Habari za Punde

Mbunge wa Uzini akabidhi vifaa vya ujenzi

 Bahati Habibu  Maelezo  Zanzibar   28/12/2020.

Mbunge wa Jimbo la Uzini ambae pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Khamis (Chilo) amewataka wazee kuwahimiza watoto wao kusoma kwa bidii ili kupata taifa lenye wasomi na wenye kuleta maendeleo.

Mhe. Chilo ameyasema hayo huko Skuli ya Mchangani Wilaya ya Kati Unguja wakati  akikabidhi vifaa vya Ujenzi wa banda moja lenye vyumba vinne.

Alisema Serikali inatilia mkazo vijana kusoma kwa bidii na kujikita zaidi katika masomo ya sayansi ili kufikia uchumi wa buluu na kuleta mafanikio mazuri nchini.

‘’Masomo ya sayansi yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuleta maendeleo ya Taifa lolote lile Duniani na pia ni masomo yenye soko la ajira hivyo nawaasa wazee na wanafunzi kujitahidi sana’’, alieleza Mbunge huyo.

Mbunge huyo alikabidhi mabati 100, matofali 500, na  mifuko ya saruji 50 ambayo yatatumika kwa ajili kumaliza ujenzi huo.

Wakati huo huo Naibu Waziri Chilo alipata fursa ya kuwakagua majeruhi pamoja Jengo la Mji Mkongwe la Beit Aljaib lililoporomoka na kusababisha vifo vya watu wawili wiki iliyopita na alivitaka vikosi vya ulinzi na usalama kuchunguza chanzo cha ajali hiyo pamoja na kujenga uzio ili kuhifadhi eneo hilo .

Aidha alisisitiza wasanifu wa majengo wa ndani na nje ya nchi kushirikiana  kwa pamoja na kutafuta suluhisho ili jengo liweze kurudi katika hadhi yake na kuendelea kuwa kivutio kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.