Habari za Punde

Kamati ya ushauri ya utekelezaji mradi wa viungo yaundwa

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara Zanzibar Dkt,Islam Seif Salum akibadilishana mawazo na Mkurugenzi mtendaji wa taasisi inayojihusisha na uhifadhi wa misitu Pemba (CFP) Mbarouk Mussa Omar mara baada ya kuzinduliwa kwa kamati ya ushauri dhidi ya mradi wa Viungo.


Mkurugenzi wa shirika la People Development Forume (PDF) Jurua Kizito akizungumza na Msimamizi mkuu wa mradi wa Viungo kanda ya Unguja Amina Ussi Khamis.
Picha ya pamoja kwa baadhi ya wanakamati ya ushauri katika utekelezaji wa mradi wa Viungo.

 Katibu Mkuu Wizara ya Biashara Zanzibar Dkt,Islam Seif Salum akizungumza wakati akizindua kamati ya ushauri ya utekelezaji wa mradi wa viungo ilioshirikisha wakurugenzi tofauti wa taasisi husika za Serikali na binafsi katika ukumbi wa mamlaka ya huduma za nishati na maji Zanzibar (ZURA)

 


Muhammed Khamis,TAMWA-Z’bar

 

Katibu mkuu Wizara ya Biashara Zanzibar Dkt,Islam Seif Salum amesema ujio wa mradi wa viungo visiwani hapa umekuja wakati sahihi na utasaidia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa ahadi za Raisi wa Zanzibar Dkt,Hussein Ali  Hassan Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

 

Ameyasema hayo katika ukumbi wa mamlaka ya huduma za nishati na maji Zanzibar (ZURA)alipokua akizindua kamati ya ushauri ya utekelezaji wa mradi wa viungo ilioshirikisha wakurugenzi tofauti wa taasisi husika za Serikali na binafsi.

 

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina matarajio makubwa kupitia mradi huo na kwamba utekelezaji wake utaisaidia ikiwemo kuwaletea maendeleo ya wananchi sambamba na kukuza ajira binafsi.

 

Akiendelea kufafanua zaidi alisema kwa muda mrefu wakulima wa Zanzibar wamekua wakikabiliwa na chanagmoto mbali za uzalishaji wa mazao bora ambayo huwapelekea kukosa soko la kimataifa.


‘’Kwa mkakati huu wa mradi ni wazi kuwa sasa wakulima wengi Zanzibar wataondokana na shida ya masoko ya bidhaa zao badala yake watakwenda kuziona fursa mpya za kilimo ambazo zitawaingizia kipato kikubwa’’aliongezea.

 

Katika hatua nyengine katibu mkuu huyo alisema Serikali imedhamiria kukuza pia bidhaa za wajasiriamali wa ndani pamoja na kutengeneza mazingira ya viwanda vidogo vidogo pamoja na kuzipa hadhi bidhaa zinazotengenezwa na wanachi wenyewe.

 

Kwa upande wake Meneja mkuu wa mradi huo kanda ya Unguja Amina Ussi Khamis alisema mradi huo utatoa fursa kwa wakulima wapatao 21,000 kutoka takribani shehia 50 za Unguja na Pemba.

 

Alieleza kuwa kilimo kitakachohusika ni mboga mboga matunda na viungo sambamba na kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na wakulima.

 

Pamoja na hayo alieleza kuwa mradi huo pia utafungua fursa za masoko ya kimataifa kwa bidhaa zinazolimwa na wakulima kutoka visiwani hapa kupitia mkakati maalumu ambau utaanzishwa na kuratibiwa vyema.


Awali Mkurugenzi mtendaji wa taasisi inayojihusisha na uhifadhi wa misitu Pemba (CFP)Mbarouk Mussa alieleza kuwa kuwepo kwa mradi huo kutaleta mabadiliko makubwa kwenye jamii.

     

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.