Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed akutana na Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara Tanzania {NMB}

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara Tanzania {NMB} Ofisini kwake Vuga.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara Bibi Ruth Zaipuma akielezea malengo ya Benki yake ya kuunga mkono maono ya SMZ katika kuimarisha Uchumi wa Buluu.
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akipokeas zawadi Maalum kutoka kwa Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara Tanzania {NMB} mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara.

 Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara Bibi Ruth Zaipuma akimuaga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla mara baada ya kumaliza mazunguimzo yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Wananchi wamepata moyo mkubwa kutokana na Taasisi za Kifedha Nchini kuunga mkono maono ya Serikali katika muelekeo wake wa kustawisha Maisha ya Jamii hapa Nchini.

Alisema Taasisi nyengine zinazojihusisha na masuala ya Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi bado zina fursa za kujitokeza katika utayari wao wa kushirikiana na Serikali kwenye azma ya kuimarisha Uchumi wake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema hayo hapo Afisini kwake Vuga wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Juu wa Benki ya Taifa ya Biashara Tanzania {NMB} ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake Bibi Ruth Zaipuma ulipofika kumpongeza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata moyo mkubwa kutokana na mfumo mpya wa Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara katika kuwajengea uwezo wa kujiendesha kiuchumi Wananchi wanaojishughulisha na ujasiri amali katika Sekta ya Uvuvi, Kilimo cha Mwani pamoja na Utengenezaji wa Chumvi.

Mheshimiwa Hemed alisema NMB inapaswa kupongezwa kwa vile tayari imeshaamuwa nguvu zake za kiuwezeshaji kuzielekeza kwa kundi hilo muhimu na kubwa linalojumuisha Watu wenye kipato kidogo kuliko makundi mengine hapa Nchini.

“ Nazielewa jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara katika kushirikiana na Serikali kwenye Miradi ya Maendeleo ambayo wakati mwengine inawagusa moja kwa moja Wananchi”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba azma ya Serikali Kuu ni kuona mafanikio makubwa ya Nchi lazima yafike kwa Mwana jamii wa kipato cha chini kwa vile Miradi yote inayotekelezwa na kuanzishwa na Serikali hulenga kumjengea mazingira mazuri ya Ustawi Mwananchi.

Mapema Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara Bibi Ruth Zaipuma alisema Taasisi hiyo ya Fedha Nchini ina sehemu yake katika Sekta ya Uchumi wa Buluu ambayo kwa Zanzibar tayari imeshaunda Wizara inayoshughulikia eneo hilo muhimu kwa Uchumi wake.

Alisema Wataalamu wa Benki hiyo wameshaanza utaratibu wa kuwajengea uwezo Wauvi, Wakulima wa Mwani pamoja na Wazalishaji wa Chumvi  kwa kuwapatia Mafunzo maalum ambapo baadae watakuwa na uwezo wa kupatiwa Mikopo ya Fedha za kuendesha Miradi yao kati ya Shilingi Laki 500,000/- hadi Milioni 5,000,000/-.

Mtendaji Mkuu huyo wa NMB alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Benki hiyo pia inakwenda sambamba na Sera ya Uwajibikaji katika Jamii kwa kusaidia huduma kwenye Sekta za Afya, Elimu pamoja na kuunga mkono misaada pale yanayotokea majanga.

Bibi Ruth aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Benki hiyo tayari imeshatoa dhamira ya kufanya kazi pamoja na SMZ baada ya kugundua maono yake,kuyaelewa. na hatimae kuazimia kuyafanyia kazi.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.