Habari za Punde

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akutana na wasanii

Balozi wa hati miliki Barani Afrika ambae pia ni msanii wa filamu nchini  Salum Stika akielezea changamoto zinazowakabili wasanii katika kazi  sanaa  katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zamzibar. 

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe: Tabia Maulid Mwita  akizungumza na wasanii wa vikundi mbalimbali vya sanaa kuhusu na  kuinua vipaji vya wasanii  hao katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zamzibar. 

Picha na Rahima Mohamed /Maelezo

Na Rahma Khamis Maelezo               22/1/2021

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe: Tabia Maulid Mwita amewataka wasanii wa Zanzibar kuwa wabunifu katika kazi zao ili kukuza na kuinua vipaji vya usanii nchini.

  Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo wakati alipokutana na wasanii mbalimbali kusikiliza changamoto zinazowakabili katika kazi zao ili kupatiwa ufumbuzi.

Amesema wasanii wa Zanzibar wanajitahidi katika kazi mbalimbali lakini hawafikii malengo kutokana na kutokuwa na ubunifu wa kubuni mbinu mpya ya kuendeleza fani hivyo ipo haja kwa wasanii hao kujituma zaidi.

 Aidha amesema kuwa katika kutatua changamoto zinazowakabili wasanii Serikali itashirikiana nao ili kuwawezesha na kufahamishishana mbinu zaidi ili kufikia malengo ya kuinua vipaji vya Sanaa ikiwa ni kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi.

 “Kaeni kwa pamoja mshirikiane,msibaguane wala msidharauliane pangeni kitu halafu mtuletee sisi Wizara tutakusaidieni ili muinue Sanaa zenu msije mmoja mmoja mtakuwa hamfikii malengo”,Waziri Tabia alisema.

Waziri Tabia amewasisitiza wasanii kukaa pamoja na kuandaa mashindano na wasanii wengine  na kupeana uzoefu kwa kuendeleza vipaji ili kuweza kuinua soko la Sanaa Zanzibar.

Akizungumzia suala la utendaji Waziri amewataka watendaji wa sekta husika kusimamia na kufuatilia majukumu yao ipasavyo kwa kukaa na wasanii wao ili kuondoa malalamiko na kufufua vikundi vya Wizara ambavyo kwa sasa havipo tena.

Hata hivyo ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wasanii pamoja na  kuandaa kanuni maalum zitakazoweza kutanua soko la sanaa ndani nan je ya Nchi.

Wakitoa malalamiko yao wasanii kutoka vikundi mbalimbali wameiomba Serikali kuweka mfuko malum utakao weza kuwasadia wasanii wa Zanzibar katika kutatua baadhi ya matatizo yao.

Aidha wamefahamisha kuwa iwapo watapatiwa miradi mbalimbali kupitia Sanaa zao itawawezesha kuendeleza vipaji na kuingiza pato la Taifa

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.