Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amezindua APP ya Sema na Rais Mwinyi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kuizindua APP ya Sema na Rais Mwinyi (SNRMWINYI ) katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar, akisisitiza jambo wakati akihutubia katika uzinduzi huo uliofanyika jana usiku 27-2-2021. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezindua mfumo wa “Sema na Rais Mwinyi (SNR Mwinyi)”, na kusisitiza kuwa amedhamiria kufanya hivyo ili kupata malalamiko ya wananchi wote kwa urahisi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizindua mfumo wa kumfikia malalamiko kutoka kwa wananchi “Sema na Rais Mwinyi”, hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni nje kidogo ya Jiji la Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo mke wa Rais Mama Mariam Mwinyi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo inatokana na matakwa ya wananchi ambapo mwaka jana 2020, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wakati alipokwenda kwa wananchi kuomba kura katika maeneo yao yakiwemo masoko, maeneo ya wajasiriamali, waanika dagaa, wakulima wa mwani wavuvi na kwengineko ambako walisisitiza kwamba watu wa serikali hawawafikii na malakamiko yao hayafiki.

Alisema kuwa hiyo ilikuwa katika azma yake na baada ya kuchaguliwa ameona ipo haja kwani bado wapo wananchi  ambao wanaeleza shida zao na kero zao hivyo, akaona umhimu wa kuzindua mfumo huo ambao ana matumaini kwamba njia hiyo itawafikia walio wengi.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni rahisi na itawasaidia wananchi wengi ambao watatunia njia tofauti kwa kutumia simu zao zikiweno sms, kupiga simu na kutumia tovuti maalum iliyowekwa.

Alisema kuwa mfumo huo utaelekeza suala zima la utekelezaji na utaonyesha ni nani hafanyi wajibu wake na utaonyesha ni nani analalamikiwa zaidi na yeye ndipo atakapotambua matatizo mengi yako wapi na hatua gani afanye.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wale ambao hawatokuwa na jitihada hatua za kuwawajibisha zitachukuliwa na kutaka kila mtendaji wa taasisi yoyote ya  serikalikatika mfumo huo atajua kama anafuatiliwa.

Alifahamisha kwamba malamiko yatafanyiwa kazi na pale itakapoonekana kuna udhaifu kutoka kwa watendaji husika hatua za makusudi zitachukuliwa.

Alitoa pongeza kwa vijana wa Kampuni ya RAHISI ya Zanzibar waliotengeza mfumo huo na kueleza kwamba mfumo huo wote umefanywa kwa ufadhili na si kwa fedha za serikali na kutoa pongezi kwa wale wote waliotoa mchango wao katika kufanikisha jambo hilo.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alisema kuwa mfumo huo utasaidia kutatua changamoto za hapa nchini sambamba na kuwahamasisha watumishi wa umma kuweza kuwajibika zaidi.

Aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha utumishi wa umma kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mapema Mkurugenzi wa Kampuni ya RAHISI Abdulrahim Hassan alisema kuwa mfumo huo ni wa pekee hapa nchini na katika Bara la Afrika ambao unaeleza kutekeleza ahadi za Rais Dk. Mwinyi na kutoa shukurani kwa Rais kwa kuwaamini vijana hao kutengeza mfumo huo.

Aidha, alisema kuwa mfumo huo umezingatia pande zote mbili ile ya wananchi na ile ya watendaji ambapo wanapokea malalamiko na juu yao kutakuwa na wasimamizi ambao wataangalia ni vipi changamoto hizo zinafanyiwa kazi na baadae kutakuwa na Meneja wa kuhakikisha changamoto zimefika na zinafanyiwa kazi ipasavyo.

Aidha, alisema kuwa katika mfumo huo pia, kutakuwa na wasimamizi ambao ni Makatibu Wakuu pamoja na Mawaziri na mwisho kabisa kutakuwa na Rais ambaye ataweza kuona hali ya malalamiko katika Taasisi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuona vipi zinafanyiwa kazi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa lengo la mfumo huo ni kutataa changamoto za wananchi ambapo itatumika simu janja na kupakuwa programu ya “Sema na Rais Mwinyi” ambapo pia alisema kuwa upo uwezekano wa kutumia tovutiya www.snrmwinyi.co.tz.

Aliongeza kwamba wale ambao hawana simu za aina ya “smartphone”, alionesha njia  maalum ya kuweza kufikisha ujumbe wao kwa kupiga namba ya simu hii ya 0772444449 na hata wale wenye simu ndogo maarufu simu za tochi.

Alisema kuwa changamoto hizo zinahifadhiwa na zitakuwa siri na pia kila lalamiko litapewa nambari ya kumbukumbu na namba ya siri ambayo atapokea yule aliyotuma ili kuweza kufuatilia changamoto yake.

Alisema kuwa maafisa wafuatiliaji wote watapatiwa vifaa vya kazi ambapo kila changamoto itafanyiwa kazi kwa muda mfupi na wa haraka ambapo pia, taarifa zitaonesha idadi ya malalamiko ambapo pia alisema mfumo huo unaweza kutuma hata viamabatanisho vya ushahidi

Alisema kuwa kila kinachofanywa na mtendaji kitakuwa kinaonekana ili kuondoa ile hali ya kuhafilika na lalamiko likifika litakwenda moja kwa moja katika taasisi husika ambapo pia hatua hiyo itarahisisha changamoto pamoja na kuonesha wingi wa changamoto na vipi zinafanyiwa kazi.

Aliongeza kwamba  mfumo huo unaendelea kuimarishwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na bado huujafikia mwisho na maoni yanaendelea kupokelewa na kusisitiza kwamba mfumo huo si wa kutoa taarifa za umma za wananchi kama vile matatizo ya moto na mengine

Alisema kuwa pia, itaonesha taasisi ambayo inalalamikiwa sana pamoja na kuonesha umahiri kwa maafisa katika kutatua changamoto hizo ambapo pia wasimazizi watapata kuona malalamiko kwa kila siku na kuona vipi yamefanyiwa ufumbuzi.

Akitoa neno la shukurani Mbunge wa Jimbo la Mpendae Taufiq Salim Turky alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kusimamia uadilifu nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Serikali ya Umoja wa Kimaifa inaimarika sambamba na kuiimarisha Zanzibar kiuchumi.

Alitoa pongezi kwa juhudi za Rais Dk. Mwinyi za kuhakikisha anafanya Mapinduzi ya kiuchumi huku akitoa pongezi kwa Tanzania kwa kuwa na viongozi waadilifu akiwemo Rais Dk. Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa uchumi wa kweli hauwezi kupatikana kama hakuna mtu wa kuyasimamia malamiko na  kero za wananchi huku akitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuchagua watendaji wenye sifa za kuongoza.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.