Habari za Punde

Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenda sambamba na SMZ Uchumi wa Buluu

 Issa Mzee  -  Maelezo 22/01/2021

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema Wizara ya Mambo ya Nje itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha mikakati ya kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na ufugaji wa samaki inafanikiwa ili kufanikisha  uchumi wa bluu nchini.

Akizungumza katika ziara yake wakati alipotembelea  kituo cha utotoaji wa vifaranga vya samaki Beitrasi pamoja na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari kuu Fumba amesema Wizara hiyo inadhamana  ya kushughulikia sheria ya uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kulinda na kuhakikisha  maslahi ya taifa yanapatikana kisheria.

 Alisema ushirikiano wa taasisi, wawekezaji  pamoja na wavuvi wa  ndani na nje ya nchi ni lazima uimarishwe kupitia balozi mbalimbali za Tanzania ili kufanikisha shughuli za uvuvi wa bahari kuu kwa mujibu wa sheria za taifa na kimataifa.

“Huwezi kuzungumzia uchumi wa buluu bila kuizungumza Wizara ya Mambo ya Nje, uvuvi wa samaki nje ya bahari kuu ni jukumu letu  kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa pamoja na Wizara ya uvuvi na uchumi wa buluu Zanzibar na Wizara ya uvuvi Tanzania ili kuona namna gani tunafanya na vipi  tunanufaika” alisema Waziri Kabudi

Alisema kuwa ipo haja ya kundelea kuwepo mifumo ya uangalizi wa shughuli za uvuvi nchini ili kuweza kufatilia wawekezaji wote wanaovua samaki kisheria katika mipaka yote ya bahari na kuwabaini waliokinyume na sheria ili kuweza kudhibiti rasilmali za bahari ya Tanzania zisipotee.

“ Ni vizuri na ni bora kuwepo mfumo huu wa kimtandao ambao unatusaidia kujua vipi samaki wetu wanavuliwa kwa kutumia dhana gani na kwa kiwango kipi ili tujiridhishe,tuthibitishe na kuilinda bahari yetu dhidi ya wavuvi haram” alisema Waziri.

Alifafanuwa kuwa uchumi wa buluu unafaida  kubwa kwa kila nchi yenye bahari duniani kwani mataifa mengi yanaendelea kutumia fursa hiyo ili kukuza pato la nchi sambamba na kuipongeza mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu kwa mfumo mzuri wa ukusanyaji mapato licha ya kupungua kwa wawekezaji kutokana na mripuko maradhi ya corona duniani.

Aidha alisema kuwa ipo haja ya kushirikiana na Wizara ya Uvuvi ya Tanzania  na Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Zanzibar pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ili kupanga mpango kazi na mkakati na kuona kwa namna gani uchumi wa buluu unatekelezwa na kuleta matunda nchini.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Tanzania ina mpango wa kununua meli nane za uvuvi nne kwa Tanzania bara na nne kwa Zanzibar ikiwa ni moja ya mikakati ya kuimarisha  uvuvi wa bahari kuu Nchini.

Aidha aliwataka watendaji wote wa taasisi na mamlaka za uvuvi  kufanya kazi kwa pamoja na kuweka mazingira bora ya uvuvi wa bahari kuu na uchumi wa buluu kwa ujumla ili kuona jinsi gani wavuvi wakubwa na wadogo pamoja na wananchi wananufaika na bahari yao.

Akizungumzia suala la ufugaji wa samaki alisema ipo haja ya kukifanya kituo cha ufugaji na utotoaji wa samaki kilichopo Beitrasi Zanzibar kuwa ni kituo mahiri cha utotoaji na uzalishaji wa vifanga vya samaki kwa Tanzania wakiwemo sato,kambare na samaki wa baharini  ili wadau wote wa ufugaji wa samaki waje kujifunza kituoni hapo.

Alisema kuwa ipo haja ya kuleta wataalamu kutoka nje pamoja na kuwatumia watalamu wazawa na kushirikiana na Taasisi ya sayansi ya bahari Tanzania kuja kutoa mafunzo ili kuondoa changamoto ya uhaba wa wataalamu na hatimae kukuza uzalishaji wa vifaranga vya samaki Zanzibar.

“Ni lazima tujipange ili kufanikisha haya mafunzo pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kutosha tutazungumza na ofisi za ubalozi ikiwemo Indonesia ili tuweze kufanikisha suala hilo” alisema Profesa Kabudi.

Aidha aliipongeza Serikali ya Zanzibar kwa kuweka Wizara maalumu ya Uchumi wa Buluu na kuimarisha zao la mwani ambalo limeinua kipato cha kina mama wengi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu Zanzibar Mh Abdallah Hussein Kombo amesema suala la kupatiwa wataalamu ni suala muhimu katika kuendeleza shughuli za ufugaji na utotoaji wa samaki ili kuhakikisha lengo la Serikali la kuimarisha sekta ya uvuvi linafanikiwa.

“Tunaamini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaweza kutusaidia pia katika kufanikisha upatikanaji wa vifaa pamoja na wataalamu wa sekta ya ufugaji wa samaki kupitia ofisi mbalimbali za ubalozi wa Tanzania” alisema Waziri

Aidha Waziri kombo amemuahidi Waziri wa Mambo ya Nje kuwa watashirikiana na Wizara hiyo ambayo pia inahusika kisheria katika suala la uchumi wa bluu pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanikisha kipaumbele cha Rais wa Zanzibar cha kukuza Uchumi wa Buluu hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.