Habari za Punde

Mama Samia mgeni rasmin katika Hafla ya Harambee ya kuchangia Mfuko wa Forum for African Woman Educationalis Zanzibar (FAWE)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Forum for African Woman Educationalis Zanzibar (FAWE) Dkt. Mwatima Abdalla Juma  kwenye Hafla ya Harambee ya kuchangia Mfuko wa Forum for African Woman Educationalis Zanzibar (FAWE) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo March 06, 2021  katika Ukumbi wa Serena Shangani Mjini Zanzibar, yenye kauli mbiu ya kumuelimisha Mtoto wa Kike ni kuiwezesha Jamii.  (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi Tuzo kwa Mwakilishi wa Taasisi ya Zanlink  Zanzibar  Bibi Yusrat Mkwale  kwa kutambua mchango wa Taasisi hiyo wa kuichangia Taasisi ya Forum for African Woman Educationalism Zanzibar (FAWE) ) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo March 06, 2021 katika  Ukumbi wa Serena Shangani  Mjini Zanzibar,  yenye kauli mbiu ya "kumuelimisha Mtoto wa Kike ni kuiwezesha Jami


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi Tuzo kwa Mwakilishi wa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Bibi Eshe Haji Ramadhani kwa kutambua mchango wa Taasisi hiyo wa kuichangia Taasisi ya Forum for African Woman Educationalism Zanzibar (FAWE) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo March 06, 2021 katika Ukumbi wa Serena Shangani Mjini Zanzibar  yenye kauli mbiu ya "kumuelimisha Mtoto wa Kike ni kuiwezesha Jamii".


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye Hafla ya Harambee ya kuchangia Mfuko wa Forum for African Woman Educationalis Zanzibar (FAWE) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo March 06, 2021 katika Ukumbu wa Serena Shangani Mjini Zanzinar, yenye "kauli mbiu ya kumuelimisha Mtoto wa Kike ni kuiwezesha Jamii".
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikabidhi Tuzo maalum kwa Mwakilishi wa Taasisi ya DollHouse Boutique Bibi Khaitham Salim Turky kwa kutambua mchango wa Taasisi hiyo wa kuichangia Taasisi ya Forum for African Woman Educationalism Zanzibar (FAWE) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani leo March 06, 2021 katika Ukumbi wa Serena Shangani Mjini Zanzibar, yenye kauli mbiu ya  "kumuelimisha Mtoto wa Kike ni kuiwezesha Jamii".


MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA

KWENYE HAFLA YA HARAMBEE YA FAWE ZANZIBAR KATIKA

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

TAREHE 06 MACHI, 2021

HOTELI YA SERENA, ZANZIBAR

 

Waheshimiwa Mawaziri;

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini;

Viongozi wa Vyama na Serikali;

Mwenyekiti wa FAWE Zanzibar;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

 

Habari za jioni

Assalam alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Niungane na walionitangulia kumshukuru Allah SWT kwa kutukutanisha leo kwa ajili ya hafla hii ya kuchangia FAWE Zanzibar.  Nichukue nafasi hii, kuushukuru Uongozi wa FAWE Zanzibar kwa mwaliko huu. Tunafanya ‘harambee’ hii kumchangia mtoto wa kike kuhamasika kusoma masomo ya Sayansi.

 

Sote ni mashahidi kuwa karne hii ya 21 ni karne ya Sayansi na Teknolojia inayoendeshwa na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.  Ili sote tuweze kunufaika na fursa mbalimbali za Mapinduzi haya ya Viwanda na kuhakikisha kwamba hakuna mtu   anaachwa nyuma katika safari ya Maendeleo, jitihada lazima zifanywe kumkomboa Mtoto wa Kike kwa kumuandalia njia ya kujiamini katika Maisha yake yanayotawaliwa na mageuzi ya kisayansi na ubunifu wa mifumo ya Kiteknolojia.

