Habari za Punde

Walimu watakiwa kuwa wapole kwa wanafunzi wanapotoa ushauri

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Idrissa Muslimu Hija akitoa nasaha zake alipofungua mafunzo ya afya ya uzazi , jinsia pamoja na UKIMWI kwa walimu wa madarasa ya Msingi ya Kati na Sekondari yaliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha walimu TC kiembe Samaki mjini Unguja
 
Baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo ya afya ya uzazi , jinsia pamoja na UKIMWI kwa walimu wa madarasa ya Msingi ya Kati na Sekondari yaliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha walimu TC kiembe Samaki mjini Unguja wakisikiliza kwa makini 
Baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo ya afya ya uzazi , jinsia pamoja na UKIMWI kwa walimu wa madarasa ya Msingi ya Kati na Sekondari yaliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha walimu TC kiembe Samaki mjini Unguja wakisikiliza kwa makini 

Picha na Maulid Yussuf, Wema


Na Maulid Yussuf WEMA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Idrissa Muslimu Hija amewataka Walimu kuwa wapole kwa Wanafunzi wao katika kuwapa ushauri mzuri utakaowasaidia kuwaongoza Katika maisha yao.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya afya ya uzazi , jinsia pamoja na UKIMWI kwa walimu wa madarasa ya Msingi ya Kati na Sekondari yaliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha walimu TC kiembe Samaki mjini Unguja amesema hatua hiyo itawasaidia katika kuwakinga na maradhi mbalimbali pamoja na vitendo vya udhalilishaji vinavyopelekea kupata maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.

Amesema lengo la kupatiwa Walimu wa madarasa mafunzo hayo ni kutokana na wao kuwa karibu zaidi na Wanafunzi ambapo itawasaidia kuwapa ushauri kwa kutumia mbinu mbadala watakazopatiwa katika mafunzo hayo.

Amesema vijana wakati huu wa sasa wanahitaji ushauri na ukaribu zaidi kwa Walimu na wazazi hasa katika masuala hayo yanayohusiana na uzazi na maambukizi ya Ukimwi kwa kuwaelimisha ipasavyo ili wasiweze kujiingiza na vitendo vilivyo nje na wakati wao.

Aidha amewataka Walimu wa kike na wakiume kutojihusisha na vitendo vya udhalilishaji hasa kwa Wanafunzi wao, kwani zimeshajitokeza kesi hizo, hivyo amewataka Walimu kuwalea vizuri wanafunzi wao na kuwaona ni sawa kama watoto wao kwa ili nao waweze kuwa na maisha bora ya hapo baadae.

Pia Dkt Idrissa amewataka Walimu kuyachukua Mafunzo hayo na kuyatekeleza katika sehemu zao za kazi kwa vitendo na kuwataka kuwatambua vizuri vijana wao kutokana na mazingira wanayoishi hivi sasa na wakati unavyokwenda ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Nae Mkurugenzi Idara ya Mafunzo ya Ualimu Bi Maimuna Fadhil Abbas amewataka Walimu kuwapa taaluma hiyo Wanafunzi wao kwa usahihi ili waweze kuwasaidia katika masuala yao mbalimbali.

Amesema Mwanafunzi anatakiwa awe huru na salama wakati wote akiwa Skuli au nyumbani na wahusika wakuu wa kuwasaidia watoto kuwa salama ni Mwalimu, kwani wazazi wengi hawawaelekezi watoto wao masuala hayo ya uzazi salama na kujamiiana pamoja na athari za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa kuona ni aibu, hali ambayo sio sahihi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewashirikisha Walimu wa vituo Vya Walimu TC Dunga, TC Kitogani na Mjini yameandaliwa na Shirika linaloshughulikia masuala ya Elimu duniani UNESCO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.