Habari za Punde

Makamu wa Rais, Mhe. Hemed mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya watu wenye Ulemavu Duniani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akipata maelezo kutoka kwa Wajasiri Amali kutoka Jumuiya za Watu wenye Mahitaji Maalum nje ya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kwenye maadhimisho ya Siku ya Watu wenye ulemavu Duniani.
Mheshimiwa Hemed akiangalia kifaa kilivyotengenezwa na Wajasiri Amali kutoka Jumuiya za Watu wenye Ulemavu ambacho kinatumika katika mapambo ndani ya Gari.
Mmoja wa Wakalimani wa Lugha ya Alama wakiwatafsiria Watu wenye Ulemavu wa Kusikia matukio yanayojiri ndani ya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani.
Watoto wenye Mahitaji Maalum wakiwasilisha  kasda Maalum yenye ujembe mzito unaoshajiisha Watoto kupenda kusoma badala ya kushughulikia mambno yasiyo na msingi.
Baadhi ya Vijana Wenye Ulemavu wakifuatilia yanayojiri ndani ya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani
Baadhi ya Viongozi, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Wananchi na baadhi ya Watu wenye Ulemavu wakufuatilia Hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman hayupo pichani.
Wafanyakazi wa Idara ya Watu wenye ulemavu hawakuwa mbali katika kufuatilia Hotuba za Viongozi mbali mbali zilizokuwa zikitolewa kwenye Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dr. Khalid Salum Mohamed akitoa Taarifa ya masuala ya Watu wenye Ulemavu kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza kwenye kwenye maadhimisho ya Siku ya Watu wenye ulemavu Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni.
Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeida Rashid Abdulla akitoa shukrani kwa Serikali zote mbili jinzi zinavyoendelea kuunga mkono Kundi la Watu wenye Ulemavu Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akipokea Picha Maalum iliyochorwa sura yake kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Bibi Abeda Rashid mara baada ya kukamilia kwa sherehe za siku ya Watu wenye ulemavu Kimataifa.

 Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiionyesha juu Picha ya Kuchora yenye sura yake iliyochorwa kwa ustadi mkubwa na Msanii chipukizi Nchini Asaa Yussuf.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewanasihi na kuwatia moyo Watu wenye Ulemavu Nchini wanaweza kufanikiwa kimaisha kama Watu wengine kwa kuzitumia fursa zinazotolewa na Serikali na Mashirika ambazo zinaweza kubadilisha maisha yao kuwa bora zaidi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelewa ukubwa wa tatizo la ulemavu Nchini na imejipanga kupambana nalo kwa njia mbali mbali  ikiwemo kuwapatia  haki na fursa Watu wenye Ulemavu ili waweze kumudu vyema mazingira yao.

Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni, Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema suala la kuielimisha Jamii kuachana na mitazamo hasi juu ya ulemavu ni jambo la msingi litakalozingatiwa.

Alisema elimu hiyo itakwenda sambamba na kupitiwa kwa Sheria, Sera na Miongozo ili Watu wenye Ulemavu wa aina zote waendelee kupatiwa haki zao za msingi kama wanavyopata Watu wengine.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwa vile muelekeo wa Taifa tayari umeshajikita kuimarisha Uchumi wa Buluu, Taasisi na Jamii zinapaswa kuwashirikisha kikamilifu Watu wenye Ulemavu katika masuala yote kwenye Sekta hiyo ili nao watoe mchango wao kwa Taifa.

Katika kufikia azma hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imejipanga kuwawezesha Watu wenye Ulemavu Kiuchumi kwa kuwapatia Elimu na ujuzi kwa kusimamia na kutathmini Mipango na shughuli zao ili waweze kujitegemea.

Alifahamisha kwamba uwezeshwaji huo utaambatana na utolewaji wa vifaa na visaidizi, kuondoa ubaguzi, kuhimiza mwenendo mzuri, kuunganisha Sera na Mipango pamoja na kuhakikisha Majengo yote yanayotoa huduma kwa Jamii yanakuwa rafiki na kufikiwa na Watu wenye Ulemavu.

“ Mtu Mwenye Ulemavu anaweza kufanikiwa  katika maisha yake kama Mtu mwengine katika Jamii. Ulemavu sio kikwazo cha kuviza mafanikio”. Mh. Hemed alikuwa akikariri maneno ya Mwanafizikia maarufu Duniani ambae alikuwa Mlemavu wa Viungo Profesa Stephen Hawking.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba idadi ya Watu wenye Ulemavu imekuwa ikiongezeka kila siku kwa sababu ya kasi ya maradhi ya kisukari na shindikizo la damu, maradhi yanayopelekea wakati mwengine Mtu kupooza au kupoteza Viungo vyake.

Alisema kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Afya Duniani {WHO} hivi sasa kuna Watu Bilioni Moja sawa na asilimia 15% ya Watu wote Ulimwenguni ambao wamekumbwa na aina mbali mbali za Ulemavu.