 

Hafla hii imeandaliwa ndani ya Juma hili lililojaa shamra shamra za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Kwa maana ya kwamba imeandaliwa wakati ndiwo (kwa Kiingereza this event has come at an opportune moment). Siku ya wanawake Duniani inatoa fursa kwa Serikali, Taasisi zisizo za Serikali na wadau mbalimbali kutathmini jinsi wanavyotekeleza harakati za kumjengea uwezo na kumkomboa Mwanamke na Mtoto wa kike, kuhakikisha kuwa anakuwa na sauti thabit katika jamii na kuchangia kwenye Maendeleo ya jamii yake na Taifa kwa ujumla, katika nyanja zote za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.

 

Nitumie fursa hii kukupongezeni wana-FAWE kwa kuendelea na wajibu wa kumpigania mwanamke kwa miaka 23 sasa tangu kuanzishwa kwake.    Katika kipindi chote hicho, FAWE Zbar Chapter imekuwa ni chachu katika kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wa kike wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi za elimu, uchumi, na haki za kijamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, kwa maendeleo ya wote.  

 

FAWE kama alivyosema Mwenyekiti wao wamekuwa mstari wa mbele katika kumuinua na kumuendeleza mtoto wa kike, pia kwa kuhamasisha ushiriki wa mwanamke katika uchumi kwa njia ya kuwaelimisha na kuwapatia fursa mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi.

 

Nafahamu wamekuwa wakifanya hivi kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu.  Ushirikiano huu umeweza kuzaa matunda makubwa kama alivyoainisha na Mwenyekiti kwamba kumekuwa na miradi wanayoitekeleza ambayo inapata baraka, na maelekezo ya kisera na kisheria kutoka Serikalini (Miradi gani?) Hongereni sana FAWE kwa kuwa wadau wakubwa wa elimu hususan katika kumuendeleza    mtoto wa kike.

Hapa niweke mkazo kuwa mapambano haya ya kumkomboa mwanamke na mtoto wa kike bila ushiriki wa wanaume ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.  Mbali na kwamba maeneo mengi ya maamuzi yamekaliwa na wanaume, bali kuna haja ya kuhakikisha kuwa Wananchi sote kike kwa kiume lazima tuwafikiane na hatua tunazochukua katika safari yetu ya maendeleo, na kwamba sote lazima tushiriki (ATE).  Hili litawezekana ikiwa wananchi wote wataelimika na kuelewa umuhimu wa kuwaendeleza watoto wetu wote bila ubaguzi. Tumekuwa tukitekeleza masuala ya uwiano wa kijinsia kisiasa zaidi kuliko kiuhalisia.

 

Katika kutekeleza majukumu yake, tumeambiwa kuwa kupitia programu mbalimbali zilizotajwa hapa, FAWE wamesaidia wanafunzi wengi wa kike (zaidi ya elfu 3000 tokea mwaka 2001 hadi sasa) kutoka kwenye kaya maskini kufikia malengo ya kupata elimu.  Vile vile, imeelezwa kuwa FAWE haikuishia tu kwa watoto wa kike na masomo ya sayansi, ila wameenda mbali zaidi na kuhakikisha wale watoto wa kike walioshindwa kuendelea na shule wanajikwamua? Tumewasikia namna walivyoweza kuwaweka wanawake hawa kwenye vikundi mbalimbali vya wajasiriamali wadogo kwenye kilimo cha mwani. (Kuwafuatilia maendeleo yao, wako wapi na wanafanya nini?).

 

Hivyo nitoe rai kwa wadau mbalimbali ikiwemo Wizara na Taasisi za Serikali zinazohusika na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kuhakikisha wanawaandalia wajasiriamali hawa mazingira wezeshi, rafiki na yenye tija.  Hapa namaanisha kuwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali, kuwaunganisha na taasisi za fedha zenye kutoa mikopo yenye riba nafuu, mifuko ya kusaidia wajasiriamali (Khalifa Fund), kuwaunganisha na masoko, kuwapa elimu ya kuongeza thamani bidhaa zao kabla ya kuingiza sokoni.

