Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam Katika Sala ya Ijumaa Masjid Nunge Jijini Dodoma leo 6/11/2020.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiisalam Jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa katika Masjid Nunge Dodoma leo 6/11/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwiyi amesema kuwa uchaguzi umekwisha na umemalizika kwa salama na kilichobaki hivi sasa ni kuendelea kuidumisha na kuilinda amani iliyopo nchini.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo mara baada ya sala ya Ijumaa katika Masjid Nunge Jijini Dodoma wakati alipokuwa akiwasalimia Waislamu msikitini hapo mara baada ya kumalizika sala hiyo ya Ijamaa.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Hussein aliwataka wananchi wote kuendelea kuidumisha na kuilinda amani kwani bila ya amani hakuna kitu kinachoweza kufanyika.

Aliongeza kuwa katika hatua iliyopo hivi sasa ni muhimu amani iwe kitu cha mwanzo na kusisitiza kwamba mustakabali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unategemea amani kwa kiasi kubwa.

Alieleza kwamba mara zote binaadamu hajui umuhimu wa kitu hadi pale kinapomuondoka akimaanisha haja ya kuilinda na kuidumisha amani iliyopo hivi sasa ili isipotee huku akitolea mfano wa mwanaandamu anapokuwa na afya na pale anapoikosa.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza kwamba amani haijaribiki hivyo, alikemea viashiria vidogo vidogo vya kuvuruga amani iliyopo na kuwataka wananchi kuidumisha amani iliyopo na kutovipa nafasi viashiria hivyo.

Akitolea mfano wa baadhi ya nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu kama vile Yemen, Somalia, Syria na Iraq ambako amani imeondoka hivi sasa na kupelekea wananchi wake kutoishi vizuri pamoja na kukosa hata muda wa kufanya ibada.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani kwa Waumini wa Msikiti huo kwa kumuombea dua kwa wingi wakati wa mchakato wa kampeni za uchaguzi ambapo Mwenyezi Mungu amezikubali dua zao hizo.

Akitoa shukurani hizo, Alhaj Dk. Hussein alisema kwamba awamu ya kwanza ya kugombea nafasi ya uongozi imeshafanyika na Allah ameshaleta rehema za ushindi na lilolobaki hivi sasa ni kuwatumikia wananchi.

Hivyo, aliwataka Waumini hao waendelee kumuombea dua ili aweze kuwahudumikia wananchi kwa haki, upendo, umoja na mshikamano mkubwa.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi aliwaeleza waumini hao kwamba hana cha kuwalipa ila ataendelea kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu na kueleza furaha yake kwa kupata fursa hiyo ya kutoa salamu msikitini hapo huku akieleza kwamba historia zinaonesha kwamba Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikuwa akipewa fursa ya kusalisha msikitini hapo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.