Habari za Punde

Waumini wa Msikiti wa Miembeni Watoa Shukrani Zao kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi Kwa Mchango Wake.

 

Imamu wa Skiti wa Miembeni Wilaya ya Mjini Unguja Sheikh Khalid Ali Mfaume akitowa shukrani kwa niaba ya Waumini wa Msikiti huu kwa mchango wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi kumalizia sehemu ya ujenzi, hafla hiyo imefanyika baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika leo 19-2-2021.

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Miembeni Jijini Zanzibar wametoa shukurani zao kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyikwa juhudi zake za kuiimarisha dini ya Kiislamu.

Waumini hao walitoa shukurani zao hizo leo mara baada ya Sala ya Ijumaa ambapo Alhaj Dk. Mwinyi aliungana nao katika msikiti huo na kueleza shukurani zao hizo kufuatia hatua zilizochukuliwa na Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuwaunga mkono katika ukarabati wa dari la msikiti huo maarufu hapa Zanzibarkwa kipindi kifupi.

Akitoa shukurani hizo kwa niaba ya Waumini wa Msikiti huo, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alieleza kwamba Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na Waumini wa Msikiti huo katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mara moja na hatimae waumini hao wanafanya ibada zao vyema.

Mapema katika hotuba ya Sala ya Ijumaa Katibu huyo wa Mufti ambaye pia, ni Khatibu wa Msikiti huo alieleza haja kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutokuwa wabahili na kuwataka katika maisha yao kutoa sadaka kabla mauti hayajawafika.

Sambamba na hayo, Sheikh Khalid aliwataka Waumini wa dini hiyo kuendelea kumuombea dua Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwani katika siku zake za mwisho ndani ya miezi hii miwili na nusu alikuwa akihubiri amani, utulivu, mshikamano na maridhiano ambayo ndio tunu ya Wazanzibari.

Sheikh Khalid alimnukuu Malim Seif Sharif Hamad pale aliposema katika hotuba yake mara baada ya kuapishwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ikulu jijini Zanzibar mnamo Disemba 8, 2020 ambapo alimnukuualiposema “ Mheshimiwa Rais mwisho nitoe wito kwa Wazanzibari wote waliopo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa maridhiano”.

Katibu huyo wa Mufti alieleza utamaduni aliokuwa nao Maalim Seif wa kuzungumza na Waumini wa dini ya Kiislamu kila Ijumaa mara baada ya kumaliza sala ambapo katika mazungumzo yake aliwa akihubiri umoja na mshikamano.

Alirejea kauli ya  Mlezi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Zubeir Kabwe aliyoitoa hapo jana (17.02.2021) katika mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika huko kijijini kwao Nyali Mtambwe, kisiwani Pemba ambapo alimnukuu maneno yake aliyokuwa akisema kwamba anaimani na Rais Dk. Hussein Mwinyi.

Katibu huyo wa Mufti alieleza kwamba Maalim Seif alikuwa akihubiri umoja na kusema kuwa hatua zake za kushiriki katika maridhiano zimeweza kupelekea amani na utulivu kuzidi kuimarika hapa Zanzibar.

Aidha, Sheikh Khalid alieleza jinsi Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad katika uhai wake alivyokuwa akisisitiza suala zima la kupambana na vitendo vya udhalilishaji  kwa watoto huku akiitaka Ofisi ya Mufti kusimama kidete katika kuhakikisha vitendo hivyo havitokei.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.