Habari za Punde

Ofisi ya Mufti Zanzibar kupanua wigo wa mafunzo ya ndoa kufikia Wilaya

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume akieleza azma ya Ofisi ya Mufti kupanua mafunzo ya ndoa hadi ngazi ya Wilaya wakati wa kufunga mafunzo ya ndoa mkupuo wa saba yaliyofanyika Masjid Jaamii Zinjibar Kiembe Samaki
Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo ya ndoa wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mafunzo hayo katika Msikiti wa Masjidi Jaamii Zinjibar Kiembe Samaki
Muhitimu wa mafunzo ya ndoa, Fatma Humoud Abdalla akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, wameahidi kutekeleza kwa vitendo mafuzo waliyopata ili ndoa zao ziweze zidumu milele.
 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, ambae alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo ya miezi mitatu ya ndoa, akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu Abdulrauf Jaffar katika hafla iliyofanyika Masjid Jammy Zinjibar Kiembesamaki.
 Baadhi ya maharusi wa kike watarajiwa walioshiriki mafunzo ya ndoa ya miezi mitatu wakiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid baada ya kuwakabidhi vyeti vya kumaliza mafunzo yao.

 Baadhi ya maharusi wa kiume watarajiwa walioshiriki mafunzo ya ndoa ya miezi mitatu wakiwa katika picha ya pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi  Zubeir Ali Maulid baada ya kuwakabidhi vyeti vya kumaliza mafunzo yao.

Picha na  Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar.


Na Khadija Khamis –Maelezo 16/11/2020.

 

Ofisi ya Mufti Zanzibar inatarajia kupanua mafunzo ya ndoa kufikia ngazi ya Wilaya ili kutoa nafasi zaidi ya wanandoa kushiriki mafunzo hayo.

 

Hayo ameyaeleza na Katibu wa Mufti Khalid Ali Mfaume huko katika Msikiti wa Jamiy Zinjibar Mazizini Unguja wakati wa ufungaji wa mafunzo ya ndoa katika mkupuo wa saba uliomalizika.

 

 Alisema ifikapo Disemba mwaka huu mafunzo mapya yanatarajiwa kufunguliwa katika Wilaya ya Kaskazini “B “na kuendeleza kutoa mafunzo hayo sehemu zote za Unguja na Pemba hatua kwa hatua .

 

Alisema mafunzo ya  ndoa kwa vijana yanasaidia kuwapa uwelewa wa mambo mbalimbali yenye muongozo wa kidini jambo ambalo huimarisha heshima katika ndoa zao .

 

Aidha alisema lengo la mafunzo hayo ni kuweza kudhibiti talaka ambazo zinatolewa kiholela ikiwemo za talaka za kutundika jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa elimu ya ndoa .

 

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid wakati akikabidhi vyeti vya wahitimu wa mafunzo ya ndoa alisema kukosekana kwa mafunzo ya ndoa huchangia migogoro katika familia na kutelekeza wanawake na watoto.

 

Alisema umuhimu wa mafunzo hayo kwa vijana kutasaidia kuepusha migogoro katika familia, utoaji wa  talaka pamoja udhalilishaji wa wanawake na watoto.

 

Aidha alisema kuwa ameridhishwa na idadi kubwa ya vijana ambao wamejitokeza kupewa mafunzo hayo, jambo ambalo litasaidia kudhibiti ndoa zao kuwa na upendo na furaha .

 

“Amani na utulivu kwa wana ndoa ni muhimu katika nyumba iwapo nyumbani hakuna amani na kazini pia amani hutoweka,” alisema Spika .

 

Spika huyo ameitaka Ofisi ya Mufti kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa vijana wazanzibar ili kupunguza ongezeko la talaka nchini.

 

Katika risala yao iliosomwa na Fatma Humoud Abdallah waliiyomba serikali kuwazidishia muda wa masomo hayo kwani muda uliopo wa wiki 10 hautoshelezi kutokana na baadhi ya mada zinazotolewa ni kubwa na zinahitaji umakini.

 

Hata hivyo walisema wameridhishwa na mafunzo walioyapata ambayo yamewajengea uwezo wa kufahamu umuhimu wa maisha ya ndoa na changamoto zake jambo ambalo litawasaidia katika kujenga upendo na kudumisha ndoa zao.

 

Jumla ya wanafunzi 108 wamekabidhiwa vyeti katika halfa hiyo na hivi sasa tayari wanafunzi wapya 146 wanaendelea na mafunzo kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.