Habari za Punde

Serikali ya Umoja wa Kitaifa imedhamiria kuendeleza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar: Dk Mwinyi


 

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 Zanzibar                                                              21.01.2021

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imedhamiria kuendeleza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar ambayo inakwenda  sambamba na misingi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ukiongozwa na Mkurugenzi  wake Joseph Butiku uliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kwua Rais wa Zanzibar pamoja na kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa  kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeweza kuimarisha amani, umoja na mshikamano hapa Zanzibar  hatua ambayo ni chachu ya maendeleo na imekuwa ikisisitizwa siku zote na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Alisema kuwa hivi sasa kumekuwepo maelewano na mashirikiano makubwa kati ya viongozi pamoja na wananchi walio wengi wa Zanzibar hali ambayo imepelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano tokea kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa nchini.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo lengo na madhumuni yake makubwa ni kuendeleza umoja, amani na mshikamano ili Zanzibar izidi kupata maendeleo na wananchi wake wazidi kuelewana.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi hiyo ya Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ndani na nje ya nchi pamoja na Jumuiya za Kimataifa.

Alifahamisha kwamba Taasisi hiyo imekuwa na mahusiano mazuri na Serikali zote mbili, mashirikiano na Taasisi za kidini pamoja na vyama vya siasa ambapo imekuwa ikifanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja na yenye kuleta tija.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi  hiyo kwa midahalo mizuri inayoiendesha ikiwemo ile inayozungumzia masuala ya amani ambayo imekuwa ikitoa maelekezo kwa wananchi katika suala zima la kusimamia amani, umoja na mshikamano nchini.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kueleza kwamba Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zina dhima kubwa ya kuleta wananchi maandeleo badala ya kujikita zaidi katika masuala ya kisiasa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Taasisi hiyo pamoja na nyengine zote hapa nchini katika kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja, amani na mshikano kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alilipokea ombi la Taasisi hiyo la kuwa na Ofisi zake hapa Zanzibar na kuahidi kufanyiwa kazi kwa azma ya kuiwezesha Taasisi hiyo kufanya kazi zake vyema.

Mapema Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya ujio wao ikiwa ni pamoja na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana mnamo Oktoba 2020.

Alisema kuwa ushindi huo ni ushahidi tosha unaoonesha kwamba kwa namna gani wananchi wa Zanzibar wanaimani kubwa na Rais Dk. Mwinyi katika azma yake ya kuwaletea maendeleo.

Sambamba na hayo, Taasisi hiyo pia, ilitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwezesha kuendeleza tena Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa  Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa lengo la kufikia demokrasia ya hali juu na maendeleo.

Pamoja na hayo, Mzee Butiku alisema kwamba hivi sasa Zanzibar imeweza kuonekana ikiwa na amani, umoja, utulivu na mshikamano  mkubwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumpa maelezo mafupi Rais juu ya lengo kuu na malengo madogo ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, muundo wake, kazi zake, ikiwa pamoja na maagizo rasmi na maalum aliyoyaacha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake kwa taasisi hiyo.

Sambamba na hayo, Mzee Butiku alimueleza Rais Dk. Mwinyi juu ya shughuli inazozifanya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na uongozi wa Asasi za Kiraia na Mrajis wao kuzungumza na viongozi wa ngazi za Wilaya na Shehia wakiwa na nia ya matokeo ya mazungumzo hayo kwa kuandaa mafunzo ya Uongozi na Uendeshaji wa viongozi wa Ngazi mbali mbali nchini.

Alisema kuwa katika zoezi hilo wamepata mashirikiano makubwa katika maeneo waliyokwenda katika Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba ambapo katika maelezo yao walieleza jinsi Madiwani wa Mikoa hiyo walivyoeleza imani na matumaini yao makubwa kwa Rais Dk. Mwinyi Serikalini.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.