Habari za Punde

Waandishi Watakiwa Kutumia Kalamu Zao Ili Kwenda Sambamba na Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane.-Dk.Mwinyi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua Kongamano la Waandishi wa Habari Zanzibar Kujadili Matumizi ya Sekta ya Mawasiliano ya Habari katika Kuijenga Zanzibar Mpya. lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza waandishi wa habari kote nchini, kuzitumia vyema kalamu zao ili kwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya nane ya kuimarisha amani, umoja na maridhiano ya Wazanzibari.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa Kongamano la kujadili matumizi ya Sekta ya Mawasiliano ya Habari katika kuijenga Zanzibar mpya, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul wakil uliopo  Kikwajuni jijini hapa.

Amesema matumizi sahihi ya kalamu yatakayokwenda sambamba na dhamira ya serikali ya Awamu ya nane katika kuimarisha amani, umoja na maridhiano ya Wazanzibar ndio njia sahihi itakayofanikisha katika kupiga hatua za haraka za maendeleo.

Aliwataka waandihi wa habari kuwahimiza wananchi kushirikiana na Serikali kwa kufanya kazi kwa bidiii na kupiga vita rushwa, ufisadi, udhalilishaji wa watoto na wanawake pamoja na uvunjifu wa sheria, huku akisisitizza umuhimu wa wafanyabiashara kulipa kodi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwataka waandishi na wadau wa habatri kutumia vyema fursa ya kufanyika kongamano hilo kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusiana na sheria ya habari ili kupata sheria itakayoweza kuimarisha zaidi sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Zanzibar.

Alieleza kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake amebaini  wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingi, ila kwa bahati mbaya wamekosa sehemu za kuziwasilisha na kupata ufumbuzi wake.

Alisema uamuzi wa serikali wa kuzindua mfumo wa mawasiliano baina ya wananchi na Serikali unalenga kufahamu changamoto hizo, hivyo akawataka waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi faida ya njia hiyo ya haraka katika kufikisha kero zao serikalini.

Alisema anaridhishwa sana na mashrikiano anayopata tangu Serikali ya Awamu ya nane iingie madarakani kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi, watangazaji pamoja na wafanyakazi wote wa tasnia hiyo.

Aidha, alivishukuru vyombo mbli mbali vya habari kwa namna vilivyotoa ushirikiano mkubwa katika kipindi cha kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa mipango na ahadi za Serikali katika siku 100 tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya nane.

“Nakupongezeni  kwa kazi nzuri mlioifanya ya kuwaarifu wananchi hatua mbali mbali za tuikio la msiba wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliekuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar pamoja na wiki ya maombolezo yake”, alisema.

Kuhusiana na vitengo vya Mawasiliano na habari vilviyoko katika Wizara na taasisi za Serikali, Dk. Mwinyi aliwaagiza wakuu wa taasisi hizo kukutana na na Maofisa habari waliopo katika taasisi zao na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kufanikisha utoaji wa habari za maendeleo katika taasisi hizo, sambamba na kutatua changamoto ziliopo.

Rais Dk. Mwinyi aliwakumbusha waandishi wa habari kuendelea kufanyakazi zao kwa weledi na ubunifu wenye kuzingatia maadili ya kazi hiyo.

“Uandishi wa habari ni taaluma muhimu inayosomewa na yenye maadili yake, si kazi ya kufanywa na mtu yeyote anaejisikia awe mwandishi, ni vyema taasisi zenu zikawa na uwezo wa kuwadhibiti watu wachache wanaoichafua tasnia ya habari kwa kauandika taarifa za uongo au kukiuka maadili”, alisema.

Alisema kuna umuhimu wa kuyadhibiti masuala yanayotokana na watu wanaopotosha habari, kwani baadhi ya mambo husababisha usumbufu na taharuki kwa wananchi.

Katika hatua nyengine, Dk. Mmwinyi aliwataka waandishi wa habari kujiongeza na kujiendeleza kitaaluma na kuacha kufanya kazi kwa mazowea, ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano duniani.

Alisema waandishi wa habari wa kisasa wanapaswa kuwa na uwezo na weledi wa kuandika makala na habari mbali mbali juu ya masuala  muhimu ya kitaalamu na kiufundi.

Aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa Serikali itahakikisha inaandaa mazingira ya kuviwezesha vyombo vya habari ili kwenda na kasi iliopo, pamoja na kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo za kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo, kusimamia stahili zao pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.

Mapema Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid alisema Wizara hiyo imeanza kuchukua hatua za kuimarisha tasnia ya habari kwa kuliboresha Shirika la Utangazaji  la ZBC pamoja na kusimamia sekta hiyo kwa kuzingatia sheria na maadili ya fani hiyo.

Aliwataka waandishi kufahamu kuwepo kwa vyombo maalum vinavyowasimamia ili kuhakikisha wanafanyakazi zao kwa uadilifu, na kusema yeyote atakaekwenda kinyume atachukuliwa hutua, huku akiwataka kuondokana na taarifa za kibaguzi au kuleta vurugu katika jamii.

Alisema Wizara hiyo itaendeleza mchakato wa kukutana an wadau wa habari katika vyombo vya Serikali pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha sheria ya habari itakayopatikana inakuwa bora.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati iliyoratibu Kongamano hilo Farouk Karim, alimuomba Dk. Mwinyi kuangalia uwezekano wa taarifa mbali mbali zinazotoka Ofisi yake, ikiwemo taaarifa za uteuzi kutoka mapema ii vyombo mbali mbali hususan magazeti viweze kunufaika kwa kwenda sambamba na muda.

Katika Kongamano hilo mada mbili zimewasilishwa, ikiwemo ile ya “Mapendekezo ya wadau wa Habari dhidi ya Mswada wa Habari” iliyowasilishwa na Mwandishi mwandamizi Suleiman Seif pamoja na “Matumizi ya mawasiliano ya habari katika kujenga Zanzibar mpya” iliyowasilishwa na Mwandishi mwandamizi Dk. Saleh yussuf Mnemo.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki katika kongamano hilo, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Juma Abdalla Sadalla, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi mbali mbali wa Vyama vya Siasa.       

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.