Habari za Punde

Zanzibar Imeamua Kujiimarisha Katika Sekta ya Biashara na Uwekezaji Mabalozi wa Tanzania Nje Kuitangaza Vyema Zanzibar. -Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (kulia kwa Rais) akiwa na Naibu Wairi wake Mhe. Willium Tate Ole, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 22-1-2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba Zanzibar imeamua kujiimarisha katika sekta ya biashara na uwekezaji hivyo Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania popote pale walipo wana dhima ya kuitangaza vyema Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Professa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi,  Ikulu Jijini Zanzibar  ambapo Waziri Kabudi alifuatana na Naibu Waziri wake Willium Tate Ole Nasha na Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vyema wakaitangaza Zanzibar katika Balozi zao nje ya nchi sambamba  na kuangalia uwezekano wa kuitangaza sekta ya utalii na masoko hasa kwa bidhaa za viungo.

Alisema kuwa Mabalozi wana kila sababu ya kuitumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina vivutio vingi kwenye sekta ya utalii, masoko pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa wakati Mabalozi hao wakifanya kazi hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kujenga uwezo katika kuuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuuimarisha uchumi wa buluu ikiwemoutalii pamoja na viungo (spice).

Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali anayoiongoza ya kukiimarisha kituo cha ufugaji wa samaki kiliopo Beit el ras ili kiweze kutoa huduma ndani na nje ya Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wakati umefika kwa vijana wa Zanzibar wanaofanya kazi katika Ofisi za Wizara hiyo kwa upande wa Zanzibar kujengewa uwezo sanjari na kupata ujuzi zaidi kutokana na kubadilishana vituo vya kazi kati ya Dodoma  na Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imepelekea amani, umoja na mshikamano kuimarika pamoja na maelewano ya wananchi wa Zanzibar ambao hivi sasa wana kiu ya kujiletea maendeleo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza umuhimu kwa Zanzibar kushiriki katika vikao vya maandalizi kuhusu utekelezaji wa maeneo ya Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi.

Alisema kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo waliyoyatarajia ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi zilizoahidiwa kwa wananchi wakati wa Kampeni za uchaguzi uliopita.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa vile Wizara ya Mambo ya  ya Nje na Ushirikiano wa  Kimataifa ni ya Muungano ana matumaini makubwa kwamba mashirikiano  yatakuwepo kati ya Wizara hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alieleza kwamba ziara ya Waziri Kabudi na ujumbe wake wa Wizara hiyo hapa Zanzibar itazidisha ushirikiano sambamba na kuweza kutekeleza vyema majukumu ili kufikia malengo yaliokusudiwa kwani Wizara hiyo imekuwa ikifanya kazi zake vizuri.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Professa Palamagamba John Aidan MwalukoKabudi  alimpongeza Rais wa Zanzibar Dk. Hussein mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata kwa kuchaguliwa kwa asilimia 76.6 ya kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba,2020.

Alisema kuwa ushindi huo unadhihirisha imani waliyonayo wananchi wa Zanzibar kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Dk. Mwinyi kufuatia ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi hasa ile ya  kuimarisha uchumi, Muungano, umoja, mshikamano, maridhiano pamoja na kuleta maendeleo na neema kwa wananchi wa Zanzibar.

Hivyo, alisema kwamba Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ipo tayari kusaidia kuyafikia malengo ya kuimarisha uchumi, Muungano, umoja, mshikamano na maridhiano kadri itakavyowezekana.

Alipongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha umoja, maridhiano na mshikamano ili kuimarisha mazingira ya amani na maendeleo nchini.

Waziri Kabudi alimueleza Rais Dk. Mwinyi Muundo wa Wizara hiyo ambao ina Idara 12  ambapo pi,a ina Idara na Vitengo Visaidizi 8 ambapo katika Idara na Vitengo vyote Wizara hiyo ina Balozi zake 45.

Alisema kuwa ushirikiano uliopo baina ya Wizara yake na Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Asasi za Kiraia zilizopo Zanzibar zinasaidia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi kwa mafanikio.

Waziri Kabudi alitoa ushauri wa Viongozi Wakuu wa Zanzibar kuzielekeza Wizara na Taasisi za Serikali kutenga bajeti maalum katika Ofisi hizo kwa ajili ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na maeneo ya kimkakati kama vile mtangamano wa Kikanda (AU,SADC,IORA,EAC) na Ushirikiano wa Kimataifa.

Aidha, Waziri alieleza azma ya Wizara yake ya kuzifanyia ukarabati mkubwa Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Zanzibar pamoja na kuwabadilisha maeneo ya kazi wafanyakazi wa Wizara hiyo walioko Zanzibar kwenda Dodoma na wale wa Dodoma kuja Zanzibar kwa azma ya kubadilishana uzoefu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.