Habari za Punde

Diwani: Wananchi wanapaswa kujua kila kata inatakiwa kuwa na shule moja yu ya kata

Na Hamida Kamchalla.

WANANCHI wa kata ya Maweni waishio mitaa ya Kasera wameiomba serikali kuwatafutia eneo la kujenga shule ya sekondari kutokana wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule ya kata ambayo ni Maweni sekondari.

Wakiongea na mwandishi wetu na wananchi hao wamesema kuwa watoto wao wamekuwa wakipata adha ya kutembea umbali wa kilomita takribani 4 mpaka 6 kufuata shule hiyo iliyopo mbali na mazingira wanayoishi.

Wamefafanua kusikitishwa kwao na hali ya kata hiyo huku wakidai mtaa huo hao hauna huduma muhimu karibu kama zahanati, shule pamoja na ofisi za serikali ambazo zote ziko mtaa wa Kange  jambo linalopelekea wananchi hao kufuata huduma hizo katika mtaa wa Masiwani ambao upo jirani na maeneo yao.

"Mtaa wetu ni kama hauna kiongozi yoyote maana hatuna hata dispensari, hatuna ofisi za serikali hapa na kama hivi shule ya kata ndio iko huko juu, jambo hili linatusikitisha sana, ebu hao viongozi watutafutie hata maeneo ya kujengea shule ya sekondari ili kuwapunguzia watoto wetu mwendo, watoto wakirudi wamechoka hata shuhuli ndogondogo za nyumbani zinawashinda" alisema mzazi aliyejitambulisha kwa jina la mama Salma.

Aidha walidai kuwa serikali inapaswa kutambua kuwa mji kwa sasa umekua na watu wameongezeka hivyo huduma muhimu zinatakiwa ziwafuate wananchi badala ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma na kuongeza kuwa wapo tayari kujitolea nguvu kazi na hata kuchangia ujenzi wa shule endapo serikali itatenga eneo.

Hata hivyo nipashe ilifanikiwa kuongea na diwani wa kata ya Maweni Joseph Colyvas ambaye alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kufafanua kwamba kila kata inatakiwa kuwa na shule moja bila kujali umbali wanaotoka wanafunzi lakini tayari wameshaanza mchakato wa maombi ya kugawanywa kwa kata hiyo.

Colyvas alisema kuwa kutokana na ukubwa wa kata hiyo wamepeleka maombi ya kugawanywa kata tatu ambazo ni Kange, Kichangani na Kasera ili kuepusha usumbufu wa upatikanaji wa huduma na kuongeza kuwa wapo wanafunzi wanaotembea kilomita nane wakitokea mitaa ya Mwisho wa shamba na maeneo ya Chote.

"Suala la umbali wa shule nataka ieleweke kwanza kwamba kila kata inatakiwa iwe na shule moja ya kata ya sekondari, kuhusu huduma ya zahanati tayari iko kwenye maombi lakini ili tupate huduma kwa ukaribu hii kata igawanywe ndipo huduma zitasogea kwa wananchi, na kuhusu suala la ofisi za serikali za mitaa zote zipo ifisi ya kata lakini kwa mtaa wa Kasera wanatakiwa kuanza ujenzi wa ofisi yao" alifafanua Colyvas.

"Kata ya Maweni ni kubwa sana ambayo ikigawanywa inatoka kata tatu, maombi tuliyopeleka ni kugawanywa kata za Kange, Kichangani na Kasera, hivyo wananchi wanaoaswa kuelewa hilo na sasa hivi tunasubiri majibu ya maombi tetu" aliongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.