 

Tukiweza kuwajengea mazingira mazuri ya kibiashara, Wafaidika hawa wataweza hata kuchangia mfuko wa FAWE na kupunguza adha ya kutegemea wahisani hata kwa mambo madogo madogo. Nasema hivi kwa kuwa tumemsikia Mwenyekiti akisema kuwa kwa sasa wanakosa misaada mingi kutokana na wahisani wengi kuhamishia fedha zao kwenye masuala ya afya kutokana na janga la Corona. Wanasema mtegemea cha ndugu hufa masikini. Wakati umefika sasa, mbali na juhudi za aina hii ya kutafuta fedha za kuendesha kazi na kutekeleza miradi, kuna haja ya kuangalia vyanzo vya mapato vitakavyokuwa endelevu, ili taasisi iweze kujitegemea. Vikundi vya wajasiriamali tunavyovisimamia vikizalisha kibiashara vitasaidia kwenye kapu lenu na kuweza kusomesha wanafunzi wengi zaidi, na vile vile, kuajiri wanawake wengi zaidi; kuinua uchumi wa wana vikundi pamoja na kuchangia pato la Taifa.

 

Ndugu zangu:   Vya kupewa huja kwa wakati ambao mtoaji huona ndio sawa, na wakati mwengine huja na masharti mengi.  Tujifunze kujitegemea, tufunge kibwebwe tutafute vyetu.  Nimeona nilisema hili kwa kuwa najua kuna baadhi ya Programu zimesimamishwa na nyingine kutoanza kabisa kutokana na kukosa fedha za wahisani.

 

Ndugu Wana-FAWE, Wageni Waalikwa,

Tunapokwenda kutekeleza Dhima na Dira ya Tanzania kuwa ni nchi itakayojengwa na uchumi wa viwanda, ni dhahili kuwa kutakuwa na mahitaji makubwa ya wataalamu wa Sayansi katika fani mbalimbali.  Hivyo, upo umuhimu mkubwa kwa wanafunzi wa kike kujikita katika masomo ya Sayansi na Teknolojia ili tuzalishe wataalamu wa kike watakaoweza kutumikia uchumi wa viwanda katika sekta mbalimbali.  Kwa upande wa Zanzibar, Serikali inajipanga kujikita kwenye masuala ya uchumi wa buluu (Mafuta na Gesi, Mwani Uvuvi wa Bahari kuu na Uvuvi wa Vizimba), ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza thamani mazao ya Baharini na ujenzi wa bandari za kisasa.  Maeneo haya yote yanahitaji wataalamu wa kike na kiume ili kuweza kuendesha na kusimamia mitambo mbalimbali.  

 

Je tunajipanga vipi kuzitumia fursa hizi? Chuo cha Karume, Tunguu ZAYEDESA na DIT fursa muhimu tunajipangaje kuzitumia? Mbali na ajira za moja kwa moja Suala la local content tunawatayarishaje? Kupeleka chakula, matunda, mboga mboga, vinywaji etc.

 

Mtoto wa kike hadi leo bado anakabiliwa na mila potofu, ndoa za umri mdogo, na majukumu ya majumbani.  Ni jambo la kusikitisha kwamba bado tunaendelea kulalamika tu bila kuchukua hatua tiba za tatizo hilo.  Kama kuna baadhi ya Sera na Sheria kandamizi zinakwamisha maendeleo ya Watoto wa kike hasa kwenye elimu, tuzibainishe ni zipi? Tuitake Serikali ichukue hatua za marekebishoTumesema sana suala la mila potofu lakini bado zipo, kwanini? Kwa maoni yangu, Hakuna fursa za matumaini!!!  (Mfano; Baba mwenye wari wane nyumbani).

