaji wa sekta hio ya ujenzi kwa kuongeza ujenzi wa barabara mpya na kuzifanyia matengenezo zile ambazo zilikuwepo.

Akieleza historia ya biashara hapa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisema kuwa katika kujitafutia maisha kabla ya Mapinduzi wananchi wa Zanzibar hawakuwa na fursa za kumiliki biashara kubwa kwa sababu biashara za aina hio zilihodhiwa na mabepari.

“Majengo kama haya ya biashara tunayakuta katika nchi za wenzetu na yameanza zamani tangu 1922 kule Marekani katika jiji la Kansas na likiitwa “Country Plaza”, alisema Dk. Shein

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba kwa wale wote waliokuwa wakifanya biashara katika eneo hilo kabla ya kujengwa jengo hilo jipya watapewa kipaumbe katika maombi ya kuomba kufanya biashara katika eneo hilo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kwa kutoa wito kwa vijana kuitumia fursa hiyo kwa kujipanga, kutafuta utaalamu wa kuandaa miradi yenye tija na kuitumia fursa ya uwepo wa “Mall” hiyo kwani tayari Serikali imeshawaandalia mazingira mazuri ya kuwepo kwa Mfuko wa uwezeshaji utakaowakopesha fedha ili wafanye biashara waitakayo.

Hivyo, Rais Dk. Shein alirejea usemi wake wa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwataka baadhi ya vijana ambao kwao wao kazi ni za kuajiriwa serikalini tu kuachana na mawazo hayo na badala yake wajitume na Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Rais Dk. Shein alisema kuwa katika kipindi hichi cha wiki mbili zilizopita amekuwa akifungua miradi mikubwa mbali mbali hapa Zanzibar ambapo matukio yote hayo yana maana kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na nchi kwa jumla ambapo pia, ni kielelezo halisi cha  Mapinduzi Matukufu ya Januri 12, 1964.

Rais Dk. Shein pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  ya kutekeleza mradi unaojulikana kwa jina la “BIG-Z” (Boosting Inclusive Growth for Zanzibar-Integrated Development Project), ambao Serikali kupitia Wizara ya Fedha itashirikiana na Benki ya Dunia kuufanikisha katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa wa miaka 5 hadi 7 na lengo lake kuu ni kuimarisha mazingira ya maeneo hayo na kushajiisha ushirikishaji wa kijamii na kiuchumi ambapo miongoni wma shughuli hizo ni uhuishaji wa eneo la mji wa Zanzibar (Michenzani Green Corridor).

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza Kampuni ya CRJE kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa kazi nzuri walioifanya ambayo imeonekana pamoja na kumshukuru na kumpongeza Mshauri Muelekezi wa ujenzi huo  Kampuni ya “Arques Africa ya Dar es Salaam kwa kuusimamia vizuri ujenzi huo huku akiupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na ZSSF kwa hatua hiyo nzuri ya maendeleo iliyofikiwa.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alieleza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 katika ukurasa wa 203 ilipoeleza hatua za kuimarisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii(ZSSF), ili uendelee kuekeza katika miradi mbali mbali ya kiuchumi inayozalisha faida kubwa na kukuza mapato ya mfuko huo.

Alieleza kuwa kati ya miradi hiyo ni ujenzi wa “Michenzani Mall”, ambapo alisema kuwa katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Dk. Shein (ZSSF) imewekeza miradi 12 mikubwa pamoja na miradi mengine midogo midogo ambayo yote hiyo imegharimu TZS Bilioni 140 huku akesema kuwa maendeleo yote hayo yamefanywa chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa alisema kuwa baada ya kukamilika kwa michoro mnamo tarehe 30 Aprili 2018 ilitolewa zabuni kumtafuta mkandarasi ambapo jumla ya wazabuni 28 walijitokeza na baada ya tathmini Kampuni ya CRJE kutoka China ilishinda zabuni hiyo na kupelekea kutiwa saini Mkataba wa ujenzi baina ya ZSSF na CRJE tarhe 4 mwezi Oktoba, 2018 kwa gharama ya TZS Bilioni 27.9.

Alisema kuwa ujenzi ulianza rasmi tarehe 23 Novemba  2018 na ulitarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 hadi kufikia 30 Juni 2020 hata hivyo kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kuibuka kwa maradhi ya COVID-19 mradi uliongeza muda.

Alisema kuwa kama zilivyo “Malls”,  ngenine duniani “Michenzani Mall” inatoa fursa kwa kufanyika biashara ya kisasa ya rejareja na huduma nyengine zinazoendana na mahitaji ya mtu kutumia muda mwingi katika jengo hilo ambalo lina ghorofa kati ya 5 na 7 kwa kuzingatia ghorofa ya chini ya ardhi na sehemu mbili za pembeni mwa jengo.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ZSSF iliamua kuwa kazi ya ukodishaji wa sehemu za jengo hilo ifanywe na Kampuni yenye uzoefu hivyo ilitangaza zabuni na kufanikiwa kuipata Kampuni ya Knight Frank (T) LtD ambayo pia ina uzoefu wa shughuli hizo kwa soko la Zanzibar.

Pamoja na kutumia Kampuni ya ukodishaji, wafanyabiashara wanaotarajia kupata nafasi katika jengo hilo ni mchanganyiko wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wageni na wazawa ambapo pia, Katibu Mkuu huyo alirejea ahadi ya Rais Dk. Shein ya wafanyabiashara wa Makontena waliokuwepo awali katika eneo hilo wapewe kipaumbele.

Sambamba na hayo, wafanyabiashara wapya ambao tayari wamejitokeza kukodi sehemu katika Mall hiyo ni pamoja na Kampuni ya GSM inayoendesha maduka maarufu ya Max, Baby Zone, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki ya Afrika, Horizon Pharmacy na Shamshu Phamacy, huku ZSSF ikiendelea na uchambuzi wa maombi mengine.

Aliongeza kuwa ZSSF inadhamiria kutekeleza nia yake ya kujenga jengo la kisasa la maegesho ya gari litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaokuja kuuza au kununua katika jengo hilo ambapo jengo hilo linatarajiwa kuwa la ghorofa tatu ambazo zote zitatumika kwa ajili ya maegesho na litakuwa na uwezo wa kuchukua gari 150 kwa wakati mmoja.

Mapema Rais Dk. Shein mara baada ya kulifungua na kukata utepe wa jengo hilo alipata fursa ya kulitembelea akiwa ameongozana na viongozi mvali mbali wa Kitaifa.  

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.