Habari za Punde

OSHA Yaaswa Kuendelea Kuzingatia Utoaji wa Huduma Bora kwa Wateja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakati wa kikao cha Nne cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo iliofanyika Jijini Dodoma.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda akieleza kuhusu shughuli za utekelezaji za ofisi yake wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo iliofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakiwa katika kikao cha Baraza la ofisi hiyo.

Baadhi ya Watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa kiako hicho.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)




NA. MWANDISHI WETU.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe Jenista Mhagama amewaasa watumishi wa  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kuhudumia wateja wao kwa kuzingatia misingi ya huduma kwa wajeta ili kuboresha utendaji wao wa kila siku.

Ametoa kauli hiyo mapema hii leo wakati akifungua kikao cha baraza la Nne la Wafanyakazi la ofisi hiyo, tarehe 17 Aprili, 2021 Jijini Doodma.

Waziri Mhagama aliwaasa watendaji wa ofisi hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa wateja kwa kuzingatia uhuhimu na unyeti wa ofisi yao.

“Ni muhimu kuhudumia wateja mnaokutana nao kwa kuzingatia Customer care, na kuzingatia Lugha nzuri katika kutoa huduma kwani ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma kwa wateja wenu”alisema waziri.

 

Waziri alieleza umuhimu wa taasisi hiyo kwa kuzingatia kuwa, ni moja ya Taasisi ambayo ni kiungo kati ya Serikali na Wananchi kwa kuwa wanakutana na wananchi wengi pamoja na wageni kutoka nje ambao ni wawekezaji.

 

“Hakikisheni mnatumia lugha nzuri na zenye staha kwa kuwasikiliza na kuwahudumia vizuri wateja wenu, tunaamini kuwa nyie ni miongoni mwa lango kuu la kuingiza Wawekezaji nchini na kukuza Uchumi kupitia sekta ya Viwanda, madini na kilimo hivyo mienendo yenu ndio picha ya aina ya Uchumi tunaoutegemea,”.alisisitiza

 

Sambamba na hilo waziri aliwapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa kuendelea kutimiza majukumu yao yanayozaa matunda na kuwahakikishia kuwa Serikali inatambua na kujali mchango wao.

“Napenda niwapongeze Watumishi wote wa OSHA kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na naomba kuwahakikishia kuwa Serikali inatambua juhudi mnazozifanya za kuhakikisha kuwa Wafanyakazi katika sekta zote wanakua salama katika maeneo yao ya kazi na kuleta tija kwa Waajiri na Serikali kwa ujumla,”Alisisitiza Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa, OSHA imeendelea kutoa matokeo chanya kwa kuzingatia kazi nzuri inayofanywa na ofisi hiyo katika kupunguza malalamiko, ajali, vifo na magonjwa yatokanayo na kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ofisi hiyo, Bi. Khadija Mwenda alimshukuru waziri kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za taasisi hiyo huku akiahidi kuendelea kutekeleza maelekezo, maagizo na wajibu wao ili kuendelea kuwa na ufanisi katika ofisi yake.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wafanyakazi Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa ofisi hiyo Bi. Joyce Mwambungu alieleza wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taaratibu za utumishi wa Umma bila kuvunja sheria hilizopo na kumpongeza waziri kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.