Habari za Punde

Wachezaji niliowatumia wana uwezo wa kutosha Mapinduzi Cup - Cedric Kaze


 Na mwandishi wetu

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga Cedric Kaze amesema wachezaji ambao wamo katika kikosi chake wana uwezo wa kutosha wa kucheza mashindano ya kombe la Mapinduzi.

Kocha huyo aliyaeleza hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati yake na Jamhuri ambao walitoka sare tasa, hali iliyoonekana kwamba matokeo hayo yametokea kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji wake.

Alisema kuwa kilichofanyika katika kikosi cha chake ni maamuzi ya ufundi kutokana na wachezaji hao kutumika sana katika mechi za ligi na iliwapasa wapumzike.

“Wachezaji wametumika sana kwenye ligi tunatoka kwenye ziara ya mikoani na siku 21 tumeishi njiani na tulicheza mechi nne sasa kuna wachezaji wengine wamechoka sana na mechi za ligi na kutokana na mwili wa mchezaji ilibidi apumzike”, alisema.

Hivyo alisema kuwa anaamini kwamba wachezaji waliopo katika kikosi chake wana uwezo wa kutosha wa kucheza katika mashindano hayo ya kombe la mapinduzi na ndio maana wakapewa nafasi za kucheza.

Alifahamisha kwamba katika mechi hiyo wamecheza vizuri na wachezaji ambao wametokea U-20 wamecheza vizuri na kuonesha uwezo wao.

“Tumecheza vizuri na mechi ilikuwa nzuri ila kilichojitokeza ni kwamba waamuzi hawakuwa kwenye kiwango cha mchezo na kuonekana kuzidiwa mbinu ingawa mimi sio msemaji wa hilo”, alisema.

Aidha alisema kuwa watajipanga katika mechi yao ya leo na Mlandege ili kuweza kufanya vizuri zaidi na kuondoka na matokeo ambayo yataiweka timu yake katika mazingira mazuri.

Kuhusu kupoteza kitu katika mchezo huo kutoakana na matokeo hayo alisema kuwa wachezaji 11 kutoka kila upande walishindana na chochote ambacho kilitokea ni moja ya matokeo ya mchezo.

Hivyo alisema kuwa haoni kama amepoteza badala yake yeye ambacho amekiona ni kwamba wachezaji wake hasa vijana wameongeza kujiamni na udhoef uwanjani.

“Watu wakicheza dakika 90 hawawezi kusema kama wamepoteza kitu, hatukupoteza kitu hata kimoja wanaume 11 walikuwa uwanjani na walikuwa wakicheza na kuongeza kujiamini kwa pande zote mbili hasa kwa wale ambao wachezaji waliotoka U-20 ambao nao walipata nafasi ya kucheza kwenye mchezo huo”, alisema.

Yanga ipo katika kundi A linaloundwa na timu tatu wakiwemo wao pamoja na Jamburi Namungo ambapo leo itashuka dimbani tena kucheza na Mlandege saa 2:00 usiku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.