Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aufungua rasmi Masjid Rahma Saateni, akagua Mashine ya uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu alipofika kuufungua Rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Al Rahma wa Saateni Pinda Mgongo.
Mwanchuoni Maarufu Nchini Sheikh Samir Zulfikar Ramadhan akimuelekeza Mheshimiwa Hemed Sehemu Maalum ya kuufungua Msikiti huo utakaotoa huduma za Ibada kwa Wafanyabiara na wanunuzi wa Soko la Saateni.
Ustadhi Khamis Hamad Khamis Akisoma Risala ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti Al - Rahma wa Saateni Pinda Mongo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Msikiti huo.
Mwanachuoni Maarufu Nchini Sheikh Samir Zulfikar Ramadhan akisisitiza umuhimu wa kutunzwa kwa Amani Nchini ambayo imeelezwa vyema ndani ya Miongozo ya Dini ikianzia na utoaji wa salamu.
Mkuu wa Wilaya ya Mjini Nd. Rashid Simai Msaraka akiwahakikishia Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi uwepo wa ulinzi wa kutosha na kuwaondoshea usumbufu wa Vijana wanaotumia Dawa za Kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akiwakumbusha Waumini wenye uwezo kuendelea kuimarisha Majengo ya Ibada ili kupata Baraka za uchamungu.
Mkurugenzi wa Idara ya  Maendeleo ya Mifugo Zanzibar Bibi Asha Zahran Mohamed akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Mashine ya uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa wa maziwa ilivyopunguza kasi ya uzalishaji baada ya kuharibika kwa kifaa muhimu cha uzalishaji wa Hewa na Nitrogen
Mkuu wa Kitengo cha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Ng’ombe wa Maziwa wa Kituo hicho Nd. Faki Ame Keis akifafanua Maziwa yanayozalishwa na Mashine hiyo ya Lita Tatu kwa saa Moja badala ya Lita Kumi kwa ajili ya Mbegu Bora za Ng’ombe wa Kisasa wa Maziwa.
Makamu wa Pili war AIS wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akiagiza kufanyiwa matengenezo mara Moja Mashine ya uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa wa maziwa iliyopo Maruhubi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman akielezea kutoridhishwa na hali halisi ya mazingira ya Kituo cha uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa wa maziwa kilichopo Maruhubi.

                                                 Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewakumbusha Watu wenye uwezo Nchini kuendelea kujenga Nyumba za Ibada ili kufikia Daraja la Ucha Mungu utakaowaletea Uongofu katika maisha yao ya sasa na Milele.

Akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu baada ya kufungua  Rasmi Masjid Al - Rahma iliyopo Saateni Pinda Mgongo uzinduzi ulioambatana na Ibara ya Sala ya Ijumaa Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema katika kutekeleza Ibada ni lazima kuwepo kwa Imani iliyokamilika hata kwa ujenzi wa Jengo dogo.

Alisema wapo baadhi ya Watu wenye uwezo mkubwa wanaoendeleza tabia na kauli ya kuzunguumkwa na hali duni ya maisha lakini wakati huo huo Watu hao Mitaani wanaporomosha Majengo ya Ghorofa kinyume kabisa na kauli wanazozitoa mbele za wenzao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Waumini na Watu mbali mbali waliojitokeza kuimaisha Nyumba hiyo ya Ibara na kusema kwamba itapendeza pale Uongozi wa Msikiti huo utakapokuwa sababu ya kuwaunganisha Waumini wanaopata huduma za ununuzi wa bidhaa sokoni hapo.

Aliwaomba Wafanyabiashara  kuendelea kutumia utaratibu uliowekwa na Serikali wa kulipa Kodi ili zile changamoto zinazowazunguuka Wananchi katika maeneo yao zipatiwe ufumbuzi kutokana na makusanyo ya Kodi hizo ambazo hazitakuwa na mjadala.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwahakikishia Waumini na Wafanyabiashara hao wa Soko la Saateni na Masoko  mengine Nchini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshajipanga katika kuwajengea mazingira bora Wafanyabiashara wake waote.

Akisoma Risala ya Waumini wa Msikiti huo wa Rahma wa Saateni Pinda Mongo Mmoja wa Kiongozi wao Ustadhi Khamis Hamad Khamis alisema wazo la kuuhuisha Msikiti huo awali uliojengwa kwa makuti limekuja kutokana na Waumini wa eneo hilo la biashara  kupata changamoto wakati wanapotaka kutekeleza Ibada ya Sala.

