Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania Dkt.Anna Peter Makakala (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha akiwa na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu
 

IDARA ya Uhamiaji imepongezwa kwa kuendelea kutekeleza vyema majukumu yake sambamba na kuanza kutafuta muwarubaini wa changamoto ya foleni za wageni ndani ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alitoa pongezi hizo leowakati alipokuwa na mazungumzo na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Peter Makakala, aliyefika Ikulu Jijini Zanzibar, kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Idara hiyo ya Uhamiaji kwa kuanza kuzifanyia kazi changamoto zilizokuwepo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani karume hatua ambayo itapunguza foleni kwa wasafiri wakiwemo wageni ambao lengo ni warudi tena kuja kuitembelea Zanzibar.

Alisema kuwa changamoto ya foleni ilikuwa ikiwasumbua sana wasafiri wakiwemo wageni hasa ikizingatiwa kwamba uwanja wa ndege huo ni lango la watalii kutoka nje ya nchi hivyo, kupatikana na ufumbuzi huo kutaweza kusaidia.

Aliongeza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha jengo jipya la uwanja wa ndege litakapoanza kazi changamoto kama hizo hazijitokezi.

Alipongeza kwa kuongeza kwa madawati na kufikia 28 ambazo zimeanza kusaidia na kupunguza foleni katika uwanja wa ndege huo hasa pale wakati zinazotua ndege nyingi kutoka nje kwa wakati mmoja.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa kuzifanyia kazi changamoto hizo na kupelekea kuongeza madawati katika uwanja huo wa ndege wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alitoa ushauri kwa Idara hiyo ya Uhamiaji kuwa ni vyema kuhakikisha kila mgeni anaekuja awe ameshapata VISA yake ili kuondosha kukaa foleni muda mrefu katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kulitafuatia ufumbuzi tatizo la mfumo wa Uhamiaji kuwa chini na kupelekea kuchelewa kwa wageni na kusababisha foleni.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kwa vile uchumi wa Zanzibar unaitegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii hivyo, ni vyema kwa kila mdau kwa upande wake akahakikisha anatoa mchango wake katika kufanikisha jambo hilo.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Idara hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya ya kushiriki katika kuleta amani nchini katika wakati wa uchaguzi hatua ambayo bado wanaendelea nayo.

Aidha, alipokea pongezi za kushinda nafasi ya kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba 2020.

Mapema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Peter Makakala alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi uliopoita wa Oktoba 2020 na kuwa Rais wa Zanzibar Awamu ya Nane.

Dk. Makakala alitoa shukurani zake yeye pamoja na Idara yake ya Uhamiaji na kupongeza mashirikaino yaliopo kati yake na Kamishna wa Uhamiaji wa Zanzibar Johari Masoud Sururu hatua ambayo alisema inazidi kuiimarisha Idara hiyo.

Alisema kuwa kazi za Idara hiyo zitaendelea kuimarishwa kwa weledi na kutoa ushirikiano sambamba na kupokea maelezo kwa Rais Dk. Mwinyi ili kuimarisha vyema kazi za Idara hiyo.

Alisema kuwa Idara hiyo imeimarisha mifumo ya utoaji wa huduma na kuimarisha mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambapo tayari wameshaanza kutoa pasi za kusafiria za elektroniki ambapo pasi hiyo iliweza kushinda kimataifa.

Aidha, alisema kuwa Idara hiyo inatoa VIZA kwenye mitandao, vibali vya ukaazi pamoja na udhibiti wa mipaka ambapo hatua hiyo imeweza kuimarisha mapato kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa tokea mifumo hiyo ianze mapato yameweza kuongezeka ambapo mnamo mwaka 2015 kabla ya kutumika kwa njia ya mifumo ya mtandao Idara hiyo ilikusanya Bilioni 10 kwa upande wa Zanzibar na mwaka 2016 ilikusanya Bilioni 17.7  ambapo mwaka 2017 ilikusanya Bilioni 23.

Aliendelea kueleza kwamba kuanzia mwaka 2018 walipoanza kutumia mfumo mtandao Idara hiyo iliweza kukusanya bilioni 28.9 na mwaka 2019 ilikusanya bilioni 31 ambapo mwaka 2020 ilikusanya bilioni 33 licha ya kuwepo changamoto kadha ikiwemo ugonjwa wa Covid 19.

Pamoja na hayo,Kamishna Jenerali huyo alisema kuwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar kumekuwa na changamoto ya kupambana katika kutoa huduma bora kwa watalii na wananchi kutokana na ndege kutua kwa wakati mmoja sambamba na uwanja mmoja kutumia ndege za ndani na nje.

Alisema kuwa  licha ya hali hiyo kutokana na kuimarisha mifumo wameweza kuongeza madawati na kufikia 28 na kuweza kutoa huduma ambapo ndege yenye abiria 400 wanaweza kuhudumia kwa saa moja.

Pia, kutokana na uhaba wa wafanyakazi wa Idara hiyo imeweza kuongeza wafanyakazi kutoka 68 na kufikia 113 huku wakichukua juhudi ya kuomba Mamlaka ya uwanja wa ndege kupeana muda jambo ambalo limekubalika jambo ambalo litaleta faraja.

Kamishna  Jenerali huyo alieleza matarajio yake katika jengo jipya la uwanja wa ndegewa Abeid Amani Karume (Terminal III)  linalotarajiwa kunza  kazi hivi karibuni.

Alieleza juhudi zilizochukuliwa kiwanjani hapo ambapo abiria hivi sasa hana haja ya kupita katika sehemu nne za madawati kama ilivyokuwa hapo awali huku akieleza kwamba tayari wameshapata vifaa ambapo wageni wanaweza kulipa hapo hapo uwanjani iwapo watakuwa na kadi za benki.

Alisema kuwa mbali ya kusimamia ulinzi na usalama Idara hiyo imehakikisha inachangia mapato na uchumi wa nchi sambamba na kuendelea na kazi zake za kufanya misako mbali mbali nchi nzima ili kuhakikisha wahamiaji haramu wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu wanachukuliwa hatua stahili.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.