Habari za Punde

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waendelea na semina elekezi
 


Watumiaji wa huduma za kibenki wameshauriwa kupata ushauri wa kitaalamu  kabla ya kuingia katika mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi ambayo haitakuwa na tija kwao wao na  badala yake kuingia katika hasara.

Wakitowa mada juu ya huduma na fursa mbali mbali zinazopatikana katika benki katika semina elekezi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi inayofanyika huko  Baraza hilo Chukwani, wawakilishi kutoka Benki za CRDB, NMB na PBZ wamesema baadhi ya wateja wa benki wamekua wakiingia  katika hasara kwa kuchukua mikopo mikubwa kwa ajili ya miradi ambayo hawakupata ushauri wa kitaalamu wa kifedha na miradi hiyo.

Wamesema  ili kujikinga na tatizo hilo, taasisi hizo za kifedha zimejipanga kwa ajili ya kutoa taaluma kwa wateja na hatimae kuwapatia mikopo mbali mbali itakayoleta tija kubwa kwao na hatimae kujikwamua na hali ngumu ya maisha pamoja na kutengeneza ajira na kuondokana na umasikini miongoni mwa jamii.

Wawakilishi hao wa taasisi za fedha wamesema wako tayari kwenda sambamba na azma ya kasi ya  serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuimarisha huduma zao mijini na vijijini.

Wakati huo huo wawakilishi hao wa Mabenki wamewaomba wateja wao kuwatumia mawakala walio mitaani ili kupunguza msongomano unajitokeza hasa mwisho wa mwezi katika benki ziliopo hapa nchini.

Nao wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamezishauri taasisi hizo za kifedha kuzitumia fursa ziliopo ili kuongeza mitaji na Biashara kwani  hivi sasa taasisi hizo zimekuwa ndio kimbilio la wanyonge.

Mafunzo hayo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yataendelea tena hapo kesho ambapo kutawasilishwa mada mbali mbali ikiwemo mbinu za uwasilishaji na ushiriki katika mijadala, Dhana ya uwajibikaji wa Serikali mbele ya Baraza la Wawakilishi  na Taratibu za Maswali na Majibunkatika Baraza la Wawakilishi.

 

Imetolewa na Divisheni ya Itifaki na Uhusiano, BLW

November 13, 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.