Habari za Punde

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi Yanaonesha Ukakamavu Uzalendo na Utayari Wao Kupagania Nchi Yao Kuyaenzi na Kuyalinda Mapinduzi.

 

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akizungumza na Vijana wa UVCCM katika viwanja vya Skuli ya Msingi Mwera wakati wa mapokezi ya Matembezi hayo, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yanaonesha ukakamavu, uzalendo na utayari wao katika kuipigania nchi yao sambamba na kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964.

Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake ya kuyapokea Matembezi ya Vijana hao wa (CCM) ya kuazimisha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar hafla iliyofanyika Mwera, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mama Mariam Mwinyi alieleza lengo lake la kuwapongeza na kuwatia moyo vijana hao kwa kuwatia faraja wazazi wao kutokana na ushiriki wao huo huku akisema kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuyatangaza Mapinduzi ya Zanzibar nchini kote.

Alieleza kuwa mbali ya kutembea vijana hao wamekuwa wakifanya shughuli mbali mbali za kijamii zikiwemo kufanya usafi katika maeneo kadha wakati wakiwa katika Matembezi hayo ambapo hatua hiyo inaonesha wazi jinsi wanavyomuunga mkono Rais Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi.

Pia,Mama Mariam Mwinyi aliwapongeza vijana hao kwa hatua zao za kujumuika katika ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika jamii ikiwemo ujenzi wa skuli hatua ambayo wamekuwa wakiiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane katika maendeleo ya nchi.

Akitoa salamu za Rais Dk. Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi  yuko pamoja na vijana hao na anawaunga mkono kutokana na juhudi zao na yuko tayari kushughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo zile za ajira, elimu na nyenginezo.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi akiwa kama mama aliwaasa vijana kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kwani zinapotosha vijana na zimekuwa zikipoteza nguvu kazi ya Taifa kwani asilimia kubwa ya watu wa Zanzibar ni wale waliozaliwa baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 wakiwemo vijana.

Aliwataka vijana kuwa amstari wa mbele katika kupiga vita suala zima la uzalilishaji wa wanawake na watoto na kuwataka kutojingiza katika masuala hayo na kusema kwamba akiwa ni mzazi mambo hayo yamekuwa yakimuumiza sana.

Hivyo, aliwataka vijana hao kuwa Mabalozi na kuwa macho kwani wengi wanaotenda mambo hayo wamo katika jamii, na kutaka wailinde nchi hayo sambamba na kuwafichua waovu wote wanaotenda mambo hayo.

Sambamba na hayo, aliwataka vijana kujitahidi kufahamu Sera na vipambele vya nchi ili waweze kujua fursa ziko wapi na kujua nchi inakwenda wapi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kufuata fursa za uchumi wa buluu ambao ndio uliopewa kipaumbele hivi sasa hapa nchini.

Alisema kuwa iwapo watafahamu Sera na kupata habari juu ya mikakati ya Serikali hatua hiyo itasaidia  kutambua na hatiamae kuweza kupata ajira na hatimae kupata kipato.

Mama Mariam Mwinyi alikubali ombi la vijana hao kuwa  mlezi wa Matembezi hayo na kuahidi kuwapelekea zawadi maalum sambamba na kupokea maombi ya kuwasidia wale vijana wa CCM wanaotoka nje ya Zanzibar kwa kuwawezesha kufika na kushiriki kikamilifu katika matembezi hayo ya kila mwaka.

Sambamba na hayo, aliwatakia kila la heri washiriki wote wa Matembezi hayo na kueleza kuwa yuko tayari kuwaunga mkono ili kutekeleza malengo ya kuyaenzi na kuyatunza Mapinduzi matukufu ya Januari 12. 1964.

Nae Makamo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa ambaye pia, ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid alimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa ujio wake huo na kueleza jinsivijana walivyofarajikahuku akieleza jinsi vijana hao wanavyoyaenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kupitia matembezi hayo.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (CCM) Zanzibar, Mussa  Haji  alisema kuwa Matembezi hayo yalizinduliwa Januari 5. 2021 na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla huko Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umekuwa na desturi ya kufanya Matembezi kila mwaka  yakiwa na lengo la  kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo pia, hufikisha ujumbe kwa jamii pamoja na kufanya shughuli kadhaa za kijamii.

Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza shughuli mbali mbali walizozifanya vijana hao katika matembeziya mwaka huu ikiwemo ujenzi wa miradi ya maendeleo  pamoja na kufanya usafi.

Aliongeza kuwa vijana hao wapatao 800 ni  kutoka  Mikoa yote ya Tanzania ambapo kila Mkoa umetoa mwakilishi  wakiwa na lengo la kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.