Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amekutana na Mwakilishi wa Kampuni ya Ufuaji Umeme wa Usarifu wa Takataka.

Bwana George Alexandru akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla.
Mwakilishi wa Kampuni ya Ufuaji wa Umeme kwa kutumia taka taka kutoka Romania Bwana George Alexandru Kushoto akionyea nia ya Kampuni yake kutaka kuiunga Mkono Zanzibar katika uwekezaji wa Miradi ya Kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla kulia  akizungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Ufuaji wa Umeme kwa kutumia taka taka kutoka Romania Bwana Georga Alexandru Vuga Mjini Zanzibar.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko makini katika kuona kasi ya Uwekezaji Nchini inaendelea kuimarika ili lengo la Taifa la kuwa na Jamii yenye Ustawi mzuri linafikiwa.

Akizungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya ufuaji wa Umeme kwa kutumia usarifu wa Taka taka kutoka Romania hapo Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alisema Serikali inaelewa fika umuhimu wa Uwekezaji kwa vile ndio njia kuu ya kuongeza Mapato sambamba na upatikanaji wa fursa za Ajira.

Alisema Zanzibar imeshajiweka tayari kuyaandaa mazingira Rafiki yatakayotoa nafasi kwa Taasisi, Kampuni na hata Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kutumia Rasilmali zilizopo Nchini katika Kuwekeza Miradi ya Kiuchumi kupitia usimamizi wa Mamlaka inayohusika na Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA}.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuyahakikishia Makampuni, Taasisi na Mashirikkia ya Uwekeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wa kina ili wale waliyoonyesha nia ya dhati ya kuwekeza Vitega Uchumi wanakamilisha taratibu zao kwa wakati.

Mapema Mwakilishi wa Kampuni ya ufuaji wa Umeme kwa kutumia usarifu wa Taka taka kutoka Romania Bwana George Alexandru alisema Uongozi wa Taasisi hiyo ya Uwekezaji uko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika muelekeo wake wa kuimarisha Sekta ya Uwekezaji.

Bwana Alexandru alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi wa Ufuaji wa Umeme kwa kutumia Taka Taka wanaokusudia kuuanzisha endapo watafanikiwa kupata fursa hiyo utatengewa Dola za Kimarekani Milioni Mia Moja.

Alisema kwa mujibu wa uzoefu wa Kampuni hiyo, Taka taka  zenye kiwango cha Tani zipatazo 180 zikisarifiwa vyema zina uwezo wa kufua Megawati 11.5 za Umeme.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo ya ufuaji wa Umeme kutoka Romania alifahamisha kwamba utafiti wa awali uliofanywa katika Jaa kuu la kutupia Taka taka liliopo Kibele umeonyesha lina uwezo wa kutosheleza kuanzishwa kwa Mradi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.