Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed akagua eneo litakalojengwa Ofisi za SMZ Dodoma

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah akifanya ziara Maalum ya kutembelea eneo lililokabidhiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Kujenga Ofisi zake katika eneo la Mji Mpya wa Mahoma Makulu  Kilomita takriban 17 nje kidogo ya Jiji la  Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amran akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed alipofanya ziara kulikagua eneo la SMZ la kujenga Ofisi za Taasisi zake Mji Mpya wa Dodoma.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah akitoa Wiki Moja tu kwa Taasisi za Ujenzi, Mipango Miji na Ardhi kukamilisha utaratibu kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Taasisi za SMZ Mkoani Dodoma alipolitembelea eneo la SMZ.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah ametoa Wiki moja kwa Taasisi za Ardhi, Mipango Miji  pamoja na Wakala wa Ujenzi Zanzibar kukamilisha utaratibu utakaowezesha kuanza kwa ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali katika Mji Mpya wa Dodoma.

Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuanza kwa Ujenzi wa Ofisi zake ikianzia ile ya Uratibu wa Shughuli za Serikali iliyopo Jijini Dar es salaam ihamie Dodoma ndani ya kipindi kifupi.

Mh. Hemed Suleiman Abdallah alitoa agizo hilo  wakati alipofanya ziara Maalum ya kutembelea eneo lililokabidhiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Kujenga Ofisi zake katika eneo la Mji Mpya wa Mahoma Makulu  Kilomita takriban 17 nje kidogo ya Jiji la  Dodoma.

Alisema Watendaji wa Taasisi hizo wanapaswa kuanza Kazi hiyo mara moja kwa vile baadhi ya Miundombinu kwenye eneo hilo la Mji Mpya imeanza kutekelezwa ikiwemo Miundombinu ya Bara bara, Huduma za Umeme ikifuatiwa na Miundombinu ya Maji hapo baadae.

Alitahadharisha kwamba wale watendaji waliopewa jukumu la kusimamia maelekezo yote yanayokuwa yakitolewa na Serikali lazima yatekelezwe ipasavyo na kwa wakati.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah ameelezea kufurahishwa kwake na Eneo zuri na kubwa iliyopatiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Taasisi zake mbali mbali.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amran alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba eneo hilo lina ukubwa wa Hekta 33.

Nd. Khalid alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pekee ilipatiwa eneo hilo  kama ilivyopeleka maombi  kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyozingatiwa katika hatua zote za maamuzi.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kuhamishia Makao Makuu ya Shughuli za Serikali Mkoani Dodoma kati kati ya ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania uamuzi uliokwenda sambamba na kuzingatia wazo la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilolitoa mwanzoni mwa miaka ya 60.

Kikosi Kazi cha kuhamia Dodoma tayari kimeanza kuwajibika  mara tu baada ya Rais wa  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kutangaza shughuli za Serikali zihamie Dodoma Mnamo Tarehe 25 Julai Mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.