Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Hussein Ali Mwinyi Ajumuika Katika Futari Maalum Aliyowaandalia Viongozi na Wananchi wa Dodoma Katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Dodoma.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Viongozi na Wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika futari Maalum aliyowaandalia katika viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma na (kushoto kwa Rais) Rais Mstaaf wa Zanzibar Awamu ya Saba Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi,  amejumuika na mamia ya Wananchi na Viongozi katika Iftari aliyoiandaa kwa ajili yao na kufanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Conversion centre, Jijini Dodoma,

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) walihudhuria, akiwemo Rais mstaafu wa awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Mama Mariam Mwinyi na Mama Mwanamwema Shein .

Wengine ni pamoja na Makamo wa Pili Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Serikali za SMZ na SMT, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said,  Wabunge, Wawakilishi, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pamoja na wageni mbali mbali.

Akitoa shukran kwa waalikwa, Dk. Mwinyi amesema amefarikijika sana na muitikio wa waumini hao, mbali na mialiko kutolewa katika kipindi kifupi.

Amesema ameamua kuandaa futari hiyo Jijini Dodoma kwa kuzingatia  uwepo wa vikao vya Bunge na vikao vya Chama cha Mapinduzi wakati huu, akibainisha kuwa ni wakati muafaka wa kukutana na kufutari pamoja na waumini hao.

Aidha, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha waumini hao kutekeleza vyema ibada hiyo muhimu ya funga, na kusema kukutana kwao huko ni jambo la kheri.

Nae, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Mustafa Rajab Shaaban amemuombea dua Rais Dk. Mwinyi pamoja na kumtakia kheri nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa maandalizi mazuri ya iftari hiyo.

Alitumia fursa hiyo kumtakia rehma yeye na familia yake , akibainisha wema mkubwa aliowafanyia waumini waliotikia mwaliko wake.

Akinukuu hadithi ya Mtume Muhamad (SAW), Sheikh Rajab amesema Mtume ameelekeza kuwalipa wema watu  wanaofanyia wenzao mambo wema na pale wasipokuwa na cha kuwalipa, basi ni vyema wakawaombea dua, hivyo dua hiyo ni jambo lililosadifu.

Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, yuko Jijini Dodoma kwa vikao mbali mbali vya Chama cha Mapinduzi, ambapo kesho April 30, 2021, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho watapiga kura ya kumthibitisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho kufuatia kifo cha Mwenyekiti wake, Rais  Dk. John Pombe Magufuli.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.