 

Fursa za masomo zikionekana kunufaisha watu, watoto wetu watapata ujasiri wa kusoma masomo ya sayansi kwa bidii kubwa (Maonesho ya wanawake wanasayansi Simu, irrigation scheme, umeme n.k). Serikali zetu zimechukua hatua ya kuimarisha hali za maskuli na kurejesha mambo yote yanayotakikana ili watoto wetu waweze kusoma na kufaulu masomo ya sayansi.

 

Serikali imeendelea kutoa elimu bure katika ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari.  Hii ni pamoja na kuimarisha mafunzo ya amali na elimu ya juu.   Kwa kipindi cha miaka tisa bajeti ya Sekta ya Elimu imeongezeka kwa asilimia 91.4 kutoka TSh. 93,468,089,000/= mwaka 2010/2011 hadi kufikia TSh. 178,917,149,000/= mwaka 2019/2020.  Ongezeko hili la bajeti limesaidia kuendeleza miundombinu ya elimu, na kuboresha zaidi mazingira ya kujifunza na kufundishia, kuweka vituo maalum vya masomo ya sayansi, kuongeza idadi ya walimu hasa wa Sayansi, pamoja na kuongeza vitendea kazi vikiwemo vitabu, pamoja na kuanzishwa skuli za watoto wa kike peke yao (kama shule ya Ben Bella).

 

Mbali na jitihada hizo, mifuko ya elimu ya juu nayo imeongeza bajeti ili kusomesha watoto wengi zaidi ngazi ya Chuo Kikuu. Serikali inaimarisha elimu ya ufundi, sayansi na teknolojia (Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) na DIT ipo kwenye mazungumzo.  Serikali inatimiza wajibu wake, hatuna budi nasi kuchangia nguvu zetu.

 

Ndugu Wageni Waalikwa,

Kutokana na ukweli huo, napenda kutoa shukurani kwa wote waliotoa wazo hili la kufanyika hafla hii yenye lengo la kuchangisha fedha ambazo zitamsaidia mtoto wa kike wa Kizanzibar kuweza kutumia fursa za masomo zilizopo na zinazoendelea kutolewa na Serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

Pamoja na hayo, natoa pongezi kwa Mwenyekiti wa FAWE Zanzibar pamoja na Wana-FAWE wote kwa kazi nzuri ya kutayarishia hafla hii, na pia kuendesha harakati za kupigania vijana wetu ambao ndio nguvu-kazi yaTaifa letu.

 

Nasaha zangu kwa Watoto wa kike kupambana na kuzitumia fursa zinazoandaliwa na FAWE Zanzibar na taasisi nyengine zenye malengo kama hayo, kwa makusudi ya kujenga kesho yenu; kwani kwa sasa dunia ina changamoto nyingi zinazokinzana na makuzi ya mtoto ikiwemo umasikini, urasimu, uonevu, udhalilishaji na mengi mengineyo.

 

Mwisho, Sio kwa umuhimu ninawashukuru wadhamini wetu wote waliojitoa kwa hali na mali kufanikisha shughuli hii. Waswahili husema Kutoa ni Moyo na sio Utajiri.  Hivyo basi, nimefurahishwa sana na ushiriki mkubwa wa wachangiaji katika shughuli hii. Ninatarajia na nawaomba kwa heshima zote tuchangie kwa moyo mmoja kusaidia kufanikisha kukamilika yale waliyopanga kama ilivyobanishwa na mratibu wa FAWE. Nina kila sababu ya kushukuru kwa ushirikiano wenu na kusema kuwa “ili tuwe na    Maendeleo endelevu, muwezeshe Mwanamke”.

 

Nakutakieni kila la kheri waalikwa wote na wenyeji FAWE Zanzibar na kumuomba Allah aturudishe majumbani salama.

 

Mungu ibariki Tanzania,

Mungu ibariki Zanzibar,

Mungu ibariki FAWE Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.