Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais akutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi  akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla Vuga, akiwa katika ziara ya siku tatu Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilish Mheshimwia Dr. Khalid Salum Mohamed akifafanua jambo katika Kikao hicho.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, akimpongeza Profesa Kabudi kwa kueteuliwa kushika nafasi hiyo kwa mara nyengine.

 Picha na – OMPR – ZNZ.


Uandishi wa vitabu vingi vya Lugha ya Kiswahili itaifanya lugha hiyo kuwa ni bidhaa, kwa nchi mbali mbali , pamoja na kuongezeka kwa watumiaji wake , ni moja kati ya sababu zinazopelekea kukuwa kwa lugha hiyo, ya utambulisho wa muafrika .

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki Profesa Palamaganba John Kabudi aliyasema hayo alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla Vuga, akiwa katika ziara ya siku tatu Zanzibar.

Alisema uwepo wa taasisi ya kiswahili Zanzibar ndani ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} itaweza kusaidia kuzidi kutoa wataalamu waliobobea zaidi katika lugha hiyo ndani nan je ya Nchi.

Alisema Tanzania imefanikiwa kushawishi lugha ya Kiswahili, kutumika katika Jumiya ya Kiuchumi ya nchi za Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, ikiwa ni agizo alilolotoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli, katika kuikuza lugha ya Kiswahili duniani.

Profesa Kabudi alisema mashirikiano yanayoendelea kwa nchi hizo hasa katika Nyanja za Kiuchumi ni dhahiri kuwa Tanzania inaendelea kuungwa mkono katika jitihada mbali mbali za maendeleo, akitoa mfano wa ziara ya Waziri wa nchi za Nje wa China aliyofanya hivi karibuni nchini Tanzania,

Alisema ziara imeonyesha kukubaliwa kwa ombi la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli, la kuisadia Zanzibar kwenye ujenzi wa kilomita za barabara 148.3,  ikiwa ni chachu ya kurahisisha miundombinu ya kukuza uchumi wa buluu visiwani Zanzibar.

Aidha Waziri Kabudi alimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kusimamia vyema mradi wa kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki kiliopo Beit El Ras , ili kitoe huduma kwa mwambao mzima wa Afrika Mashariki na Kati, na kuahidi kuwa wizara yake itafanya mazungumzo na Mabalozi mbali mbali, ili kukisaidia kituo hicho, na  kukisimamia vyema kutafuta soko kwa mataifa mbali mbali.

Akizungumzia sekta ya Uvuvi na Kilimo alisema ni dhahiri Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dr John Pombe Magufuli, imeweka bayana kukuza uvuvi wa bahari kuu, kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, na kueleza kuwa Serikali imeahidi kuleta meli nane za uvuvi, ambapo nne kati ya hizo ni kwa ajili ya Zanzibar.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, alimshukuru Profesa Kabudi kwa kuona umuhimu wa kumtembelea ofisini kwake, na  kumpongeza kwa kueteuliwa kushika nafasi hiyo kwa mara nyengine, huku akizungumzia imani ya Wazanzibari na Watanzania juu ya uteuzi wake.

Mheshimiwa Hemed alisema Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza mashirikiano yake na Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kuwa Ofisi yake ndio inayosimamia na kuratibu masuala ya Muungano, na Wizara ya mambo ya Nje ni mdau mkubwa wa Muungano.

Alisisitiza kwamba changamoto zote zilizobaki zinaweza kupatiwa ufumbuzi ili wananchi wa Tanzania wazidi kunufaika na muungano huu.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane inafanya vyema katika utekelezaji wa majukumu yake chini ya uongozi wa Dr Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Alibainisha kwamba yapo mafanikio mengi yaliyopatikana katika awamu hii, na Imani ya wazanzibar kwa serikali zao zote mbili, na kumtaka Waziri Kabudi kufanya ziara Kisiwani Pemba ili kujionea namna wananchi wa kisiwa hicho walivyokuwa na imani na serikali zao.

Mheshimmiwa Hemed aliwapongeza watendaji wa wizara hiyo wanaofanya kazi ofisi ya Zanzibar kwa mashirkiano yao wanayoonyesha kwa ofisi yake, hasa pale panapohitajika msaada wowote kutoka kwao.

Mapema Waziri wa Nchi Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilish Mheshimwia Dr. Khalid Salum Mohamed, alimshukuru Waziri Kabudi pamoja na watendaji wa wizara yake, kwa ziara ambayo wamefanya muda muwafaka kwa kutembelea ofisi mbali mbali hapa Zanzibar, akieleza kuwa itaamsha hisia na moyo wa utendaji, hasa kwa Mawaziri ambao wengi wao ni wageni katika majukumu hayo.

Aidha Dr. Khalid alisema wizara yake imedhamiria kuzimaliza changamoto zilizobaki za muungano kwa muda mdogo sana, ili kuendana na kasi ya serikali zote mbili.

Ziara hiyo ya Waziri Kabudi imeambatanisha pia na Naibu waziri wa wizara hiyo mheshimiwa Willium Olenasha, Katibu Mkuu Wizara hiyo, balozi bregedia jenerali Wilbert Ibuge, kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Zanzibar na watendaji wengine mbali mbali wa wizara hiyo.



 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.