Habari za Punde

Serikali awamu ya nane kuongeza juhudi za kufufua uchumi : Dk Hussein Mwinyyi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea kuchukua juhudi za kufufua uchumi hatua kwa hatua ambapo tayari ongezeko la makusanya limeanza kuimarika.

Dk. Hussein Mwinyi alimeyasema hayo leo katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni sherehe zake za kwanza tokea achaguliwe kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari makusanyo yameanza kuongezeka kutoka bilioni 22 mwezi wa Oktoba hadi kufikia bilioni 36.9 mwezi wa Disemba 2020, makusanyo ambayo yalikusanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Dk. Mwinyi alisema kuwa sekta ya utalii imeendelea kuimarika ambapo lengo lililowekwa la kupokea watalii 250,855 ifikapo Disemba 2020 baada ya kuzingatia mwenendo wa maradhi ya COVID 19, hadi Novemba 2020 jumla ya watalii 212,050 wameitembelea Zanzibar sawa na asilimia 85 ya makadirio.

Hivyo, Serikali ya Awamu ya Nane itaisimamia kwa karibu uratibu, utangazaji na uendelezaji wa sekta hiyo ili itoe mchango mkubwa zaidi kwa Wazanzibari na uchumi kwa jumla.

Alisema kuwa hivi sasa linatafutiwa ufumbuzi tatizo lililojitokeza la kuchelewa kupatiwa wageni huduma za msingi wanapofika katika Uwanja wa ndege na kuwasababishia usumbufu lengo ni kuhakikisha wageni wanafurahia makaazi ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha sekta ya utalii inakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya uchumi wa buluu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa alitamani sherehe hizo ziwe na shamrashamra kama ilivyozoeleka kutokana na umuhimu wake hata hivyo, imelazimika kuzifanya kwa namna tofauti kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioikumba nchi na ulimwengu kwa jumla.

Kwa hivyo, alisema kuwa busara na hekima zimeelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya sherehe hizo zielekezwe katika kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji safi na salama.

“Ieleweke kuwa hali hii ni ya mpito, tunatarajia katika kipindi kijacho, sherehe hizi zitafanyika katika utaratibu uliozoeleka’, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mmwinyi alisema kuwa kuna kila sababu za kuyaenzi Mapinduzi kwa sababu ndicho chombo kilichowavusha wananchi wa Zanzibar katika dhoruba za kutawaliwa na kubaguliwa katika nchi yao.

“Kwa mnasaba huu, leo ni siku muhimu sana katika historia ya Zanzibar, ambapo miaka 57 iliyopita, wakulima na wafanyakazi wanyonge walikataa madhila ya kubaguliwa’,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Alisisitiza kwamba zinapoadhimishwa Sherehe za Mapinduzi kutimiza miaka 57, kuna wajibu wa kuwakumbuka na kuwashukuru wazee waasisi wa Chama Cha Afro-Shirazi, walioongozwa  na Marehemu Mzee Abeid Amani karume.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuendelea kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano uliopo ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo.

Alieleza kwamba Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au kikundi cha watu watakaojihusisha na vitendo vya kuvuruga amani ya nchi na kuwasihi wananchi kuendelea kuaminiana, kuheshimiana na kuvumiliana na kusahau tofauti zao.

Alisema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara kuelekea eneo huru la uwekezaji la Micheweni, Pemba ambapo pia, kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza ujenzi wa skuli za ghorofa katika ngazi zote za elimu pamoja na kujenga vituo vya mafunzo ya amali kwa mujibu wa mahitaji ya wananchi pamoja na ununuzi wa vifaa vya elimu ikiwemo madawati kwa ajili ya skuli za Unguja na Pemba.

Alisema kuwa Serikali inatarajia kujenga hospitali kubwa ya rufaa na ya kufundishia katika eneo la Binguni, ambayo itakidhi mahitaji ya wataalamu, vifaa na uwezo wa kimiundombinu ambapo mchakato wa ujenzi umeshaanza.

Aidha, Serikali itahakikisha sehemu zote ambazo hivi sasa zinakosa huduma za umeme na maji zinapata huduma hiyo kwa mujibu wa mahitaji ya wananchi pamoja na kufanya mapitio ya miradi yote ya maji na umeme Unguja na Pemba.

Aliitaka Wizara ya Ardhi kushirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kumaliza migogoro yote ya ardhi ifikapo mwisho mwa mwaka huu na hatopenda kusikia kuna mwananchi analalamikia kudhulumiwa ardhi yake.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali imeamua katika mwaka ujao wa fedha kuongeza uwezo wa bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili iweze kuwahudumia vijana vizuri zaidi.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, itaendelea na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara katika maeneo ambayo huduma hiyo haijafika ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kuimarisha maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo.

Sambamba na hayo, alisema kwamba Serikali ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mangapwani, pamoja na jitihada hizo, usimamizi wa shughuli za bandari na viwanja vya ndege utaimarishwa.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kurejesha nidhamu ya kufanya kazi na kutokomeza mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha  na kamwe watumishi wa umma wasisahau kuwa wao ni watumishi sio mabwana na  wawatumikie kwa ufanisi, uadilifu na kwa heshima wananchi huku wakitambua kuwa huo ndio wajibu wao.

Aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuandaa utaratibu maalum wa kushirikiana na Manispaa na Mabaraza ya Mji pamoja na wananchi katika kushughulikia usafi wa miji na maeneo yao.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza na kuuimarisha Muungano.

“Mimi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunatambua uzito wa dhamana mliyotupa Watanzania, katika kuhakikisha kuwa Muungano wa Tanzania unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa Awamu zilizopita”, alisema Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Rais Dk. John Magufuli  kwa jitihada zake za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, uhujumu wa uchumi, dawa za kulevya na kuzilinda rasilimali za nchi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.