Habari za Punde

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Alihutubia Bunge Jijini Dodoma.


 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelihutubia Bunge na kutumia hotuba yake ya Bunge kutuma kile alichokiita ni onyo kwa  watu wanaofanya ubadhirifu wa mali za umma  na kufanya uchonganishi kupitia mitandao ya kijamii.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa na mkewe Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wengine wa Serikali, dini, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mabalozi wa nchi mbali mbali waliopo Tanzania, pamoja na viongozi wakuu wastaafu na wake wa viongozi wakuu.

Alisema kwamba mara baada ya kifo cha Rais Magufuli tayari kuna viongozi wa umma na mashirika ambayo yameanza kulega lega.

“Niwaonye wale wote wanaosimamia mali za umma ukwepaji wa kodi, ubadhirifu, kukemea uzembe na wizi kuwa yameodokakutokana na kuondoka kwa Hayati Magufuli , Hayati mpendwa wetu amekwenda  peke yake lakini maoni na mikakati aliotuachia tunayafanyia kazi”.

Rais Samia pia, amekemea vikali taarifa za uchonganishi ambao alisema unafanyika mitandaoni juu ya kifo cha Hayati Magufuli na kusema kwamba kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa kinyume cha ripoti ya madaktari basi azipeleke kwenye mamlaka husika na si kuchochea uhasama mitandaoni.

“Taarifa tuliyopewa juu ya kifo cha mpendwa wetu ni udhaifu wa moyo ambao ameishi naokwa zaidi ya miaka kumi , kuna watu huko mitandaoni wanasema fulani na fulani wamempa sumu, kama wanataarifa za maana waje tuwasikilize na taarifa zao”alisema Samia.

Aidha, Rais Samia aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi kwa kuonesha ushirikiano mkubwa kwake katika kipindi chote cha uongozi wake hasa katika kipindi cha msiba wa Rais Magufuli.

Alieleza azma ya Serikali yake anayoiongoza ya kuimarisha sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji, madini, biashara na nyenginezo huku akieleza azma ya serikali yake ya kununua meli nane za uvuvi kwa kushirikiana na shirika la IFAD ambazo zitagawiwa nne kwa Zanzibar na nne kwa Tanzania Bara.

Alitumia fursa hiyo  kuwaambia Wabunge kwamba wana haki ya kuikosoa Serikali na hata ikibidi wafanye hivyo kwa ukali ilimradi watumie lugha za Bunge.

Rais Samia ameliambia Bunge kwamba amepanga kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili kwa pamoja waweke msimamo wa kuendesha shughuli za kisiasa.

Kiongozi huyo amesema hivyo wakati akitaja jinsi alivyopanga  kuimarisha mazingira ya uhuru na demokrasia nchini Tnaznaia.

“Nakusudia kukutana na viongozi wa kisiasa wa Tanzania ili kwa pamoja tuweke msimamao wa kuendesha shughuli  za kisiasa”.

Aidha, alisema kuwa Serikali yake itaendela kulilea Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) kimkakati ikiwemokulitua mzigo wa madeni kwani shirika hilo limerithi madeni na hivyo kwa sasa linaonekana kuwa halina thamani na limekuwa likitengeneza hasara.

“Hatutakubali liendelee kutengeneza hasara baada ya uwekezaji mkubwa uliofanyika ....tutaenda kulifanyia uchambuzi yakinifuna tutaweka watu ambao wataliongoza ili kutengeneza faida”, alisema Rais Samia.

 

Alisema kwamba Seikali inatambua kwamba biashara ya ndege ni ngumu na ina hitaji kuepuka yote ambayo hayana tija kwa Shirika.

Aliongeza kuwa Serikali yake itafanya mabadiliko ya kisera na sheria ili kuwavutia wawekezaji zaidi nchini kwani kumekuwa na malalamiko juu ya urasimu, na kutokutabirika kwa sera za uwekezaji, hivyo, eneo hilo litaekewa kipaumbele ili kutoa tija kwa uchumi wa Taifa.

Alieleza kwamba athari za mripuko wa virusi vya Corona umefanya  ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuanguka kutoka wastani wa asilimia 6.9 mwaka jana mpaka kufikia 4.7 mwaka huu.

“Ningependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wanalipa kodi bila shuruti wala matumizi ya nguvu”,alisisitiza Rais Samia.

Alisema kuwa lengo kuu la serikali yake ni kuendeleza na kuimarisha mambo yote mazuri yaliyofanyika na watangulizi wake huku akisisitiza kwamba Serikali yake itayaendeleza makamo makuu ya Serikali yaliopo Dodoma.

Aliahidi kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kuteua wanawake wengi zaidi katika nafasi mbali mbali za uongozi kuendana na  sifa na uwezo wa mtu.

Alisisitiza kwamba akina mama lishe wataangaliwa zaidi huku sekta za sanaa na utamaduni kuimarishwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa hati miliki sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya timu za taifa zikiwemo za wanawake.

Pia, ameliambia Bunge kwamba mabadiliko yatafanyika katika baadhi ya maeneo ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji.”Ndio maana kaulimbiu yetu ya hapa kazi tu inaendelea”,alisisitiza.

Rais Samia alieleza uzoefu alionao katika kazi na kueleza kwamba  amekulia  katika jamii sahihi na ana uzoefu wa kutosha katika shuguuli za Serikali na za Kichama.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.