Baadhi ya Wajumbe wa Kikosi Kazi cha Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP) wakionyesha kutokuridhika kwao na hali ya uchafu katika mtaro uliopo kwa Biziredi wakati wa ziara ya kutembelea maeneo hatarishi ya maradhi ya mripuko
Huu ndio hali halisi ya muonekano mtaro ambao umetuama uchafu katika eneo la Biziredi.
PICHA ZOTE NA KHADIJA KHAMIS - MAELEZO ZANZIBAR
Na Kijakazi Abdalla Maelezo 7/02/2021
Baraza la Manispaa Mjini limetakiwa kushirikiana na wafanyabiashara kuhakikisha mitaro ya maji machafu inakuwa safi ili kujiepusha na maradhi ya mripuko.
Hayo ameyasema Mkurugenzi wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Makame Khatibu Makame wakati alipofanya ziara akiwa na kikosi kazi cha kukabiliana na maradhi ya kipindupindu (ZACCEP) katika mtaro uliopita biziredi kuelekea Gulioni .
Ameonyesha kutoridhishwa na hali ya mtaro huo kutokana na kujaa uchafu jambo ambalo linaweza kusababisha mripuko wa maradhi ya matumbo na kipindupindu.
Alilitaka Baraza la Manispaa kuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya maduka na mitaro ili kuweza kudhibiti uchafu ambao unaweza kuleta madhara kwa wananchi.
Aidha Mkurugenzi Makame amewashauri wafanya biashara kujenga utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo yao na kuhifadhi taka katika sehemu ambazo zitazuia kusambaa na kuingia katika mitaro na hatimae kuleta athari.
Kaimu Msaidizi Mkurugenzi Idara ya Maendeleo Huduma za jamii Baraza la Manispaa Mjini Said Soud Mtambuka amesema kuwa kuna baadhi ya nyumba katika eneo hilo zimekuwa zikitiririsha maji machafu katika mtaro huo jambo ambalo limekuwa likileta usumbufu kwa Baraza hilo.
Amesema kuwa suala la usafi ni la wananchi wote sio kwa kampuni pekee hivyo ni vyema kwa wananchi kushirikiana ili kudhibiti maradhi kusambaa.
Kaimu Mkurugenzi Soud amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa na dhana kuwa Baraza la Manispaa pekee ndilo lenye jukumu la kufanya usafi lakini jukumu hilo linawahusu wananchi wote wanaoishi ndani ya Manispaa husika.
Kaimu Mkurugenzi huyo ameyafungia baadhi ya maduka ambayo yamekaidi agizo la kuweka vyombo maalum veya kuhifadhia taka katika maeneo ya maduka yao.
Ziara za kutembelea maeneo yenye visababishi vya maradhi ya mripuko zitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuhakikisha usafi wa mazingira unaimarishwa ikiwa ni miongoni mwa Utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Kipindupindu Zanzibar (ZACCEP).
No comments:
Post a Comment