Habari za Punde

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli Azindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma leo

 

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akilihutubia Bunge la 12 la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma leo, wakati wa Uzinduzi wa bunge hilo uliofanyika katika ukumbi wa Bunge.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amemuahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwiyi kwamba miaka mitano ijayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa wakati akilifungua rasmi Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alihudhuria.

Kabla ya kuanza hotuba yake Rais Dk. Magufuli aliwasihi wote waliohudhuria hafla hiyo kusimama kwa ajili ya kumkumbuka Rais wa Jamhuri ya Muungano Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Wilium Mkapa pamoja na Wabunge wote waliofariki dunia tangu kufungwa kwa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli alieleza kuwa Serikali zote hizo mbili zitafanya kazi wka pamoja kwa lengo la kuleta maendeleo kwa pande zote mbili za Muungano.

Na kwa hilo alimpongeza Dk. Hussein Mwinyi  kwa hotuba nzuri aliyoitoa wakatiw a kuzindua  Baraza la Wawakilishi  ambapo katika hotuba hiyo alitoa dira, mwelekeo na kutaja vipaumbele vya Searikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar.”Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa hotuba nzuri”,alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli kupitia Bunge hilo alimuahidi Rais Dk. Hussein Mwinyi kwua atampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza yote aliyoyaahidi wakati wa Uzinduzi Rasmi wa Baraza la Wawakilishi.

Rais Magufuli alieleza kwamba jambo la kwanza na muhimu atakalolipa kipaumbele kikubwa kwenye miaka mitano ijayo ni kuendelea kulinda na kudumisha tunu za Taifa akikusudia kuwa ni amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi, Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Na katika hilo aliahidi kushirikiana kwa karibu sana na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi na kamwe hawatokuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi, mwenye nia ya kutaka kuvuruga umoja na mshikamano na pia mwenye kutaka kutishia uhuru, Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo alitoa shukurani kwa wananchi wa Tanzania kwa kushiriki vizuri na kuonesha utulivu mkubwa kwenye Uchaguzi mkuu uliopita kuanzia kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura, wakati wa kampeni, upigaji kura na kupokea matokeo.

Alisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu umeuthibitishia ulimwengu kuwa Watanzania ni wapenda amani kwani wanajitambua na hawadanganyiki na wamekomaa kidemokrasia.

Katika hotuba yake hiyo alimpongeza Spika wa Bunge Job Ndugai Mbunge wa Jimbo la Kongwe kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge hilo akiwa Spika pamoja na kumpongeza Naibu Spika Dk. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa mara nyngine tena kuwa Naibu Spika na mara hii akitokea Jimboni katika Jimbo la Mbeya Mjini.

Rais Magufuli katika pongezi zake alisema kuwa Serikali anayoiongoza na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina waamini sana wanawake hivyo, Serikali itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha, aliwashukuru Wabunge wa Bunge hilo kwa kuridhia na kumpitisha Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Magufuli pia, alitumia fursa hiyo kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutumia Bilioni 262 tu kati ya Bilioni 331 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu hasa ikizingatiwa kwamba uchaguzi wa mwaka huu umegharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli katika hotuba yake hiyo alisema kwamba sambamba na kulinda na kudumisha tunu  za nchi kwenye miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuimarisha Utawala Bora, hususan kwa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma pamoja na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Alisema kwamba kwenye miaka mitano iliyopita walichukuliwa hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha nchi kushika nafasi ya wkanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa kwa mujibu wa “Transparency International”.

Aliongeza kuwa pia, Tanzania ilishika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa Utafiti wa Jukwa la Dunia wa mwaka 2019.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba watumishi wazembe bado wapo, walarushwa bado wapo hivyo kwenye miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kushughulikia matatizo hayo huku akieleza kwamba utumbuaji majipu utaendelea.

Hata hivyo, kwa upande mwngine alieleza kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania na kuwataka watumishi wasiwe na wasi wasi.

Alieleza kwamba kwenye miaka mitano ijayo Serikali imejipanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi kama juhudi zilivyochukuliwa katika kuusimamia uchumi huo ambao ulikuwa kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka .

Alisema kwamba mafanikio hayo ndiyo yaliyowezesha mwezi Julai mwaka 2020 Tanzania ikatangazwa kuingia kundi la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi masikini.

Rais Magufuli alieleza kwamba mbali na hatua hizo kwa lengo la kukuza uchumi, kupambana na umasikini na pia kukabilia na tatizo la ukosefu wa ajira, Serikali inakusudia kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta kuu za uchumi na uzalishaji, hususan kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, biashara na utalii.

Alisema kuwa sekta hizo ndizo zenye kuajiri watanzania wengi kwa hivyo ni wazi kwamba Serikali ikifanikiwa kuzikuza uchumi utakuwa kwa kasi na hivyo kupunguza matatizoya umasikini na ukosefu wa ajira nchini.

Nao wabunge walimpongeza Rais Magufuli kwa hotoba yake nzuri na kuleza kwamba wataifanyia kazi. Bunge hilo linatarajiwa kurudi tena Februari 2 mwakani.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, Makamo wa Rais Mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilali, Mawaziri Wakuu Wastaafu, wake wa viongozi wakitaifa, viongozi wa vyama vya siasa, Babalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na wengineo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.