Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Viongozi wa CCM na Mabalozi wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Pemba leo.18-12-2020

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza Viongozi wa CCM na Mabalozi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa mkutano wake wa kutowa shukrani kwao kwa kumchagua kuwa Rais wa Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa ni vyema viongozi na wanachama wakanza kufanya kazi kwani uchaguzi umekwisha na yeye pamoja aliowateua wako tayari kutekeleza majukumu yao.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati alipokutana na Viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa huo kwa ajili ya kuwashukuru na kuwapongeza kufuata ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu 2020.

Alisema kuwa matumaini kwa wananchi ni makubwa sana, na kama chama wanalo jukumu la kusimamia katika kutatua kero za wananchi pamoja na kufanya ziara za mara kwa mara katika miradi ya maendeleo na kuwa na jukumu la kuhakikisha pale penye kasoro wanatoa taarifa mapema kwani hayo yakifanyika mafanikio makubwa yatapatikana.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wakati wa kuleta maendeleo ndio huu kwani tayari amani na umoja vyote vipo hapa nchini hivyo, kilichoobaki ni kufanya kazi ambapo kila mmoja ni vyema akawajibika ili kuhakikisha yale yote yaliokusudiwa yanatimia.

Alisisitiza kwamba wale wote wanaofanya kazi Serikalini wahakikishe wanawajibika na wale wasiowajibika basi watawajibishwa kwani anaamini kwamba kuleana pamoja na kuoneana aibu hakutaleta mafanikio.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliwataka wananchi pamoja na wanaCCM kutoa taarifa mapema za changamoto zinazowakabili hasa wale waliopo vijini.

Aliwataka wale wote waliopo Serikalini kuhakikisha kwamba kila senti ikiwa ya Serikali ama mkopo lazima thamani yake ionekane ambapo hatua hiyo ikichukuliwa maendeleo yataimarika.

“Si kweli kama hatuna pesa wala si kweli hatujachukua mikopo lakini tatizo kuna watu wanasubiri zile fedha wafanye zao, iko miradi mingani ambayo maji hayatoke, zipo barabara ngani ambazo baada ya muda mfupi zikishajengwa mashimo yanaaza, sasa mamba kama haya tusipochukulia hatua mapema ahadi zetu zote tutashindwa kuzitekeleza” alisema Dk. Mwinyi.

Alisisitiza kwamba anasema mapema ili hatua zitakapoanza kuchukuliwa watu wasije wakashtuka na kutaka kila mfanyakazi wa Serikali atambue kwamba fedha za Serikali ni kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Alieleza kuwa kukiwa na miradi ya Serikali ikiwemo miradi ya maji ni lazima visima vikachimbwa na maji yakatoka bila ya kufanywa ukiritimba wowote.

Alisema kuwa anaetaka kufanya kazi ya Serikali yupo kwa ajili ya kuwajibika kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu kampeni ya aina yake ambayo ni ya kisayansi ilifanyika ambayo imetokana na utekelezaji wa Ilani kuwa amzuri sambamba na kuwafikia wananchi wote wakiwemo wanaoishi vijijini.

Alipongeza kwa ushindi wa kihistoria uliopatikana wa aslimia 76.27 na kuwapongeza viongozi wa CCM wakiwemo Mabalozi kwa kazi nzuri ya Kampeni hali ambayo imepelekea ushindi mkubwa.

Alisisitiza haja ya kuendelezwa amani na kueleza kuwa bado kuna dhima ya kuendelea kuhubiri amani na kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anaitunza amani kwa azma ya kupata maendeleo.

Alisema kuwa jukumu la amani si la vyombo vya ulinzi na usalama peke yaokwanai  jukumu la amani ni la kila mmoja na kuwataka wananchi wote wa Zanzibar bila ya kujali itikadi zao za kisiasa kuhakikisha wanaiendeleza amani iliyopo.

Alieleza kuwa kwa upande wa umoja, katika nchi watu wakifarakana kuleta maendeleo inakuwa shida na ndio maana kukaundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hivi sasa kumeamulwia kuweka tofauti zote pembeni.

Alisema kuwa wapo baadhi katika chama cha CCM na baadhi katika vyama vya upinzani ambao hawajafurahishwa na suala la Umoja wa Kitaifa na kueleza haja ya kuendelea kupeana elimu kutokana na umuhimu mkubwa wa kuwa wamoja na kushirikiana.

Alisema kuwa wananchi wanataka maisha bora, huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu bora kwa watoto wao na hawataki chuki na hasama miongoni mwao huku akitoa ahadi kuwa atafanya kazi sana kwa azma ya kutekeleza yale yote  ambayo wananchi wana matumaini nayo.

Rais Dk. Mwinyi alielezaa haja ya kujipanga kutekeleza Ilani ya CCM, kutekeelza ahadi zilizoahidiwa, kusimamia kwa pamoja utekjekezaji kwani hiyo si kazi ya serikali peke yake bali na chama nacho kina nafasi ya kusimaimia utekelezaji pamoja na kuhakikisha kinakuwa mstari wa mbele.

Sambamba na hayo, alisema kuwa yeye binafsi amejipanga kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kumuomba Mwenyezi Mungu na kuwaomba viongozi hao wa CCM pamoja na wananchi kumuombea ili apate wepesi wa kutekeleza dhamira aliyonayo.

Alieleza kuwa wana kila sababu ya kuwatumikia wananchi na  kuhakikisha yale yote aliyoyaahidi yanatimia huku akiwaeleza wanaCCM hao kuwa anayo azma ya kufanya mkutano kwa wanaCCM wote kisiwani humo.

Alisisistiza kuwa rekodi ya ushindi wa asilimia 76.27 wa kura uliyopatikana basi ivunjwe mnamo mwaka 2025 kwa kuwatumikia wananchi vyema.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.