Habari za Punde

Serikali Imeanza Kuchukua Hatua za Makusudi Kupambana na Rushwa,Wizi,Ubadhilifu wa Mali ya Umma na Ufisadi -Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Viongozi wa CCM na Mabalozi wakati wa mkutano wa wa kutoka shukrani wakati wa ziara yake Wilaya ya Kati Unguja uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Makunduzi Mkoa wa Kusini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwatayari ameazakuchukua hatua na ataendelea kuchukua mpaka kila mmoja awajibike katika nafasi yake ya kazi aliyonayo.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika Skuli ya Sekondari Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja wakati  alipokutana na Viongozi wa CCM wakiwemo Mabalozi, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Tawi, Wadi,Jimbo pamoja na Wazee wa CCM na watumishi mashuhuri.

Alisema kuwa hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kupambana na rushwa, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi.

Alifahamishwa kwamba hata juhudi zikifanyika iwapo wapo watu wanaendelea na vitendo hivyo hakuna maendeleo yatakayopatikana hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika katika kupambana na hilo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa amani na umoja vyote vipo na tayari wapo walioelewa kwamba lazima wafanyakazi wa serikali wawajibike.

Alisema kuwa ameanza kuchukua hatua kali ya kuondoa wizi, ufisadi, ubadhirifu na sasa mazingira yako tayari kuleta maendeleo.

Aidha, alisema kuwa madhumuni ya mkutano huo ni kwenda kutoa shukurani kwa wanaCCM pamoja na wananchi wa Wilaya hiyo kwa kuipa ushindi CCM na kuweza kuongoza nchi.

Alisema kuwa ana kila sababu ya kurudi wkao na kutoa shukurani kutoakana na kufanikiwa katika chama hicho kutokana na Kampeni zilizofanywa wakati wa uchaguzi na kuwapongeza viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo.

Aliongeza kuwa kazi iliyopo mbele ni kwualetea wananchi maendeleo lakini maanedleo hayawezi kupatikana kama hakuna amani na kuwashukuru wananachi wa Zanzibar kwa kuidumisha amani.

Rais Dk. Mwinyi ambaye katika ziara hiyo amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi alisisitiza kwamba baada ya amani kuna jambo muhimu la kuleta maendeleo amabalo ni umoja kwa wananchi.

Alisema kuwa Zanzibar iligumbikwa na uhasama na chuki, watu kutokuwa wamoja ambao walikuwa hawazikani, hawasali pamoja ndoa zilikuwa zikivunjia wakati wa uchaguzi.

Alisisitiza kuwa ili kuweka mazingira mazuri ya kuleta maendeleo ni lazima umoja upatikane na ndipo yakawekwa mazingira ya kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo yatapelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano.

Alisema kuwa jambo hilo limefanywa kwa nia safi ya kuunganisha watu na kusisitiza haja ya kuwaelimisha wale ambao bado hawajatambua kwamba jambo hilo lina faida na umhimu mkubwa katika kuleta maendeleo.

Alisisitiza haja ya kuwajibika na kueleza kuwa maendeleo hayapatikani ikiwa hapana uwajibikaji, kuwepo kwa wazembe ambao bado wanaendelea kupata mishahara.

Katika hotuba yake hiyo alieleza kwamba jukumu lake kubwa ni kuhakikisha ahadi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo inatekelezwa sambamba na kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alisisitiza kwamba licha ya kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wateule wake wote wajue kwamba wana jukumu la kutekeleza Ilani ya CCM.

Aidha, alisema kuwa tayari ameanza kuleta watu wa kushirikiana na Serikali  kuleta maendeleo hapa Zanzibar huku akisisitiza haja ya kufuatia njia tatu ambazo ni makusanyo ya serikali kupitia bajeti, kukopa kupitia kwenye benki na taasisi mbali mbali pamoja na kushirikiana na sekta binafsi.

Alisema kuwa tayari mipango imeshapangwa kupitia bajeti ya Serikali ijayo kwa ajili ya mipango ya maendeleo, kukopa kwenye taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na hivi sasa kujitokeza wawekezaji mbali mbali wa kujenga kwa ubia kati yao na serikali miradi kadhaa.

Aliongeza kuwa hivi karibuni Serikali imetia saini ujenzi wa bandari ya kubwa ya kisasa huko Mangapwani/Bumbwini na wiki ijayo kutakuwa na hafla nyengine ya utiaji saini wa ujenzi wa bandari ya uvuvi ambayo nayo itakuwa ya kisasa.

Sambamba na hayo, alisema kuwa Serikali itajitahidi kutekeleza yale yaliyoahidiwa na kuwataka wana CCM, kuwahimiza viongozi ili kuhakikisha wanatekekeza wajibu wao kwa wananchi.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki ni kuiimarisha Serikali katika kuhakikisha inaleta maendeleo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kufanya Maridhiano na hatimae kufanyika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa sambamba na kuimarishwa kwa amani, umoja na maelewano hapa nchini.

Nao viongozi wa CCM wa Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja, walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua na kusisitiza kwa wale wote aliowateua wasimuangushe na badala yake wachape kazi.

Pia, walimpongeza kwa hatua zake za kuhakikisha matumizi makubwa ya serikali yanaondoshwa huku wakimpongeza kwa kupambana na rushwa, wizi, ufisadi na kuahidi kuendelea kumuombea dua.

Mapema Rais Dk. Mwinyi alizuru kaburi la Marehemu Hasnu Makame Mwita muasisi wa ASP, huko Mzuri Makunduchi ambapo katika maelezo yake Mzee Ramadhani Haji Simai mwenye umri wa miaka 83 ambaye alikuwa mtu wa karibu wa marehemu alieleza historia fupi ya marehemu na hatimae walimuombea dua kwa pamoja akiwa na viongozi wengine wa CCM.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alifika kijiji cha Kiongoni Makunduchi na kuzuru kaburi la Marehemu Sheikh Idrissa Abdul Wakilaliyekuwa Rais  wa Zanzibar wa Awamu ya Nne (1985-1990) na kumuombea dua akiwa pamoja na viongozi wengine wa CCM.

Wakati huo huo,Rais Dk. Mwinyi aliitemebelea jengo la CCM Wilaya hiyo ya Kusini ambayo iliungua moto  mnamo tarehe 13.01.2021 na kupata maelezo juu ya athari zilizotokea pamoja na kuelezwa azma na mikakati ya CCM ya Wilaya hiyo ya kujenga jengo jipya la kisasa katika eneo hilo na kuahidi kuchangia milioni 20 taslim za ujenzi wa Ofisi hiyo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alipitisha harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi hiyo na kujitokeza viongozi mbali mbali kuchangia ujenzi huo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.