Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Watendaji wa Serikali Pemba Akiwa Katika Ziara Yake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Watendaji wa Serikali na Kamati ya Ulinzi na Usalama Pemba, mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kwamba suala la udhalilishaji atalichukulia hatua za makusudi kupambana nalo na  kamwe halitomshinda.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo huko katika ukumbi Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba wakati alipokutana na Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama  za Mikoa Miwili ya Pemba.

Alisema kuwa visiwa vya Zanzibar ni visiwa vinavyopaswa visiwe na matatizo ya udhalilishaji hasa kutokana na imani za kidini zilizopo lakini inaonekana kadhia hiyo imeshika hatamu na kuahidi kwa upande wake hatokubali kushindwa.

Alisema kuwa suala la udhalilishaji limekuwa sugu katika jamii na kueleza  kwamba hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa licha ya kuwa takwimu za janga hilo zinatisha.

Alisema kuwa suala la udhalilishaji halina mmoja na  limekuwa likianza katika jamii  na likifika Polisi halishugulikiwi vizuri ama wahusika wanapatanishwa nje ya Polisi ama mtu anachukua rushwa na aliyeonewa ndie anayetuhumiwa na hatimae likienda mbele katika sheria linakuwa tatizo.

Alisisitiza  wajibu wa kukaa kama nchi kutafuta muwarubaini wa suala hilo kati ya Serikali mpaka vyombo vya usalama ikiwemo na mahakama na kueleza kwamba kamwe jambo hili haliwezi kushinda.

Alisema jambo hilo ni baya sana, linadhalilisha watu, linabadilisha maisha ya watu hasa watoto pamoja na kuwapelekea wazazi wamekuwa wakipata  matatizo ya kisaikolojia na kueleza haja ya kutafutiwa ufumbuzi kwani kama ni sheria basi sheria zimetungwa na Serikali na zinaweza kubadilishwa.

Aliwataka Polisi kulipa kipamumbele suala hilo na kutaka lisiishie kwa maofisa katika deski la Polisi na kutaka kila mkuu wa kituo ajue hilo na alisimamie kama lake.

Aliwataka Wakuu wa Polisi wa Mkoa na Wilaya kuyasimamia hayo na kuhakikisha wanayasimamia hayo huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa hatua za makusudi katika kuliondoa tatizo hilo.

Alisema kuwa kuna sheria zinatungwa ambazo kwa upande wa Zanzibar hazipo na kutolea mfano kwa Tanzania Bara ambako kumetungwa sheria ikiwemo ya uhujumu wa uchumi ambayo haina dhamana na kutaka kufika sehemu kutungwa sheria za namna hiyo kwa Zanzibar.

Alisema kuwa wapo watu wanadhalilisha wenzao lakini bado wako mitaani, pia kuwepo kwamahakama ambazo mamlaka yao ya kutoa sheria ni miaka michache ya kuwafunga watu na kusema kuwa hali hiyo haitosaidia na kusisitiza kwamba iwapo watu hawatofungwa kadhia hiyo halitoisha.

Alisema kuwa kuna haja ya kuonesha kwa vitendo mapambano ya rushwa na kueleza jinsi alivyoitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kutosubiri siku ya rushwa duniani na kutoa idadi ya kesi na badala yake kuwataka kupambana hadharani katika suala la rushwa na udhalilishaji kwa kuanza katika jamii kwani watu wanajulikana.

“Ndugu zangu mtanisamehe nalisema hili kwa msisitizo zaidi kwani ni kitu ambacho kinanikera na kitu ambacho kinaonekana kama vile kinataka kuonekana kushinda lakini natambua kwamba iwapo kutaamuliwa tatizo hilo halitoshinda”,alisisitiza Dk. Hussein Mwinyi.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi hao wote kwa kutimiza majukumu yao na kuvipongeza kwa dhati vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kudumisha amani na usalama nchini.

Aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wote wa Unguja na Pemba kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni mnamo mwezi wa Oktoba mwaka huu kwa kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kudumisha amani.

Akizungumza kwa upande wa watendaji wa serikali alitaka wajue matarajio yake

alirejea kauli yake ya mara nyingi ya uwajibikaji kwani amegundua kwamba bado watu hawajawajibika na kutaka kila mtu awajibike katika majukumu waliyopewa ili kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa.

Aliwataka watendaji wote wa Serikali kuwajibika katika majukumu waliyopewa sambamba na kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Alieleza haja ya kuondoa urasimu, kwani kuna mambo yanachelewa kutokana na urasimu uliopo na kusisitiza haja ya kutokuwepo urasimu hasa katika masuala ya uwekezaji na kutaka kuondolewa kabisa.

Aliongeza kwamba mbali ya kuwepo urasimu katika uwekezaji pia, kuna urasimu wa kutoa hudumakatika taasisi za serikali na kutaka kadhia hiyo kuondolewa katika utendaji wa kazi.

Rais Dk. Mwinyi alieleza suala zima la rushwa makazini na kusema kuwa watu wanadaiwa rushwa na kusisistiza kwamba jambo hilo haliwezi kustahamilika na kusema bora liwekwe wazi.

Alisema kuwa rushwa ipo katika maeneo mengi yakiwemo katika vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na maofisi ya serikali ambapo watu kwa kutaka haki zao ama huduma bado wamekuwa wakidaiwa rushwa na kutaka viongozi wajitathmini wao wenyewe.

Rais Dk. Hussein alieleza suala zima la ubadhirifu hasa katika kipindi hichi ambapo hali ya fedha haiko vizuri bado kumekuwa na watu wakiendelea kufanya ubadhirifu wa fedha ikiwa ni pamoja na kuendelea na makongamano, semina, kukata sare za kwenda kwenye semina na bila ya kuwepo kwa vipaumbele.

Alisema kuwa yale mambo ambayo yanataka akufanya kutokana na uhaba wa rasilimali fedha hayafannywi na badala yake yanafanywa yale mambo ambayo hayana tija.

Katika suala la kutatua kero za watu, Rais Dk. Hussein alisema kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji katika kutatua kero za wananchi kwenye ofisi za serikali, Polisi na sehemu nyengine na kutaka wawe tayari kuondokana na utendaji wa mazoea na kusisitiza haja ya kuweka kipaumbele katika kutatua kero za wananchi.

Alisema kuwa katika Mamlaka pamoja naIdara za Serikali bado kumekuwa na shida katika kutatua kero za wananchi.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa kumekuwa nakasi ndogo ya kutatua kero za kufuatilia miradi kwani kuna kero nyingi za miradi ikiwa ni pamoja na viwango vidogo vinavyojengwa miradihiyo sambamba na kufanywa ubadhirifu wa fedha na kutaka kila mwenye Idara yake kufuatilia miradi inayomuhusu.

Alisema kuwa Serikali imekopa fedha nyingi kwa ajili ya kujenda miradi lakini bado utekelezaji wa miradi hiyo hauko vizuri.

Alisema kuwa haki za wafanyakazi zimekuwa zikikosekana kwani kila mfanyakazi ana haki zake na wajibu wake  ikiwemo likizo, posho kwa muda wa ziada wa kazi na nyenginezo na kutaka kila kiongozi kama rasilimali fedha zipo basi ahakikishe wafanyakazi wake wanapata haki yao hiyo.

Aliwataka viongozi hao kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi mwenye haki yake apewe kwani kumekuwepo na ukiritimba makazini na hatua hiyo ikiendelea hapatakuwa na ufanisi makazini.

Suala la usimamizi nalo alilieleza na kusema kuwa mfanyakazi yoyoyte akipewa jukumu na kutokuwepo msimamizi utendaji unakuwa mdogo na kusema kuwa kumejengeka tabia ya watu kutosimamiwa.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alitaka usimamizi kwa kila mtu na kila kazi ili kuweza kufanya kazi kwa ustadi mzuri zaidi.