Ustaadhi Khamis Hamad alisema inatia moyo kuona kwamba waumini wenye licha ya kutoa michango ya hiari lakini pia baadhi yao walijitolea kufanya huduma stahiki za msikiti huo bila ya malipo kama inavyokuwa kwa Misiki mengine hapa Nchini.

Akifafanua changamoto zinazowasumbua Waumini wa Masjib Al Rahma kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kuzungumza na Waumini wa Msikiti huo Mkuu wa Wilaya ya Mjini Nd. Rashid Simai  Msaraka alisema Serikali ya Wilaya tayari imeshajipanga kupambana na Janga la Dawa za Kulevya.

Nd. Msaraka alisema mkazo Zaidi utawekwa katika kuimarisha ulinzi kwa kuzuia miyanya inayosababisha na kuchangia uingizwaji wa dawa hizo haramu hata katika maeneo yasiyo rasmi.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar kuhakikisha kwamba Mashine inayotumika katika uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa wa maziwa inarejea katika uhalisia wake ndani ya kipindi kifupi.

Alisema Wizara hiyo lazima itafute Euro Elfu Tano sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 15,000,000/- kwa gharama zozote ili Mashine hiyo irejee uzalishaji wake wa kawaida kwa kutoa Lita Kumi za Maziwa ya Mbegu kwa saa Moja badala ya Lita Tatu zinazopatikana hivi sasa kutokana na kufa kwa Moja ya kifaa muhimu.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya ghafla katika Kituo cha uzalishaji wa Mbegu Bora za Ngombe wa Maziwa kilichopo Mtaa wa Maruhuri na kusikitishwa na hali halisi ya Mazingira isiyoridhisha ya Kituo hicho.

Alisema Kituo cha uzalishaji wa Mbegu Bora za Ng’ombe wa Kisasa wa Maziwa ni eneo muhimu katika kukuza Uchumi wa Taifa unaokwenda sambamba na ongezeko kubwa  la upatikanaji wa Ajira kwa Wananchi wanaojihusisha moja kwa moja na masuala ya Ufugaji.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba kutengenezeka kwa Mashine hiyo kutasaidia kuwajengea uwezo Wafugaji Nchini jambo ambaloWizara inayosimamia masuala ya Ufugaji inapaswa kuwa na Mikakati za ziada katika makusudio yake ya kuongeza uzalishaji katika eneo hilo muhimu la Ufugaji.

“ Wizara lazima isimamie vizuri suala hili muhimu la Mashine hii iliyonunuliwa kwa Fedha za  Serikali Kuu kwa gharama kubwa ya Zaidi ya Shilingi Milioni Mia 500,000,000/-“. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kupitia Kituo hicho kuimarisha Mazingira ya eneo hilo yanayoonekana kutupwa bila ya uangalizi Maalum

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya  Maendeleo ya Mifugo Zanzibar Bibi Asha Zahran Mohamed alisema Mashine hiyo ya uzalishaji wa mbegu bora za Ng’ombe wa Kisasa wa Maziwa umefanyiwa matengenezo baada ya kupata hitilafu mapema Januari Mwaka 2020 na kubainika uwepo wa uchakavu wa Kifaa kinachozalisha Hewa na Nitrogen.

Bibi Asha alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Kituo hicho ulichukuwa hatua za kuiarifu Wizara iliyoambatana na barua ya maombi ya ununuzi wa Kifaa hicho ili uzalishaji urejee kikawaida.

Mkurugenzi huyo wa Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar alifahamisha kwamba kwa mujibu wa sensa ya uzalishaji wa Maziwa ya Mwaka 2020 Zanzibar inazalisha Lita 20,075   za Maziwa ambayo soko lake bado halijawa la kuaminika.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Ng’ombe wa Maziwa wa Kituo hicho Nd. Faki Ame Keis alisema ukosefu wa Hewa na Nitrogen katika mfumo wa kupandishia mbegu katikia Mashine hiyo huchangia kupunguza uzalishaji.

Nd. Faki alisema Mashine hiyo hivi sasa ina uwezo wa kuzalisha Maziwa Lita Tatu kwa saa Moja badala ya Lita Kumi kwa ajili ya Mbegu Bora za Ng’ombe wa Kisasa wa Maziwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.