Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amepokea Salamu za Pongezi Kutoka kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud bin Saqr Al -Qasimi.

 
SALAMU za pongezi zimendelea kutolewa na viongozi mbali mbali wa ndani na nje ya nchi kufuatia ushindi mkubwa wa Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alioupata Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kufuatia uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni hapa nchini.

Salamu za pongezi za hivi karibuni zimetolewa na Mtawala wa Ras Al Khaimah, Sheikh Saud bin Saqr Al- Qasimi.

Katika salamu hizo Sheikh Saud bin Saqr Al-Qasimi alimpongeza Rais Dk. Hussein kwa ushindi huo mkubwa alioupata katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu 2020.

Kutokana na ushindi huo mkubwa alioupata Rais Dk. Hussein, Sheikh Saud bin Saqr Al-Qasimi aliuelezea kuwa ni wa mafanikio makubwa yanayotokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake wote.

Hivyo, Sheikh A-Qasimi alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba Ras Al Khaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Nae Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa upande wake alitoa shukurani zake za dhati baada ya kupokea salamu hizo kutoka kwa kiongozi huyo wa Rais Al Khaimah na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake inazisamini na itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alimpongeza kiongozi wa Oman Sultan Haitham Bin Tariq Al Said pamoja na wananchi wake kwa kusherehekea siku ya Uhuru wa Taifa hilo.

Aidha, katika salamu hizo Rais Dk. Hussein alimuhakikishia kiongozi huyo wa Oman kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Oman sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa Oman na wananchi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa siku hii adhimu inaendelea kutoa nafasi zaidi ya mashirikiano kati ya pande mbili hizo pamoja na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Oman katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimtakia heri, mafanikio, afya njema na maisha marefu  kiongozi huyo wa Oman pamoja na wananchi wake wote sambamba na kukuza na kudumisha amani na maendeleo yaliopatikana nchini humo.

Oman ilipata uhuru wake kutoka ukoloni wa Kireno mnamo Novemba 18 mwaka 1660 chini ya kiongozi na muasisi wa Taifa hilo Iman Sultan Bin Saif Bin Malik Al Yarubi ambaye alisimamia kung’oka kwa koloni hilo kutoka nchini Oman pamoja na bandari zote za nchi hiyo zilizokuwa chini ya Utawala wa Kireno.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.