Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa juu wa Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} Afisini kwake Vuga.

Na.Abdurahim Khamis

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imedhamiria kuzitatua changamoto zote zinazowakabili wananchi katika kila nyanja, ili lile lengo lililokusudiwa na Serikali ya Awamu ya nane liweze kufikiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla,  ameyasema hayo alipokutana na uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Ofisini kwake Vuga,  kwa ajili ya kujadiliana kuhusu namna bora zitakazoweza kutatuta kero za wananchi katika tatizo la huduma ya maji, na kuondosha kabisa changamoto hiyo kwa wananchi.

Mheshimwa Hemed alieleza kwamba anatambua changamoto  za kiutendaji katika Idara mbali mbali, kama rasilimali fedha , na watendaji, jambo ambalo linaweza kusababisha kuzorota kwa  huduma bora kwa wananchi.

Alibainisha wazi kwamba lengo la kukutana na Watendaji wa Taasisi za Serikali ni kuweza kujadiliana kwa pamoja, kwa mantiki ya kupata mawazo ya jumla yatakayosaidia kupata nguvu kubwa zitakazorahisisha nguvu za kuwatumikia wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka viongozi hao, kuwa tayari kwa umoja wao kuhakikisha wazanzibar wanapata huduma bora ya maji safi na salama, bila ya usumbufu wowote.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameamuwa kukutana  na viongozi wa taasisi mbali mbali za Serikali,  baada ya ziara yake ya kutembelea Wilaya zote 11 za Zanzibar, ili kuona changamoto zinazowakabili wananchi wa Zanzibar.

Vikao hivyo vimelenga  kutafuta mbinu na njia  kuona jinsi gani Viongozi na Watendajio wa Taasisi hizo wataweza kuzitatua changamoto zilizojichomoza kwenye ziara hizo za Kikazi.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikutana na Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Mheshimiwa Hemed alisema Benki ya Watu wa Zanzibar inawajibu wa kwenda na wakati katika harakati zake za Kibiashara ndani ya mfumo wa ushindani ya Kibenki uliopo Kitaifa na Kimataifa.

Aliukumbusha Uongozi na Watendaji wa Benki hiyo Kongwe Nchini Tanzania kutumia uzoefu iliyonao wa Kibenki kuendelea kutoa huduma bora zitakazokidhi mahitaji ya Wateja wake.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Nd. Muhsin Salim Msoud alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo tayari umeshaandaa Mpango Maalum utakaotoa muelekeo sahihi wa jinsi Benki hiyo itakavyofanikisha malengo yake.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.