Habari za Punde

Sijaridhishwa na matumizi ya fedha za ujenzi wa nyumba za askari kisiwani Pemba - Naibu Waziri Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (kulia), Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Hassan Haji, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi Hamis na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Sururu wakiangalia paa la moja ya nyumba za askari polisi zinazojengwa eneo la Finya, wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba,wakati wa ziara ya naibu waziri kukagua miradi ya taasisi zilizopo chini ya wizara yake, leo Kisiwani Pemba.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  


Bahati Habibu Maelezo Zanzibar         29/12/2020.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Hamza Khamis (Chilo) amesema hajaridhishwa na matumizi ya fedha za ujenzi wa nyumba za askari kisiwani Pemba kwani gharama zilizotumika haziendani na ubora wa nyumba hizo.

Ameyasema hayo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za Polisi na askari wa Uhamiaji katika ziara ya siku mbili  huko Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni ishirini kwa kila nyumba.

  Amesema kuwa thamani iliotumika katika ujenzi wa nyumba hizo ilitakiwa ziwe tayari kwa makazi lakini bado nyumba hizo haziwezi kukalika na gharama iliotumika ni kubwa.

“Ujenzi wa nyumba hizi kuanzia msingi hadi kuezekwa sijaona ubora wowote ambao umefanya zitumike milioni ishirini kiukweli sijaridhishwa na ujenzi huu hauna kiwango” alisema Naibu Waziri

Awali naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi alipokea taarifa ya mradi huo kutoka kwa Kamanda wa Polisi Wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis kuwa mradi wa nyumba hizo umegharimu shilingi million ishirini na mbili laki saba na elfu nane na mia mbili kwa kila nyumba

 Hivyo Naibu Waziri huyo amevitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara hiyo kutumia kwa umakini fedha za miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi hizo huku akiwaasa kuangalia thamani ya mradi husika.

 

Aidha naibu waziri huyo amesema wapo baadhi wa watu  huitumia vibaya bandari ya Wete kwa kuingiza dawa za kulevya pamoja na bidhaa nyengine zisizo ruhusiwa nchini hivyo amevitaka vyombo vya ulinzi kulishughulikia tatizo hilo mara moja.

Pamoja na hayo alipata nafasi ya kuzungumza na wafanya biashara  na wavuvi wa samaki katika pwani ya Shumba Mjini iliyopo  Wilaya ya Micheweni ambapo wavuvi hao wameiomba Serikali kuwapelekea boti ya kuokolea wahanga wa ajali za majini pindi zinapotokea.

Akiendelea na mazungumzo hayo mwenyekiti wa wafanyabiashara hao ndugu Husein Rashid alimwambia naibu wazir kuwa jumla ya watu kumi wamepoteza maisha baada ya kuzama kutokana na kukosa vifaa vya kuokolea.

akijibu Naibu Waziri amewataka wafanya biashara hao kuwa wastahamilivu kwani Serekali inayoongozwa na Dkt Hussein  Ali Mwinyi imekusudia kuzirasimisha Bandari zote bubu za Zanzibar kuwa Bandari rasmi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.