Alisema kwa Zanzibar idadi ya Watu wenye Ulemavu inakadiriwa kufikia Elfu 8,265 kati yao Wanawake 3,890 na Wanaume 4,375 ambapo kwa tafiti za Wataalamu upo uwezekano wa kuongezeka kwa idadi hiyo kutokana na sababu ya kuzidi kwa maradhi yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Hemed hata hivyo alibainisha wazi kwamba kasi ya ongezeko la Ulemavu inayotokana na maradhi yasiyoambukiza inaweza kupungua kwa Watu kufuata ushauri wa Madaktari ikiwemo kutumia vyakula vya asili kama mboga mboga, Matunda, pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kuwa karibu na Taasisi zinazosimamia masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa kuendelea kushirikiana katika kuona changamoto zinazowakabili wasimamizi hao pamoja na Watu wenye Ulemavu wenyewe zinapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kupitia Mkutano huo wa Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulamavu ameviagiza Vyombo vya Dola kuanzia sasa kumchukulia hatua za kisheria mara Moja Mtu anayewadhalilisha Watu wenye Ulemavu kwa kuwapa Majina yasiyostahiki.

Alisema Wananchi lazima waendelee kutoa ushirikianokatika kuona udhalilishaji huo wa majina yasiyostahiki dhidi ya Watu wenye Ulemavu linafutika katika Jamii kwa sharia ya kuwachukulia hatua wadhalilishaji ipo ndani ya Katiba.

Akiwasilisha Risala ya Watu wenye Ulemavu, Mwakilishi wa Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar {Shijuwaza} Nd. Ali Omar alisema Kundi la Watu wenye Ulemavu limefarajika na azma ya Serikali katika kuwashirikisha  Viongozi wa Jumuiya za Kundi hilo katika ngazi mbali mbali za Maamuzi.

Nd. Ali Omar alisema fursa mbali mbali zitakazoibuliwa ndani ya Mfumo Mpya ulioanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Uchumi wa Buluu utasaidia kupunguza ukosefu wa ajira sambamba na utegemezi kwa Kundi la Watu wenye Ulemavu Nchini.

Alisema ili kuwasaidia Watu wenye Ulemavu kupitia mfumo huo wa Uchumi wa Buluu hapana budi kulijengea uwezo kundi hilo kwa kutengewa Bajeti Maalum itakayokidhi mahitaji kwa Watu hao sambamba na uimarishaji wa Miundombinu hasa kwenye Majengo ya huduma za Jamii.

Kwa upande wake akitoa Taarifa fupi ya Maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdula Hassan Mitawi alisema Zanzibar imeanza kuadhimisha Siku hiyo tokea Mnamo Mwaka 1981.

Ndugu Mitawi alisema siku hiyo muhimu imekuwa ikisherehekewa chini ya Muasisi wa Uliokuwa Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar Mwenyekiti wake Marehemu Maalim Khalifan Hemed Khalfan.

Alieleza kwamba Tanzania na Zanzibar kwa ujumla zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavuna  uliotolewa na Umoja wa Mataifa na kutia saini mnamo Mwaka 2009.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye sherehe hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Wizara tayari imeshapokea Ahadi za Rais wa Zanzibar alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu zile zinazowahusu Watu wenye Ulemavu Nchini.

Dr. Khalid alisema Utekelezaji wa Ahadi hizo utakwenda kwa kasi kubwa kwa vile suala la Watu wenye Ulemavu ni Mtambuka kutokana na kugusa na Sekta, Taasisi na Idara na kuonyesha unaigusa Jamii moja kwa moja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi alisema Wizara hiyo inatarajia kuitisha Mkutano wa Wadau wote hivi karibuni kupitia Sera kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Watu wenye Ulemavu, Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdulla aliwapongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa moyo wao wa upendo waliyouonyesha wa kulithamini kundi la Watu wenye Ulemavu Nchini.

Bibi Abeid alisema dalili za ushiriki wa Kundi hilo katika masuala mbali mbali ya Maendeleo zimeanza kujichomoza hasa ikizingatiwa kwamba kasi ya Serikali imeelekea katika mwendo wa haraka mno.

Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani imetangazwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mnamo Mwaka 1992 chini ya Azimio Nambari 47/3.

Lengo la kuadhimisha Siku hii kila Mwaka ni pamoja na kuzitaka Nchi Wanachama wa Umoja huo kuimarisha Uwezeshaji pamoja na kuwapatia  fursa stahiki Watu Wenye Ulemavu ili waweze kuendesha maisha yao kama Watu wengine.

Ujumbe wa Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani Mwaka huu unasema:- “ UCHUMI WA BULUU JUMUISHI UTATOA FURSA KWA WATU WENYE ULEMAVU”.                                      

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.