Alisisitiza kwamba kuna tabia ya baadhi ya viongozi kutochukua hatua dhidi ya wale watu wasiotekeleza majukumu yao na kusisitiza haja ya kuchukua hatua kwani hilo pia ni jukumu lao.

Alisema kwamba iwapo mambo yote hayo yatarekebishwa utendaji mzuri utafanikishwa na utendaji wa serikali utaimarika zaidi na kusisitiza kwamba  mambo mengi hayahitaji fedha na badala yake yanahitaji utendaji tu.

“Tunataka kuleta maendeleo tuliyowaahidi wananchikamatunataka kufanikiwakatika miradi tuliyoileta, kama tunataka wananchi waone huduma zinabadilika basi kwamnaza tujitathmini sisi wenyewe kabla hajatoka mtu wa nnje basi tujitathmini sisi wenyewe mimi nataka niseme wazi kwamba nitachukua hatua”, alisisitiza Dk. Hussein.

Alisema kuwa asipochukua hatua gurudumu la uzembe litaendelezwa huku akiwataka wateule wake nao wachukue hatua kwani kila mtu ana mamlaka yake nawasipofanya hivyo basi wateule hao hawamfai.

Aidha. Alieleza azma yake ya kutaka ufanisi katika Serikali na iwapo kutaondolewa , urasimu, rushwa, ubadhilifu wa mali ya umaa ufanisi mkubwa utapatikana kwani jambo hilo halina mmoja.

Alieleza haja ya kufanya kazi ya kwuatumikia watu kwani yeye amechukua jukumu na kwuaambia watu wamchague kwa azma ya kuwaondolea kero zao na watakaomsaidia ni viongozi hao.

Aliwataka kwenda na kasi mpya ya akuhakikisha kwamba wananchi wanawatumkia kweli kweli na kwa wale wateule wake Mawaziri ambao wameanza kwa kasi mpya pamoja na wakuu wa Mikoa na hivi katribuni atawateuwa wakuu wa Wualaya na Makatibu wakuu na ambaye hatowajibika hatomuacha ofisini hata kama amemteua kwa siku moja.

Alisisitiza kwamba rushwa ataipiga vita hadharani na hapatakuwa na utaratibu wa kufunika funika na kutakuwa na utaratibu wa kuchukua hatua za papo kwa papo kwani nia yake ni  kuweka dhamira yake wazi.

Alisisitiza kwamba kila mtu anatekeleza wajibu wake na wale wanaofanya vitu kinyume na maadili basi wasiendelee kufanya na kuahidi serikali itafanya kila ;linalowezekana katika kuhakikisha kila mtu anapata maslahi yake.

Alisema kuwa vipaumbele katika maslahi ya serikali ikiwa ni pamoja na maslahi ya wafanyakazi yatafanyiwa kazi lakini kwani anatambua wako wafanyajazi haki zao hawapati na kuahidi vipaumbele vitawekwa kwa wafanyakazi.

Alisisitiza kwamba hatomvumilia kiongozi yoyote ambaye anawanyima haki zao wafanyakazi, alieleza kwamba mabadiliko katika utendaji wa serikali wananchi ndio watakaosema ukweli baada yakuona huduma bora wanazipata

Aliwataka viongozi wote wa Serikali kuhakikisha kila mtu anatambuliwa na wafanyakazi wanavaa vitambulisho maalum (beji) kwa lengo la kutambuliwa hatua ambayo pia, itakuwa rahisi kuchukuliwa hatua.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitaka kwa muda mfupi watu waseme kwamba kuna mabadiliko makubwa katika serikali kwani hiyo itakuwa ndicho kigezo kikubwa ndani ya serikali na kuwataka wasimamizi wafanye kazi na matumaini yake kwamba katika kipindi kifupi kijacho tofauti ya utendaji itaonekana Serikalini.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.