PICHA NA RAMADHANI ALI MAELEZO
Na Khadija Khamis- Maelezo Zanzibar 07/02/2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora Seif Shaaban Mwinyi amewataka wahitimu wa mafunzo ya ndoa kuwa na subira ustahamilivu na kusameheana katika kudumisha ndoa zao .
Hayo ameyaeleza wakati wa Sherehe ya Ufungaji wa Mafunzo ya kwanza ya Ndoa katika Wilaya ya Kaskazini B , ambapo jumla ya Wananchi 201 walihitimu mafunzo hayo ya wiki 10 Huko Mkoa ya Kaskazini, Mahonda.
Alifahamisha mafunzo ya ndoa yanajenga heshima na kila upande kujuwa haki yake ya msingi katika kuimarisha na kutunza familia .
Aidha alifahamisha kwamba mafunzo ya ndoa yatapunguza utitiri wa talaka ambao umeonesha kukidhiri kwa wingi hasa kwa vijana.
Naibu Mufti Mahmoud Mussa Wadi amewashauri wahitimu wa mafunzo hayo, ambao wengi wao ni watu wazima, kuyasambaza mafunzo hayo kwa vijana ambao hawajapata elimu ya ndoa.
Ameeleza matarajio makubwa kwa Mkoa wa Kaskazini unguja baada ya mafunzo hayo yatasaidia kupunguza mizozo ya ndoa ndani ya mkoa huo iwapo yatatumika kikamilifu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B,
Katibu Tawala Makame Machano Haji aliiomba Ofisi ya Mufti kuendeleza elimu ya ndoa katika maeneo mengine ya Wilaya ya Kaskazini B, ikiwemo Bumbwini Mahonda na Kiwenga.
Alisema kutolewa mafunzo hayo kutaepusha utoaji wa talaka kiholela pamoja na vitendo vya udhalilishaji ambayo vinaongoza katika Mkoa huo .
Nao Wahitimu hao wameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Mufti kwa kuwapatia elimu hiyo ambayo imewasaidia kuzijua haki zao.
Wametoa wito kwa vijana wenzao kushiriki katika mafunzo hayo ili kuweza kujuwa mambo mbali mbali ya sheria za kiislamu .
No comments:
Post a Comment