Habari za Punde

Wazee na Walimu wa Madrasa Nchini, kuwaendeleza kielimu katika fani mbali mbali za dini na dunia, Wanafunzi waliohifadhi Qurani,

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kumalizika kwa Mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika Jaamiu Zinjibaar Mazizini.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, amewataka Wazee na Walimu wa Madrasa Nchini, kuwaendeleza kielimu katika fani mbali mbali za dini na dunia, Wanafunzi waliohifadhi Qurani, ili kupata radhi zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika hafla ya Mashindano Makuu ya kuhifadhi Quran ya Kitaifa Zanzibar ya juzuu 30 yaliyohitimishwa katika Masjid Jaamiu Zinjibaar, Mazizini Zanzibar.

Amesema kuwa wanafunzi waliopata fursa ya kuhifadhi Quran ni vyema kuandaliwa mazingira mazuri ya kielimu, ili wasiishie kushiriki mashindanoni na kupata zawadi, bali waandaliwe mfumo mzuri wa kuendelea na masomo akitolea mfano kujua tafsiri ya kile walichokihifadhi.

Ameipongeza jumuiya ya kuhifadhisha quran Zanzibar, kwa juhudi wanazochukua za kuwahifadhisha wanafunzi kitabu hicho kitukufu , hadi kuandaa Mashindano makubwa kila mwaka, na kusema juhudi hizo zimefikiwa kutokana na uongozi mzuri waliyonao ndani ya jumuiya hiyo.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza Jumuiya hiyo kwa hatua nzuri iliyofikia, na kutia moyo kwa kuona kuwa hadi sasa Jumuiya hiyo imeshahifadhisha Zaidi ya wanafunzi 300 juzuu 30, wa jinsia zote na kusema kuwa huo ni mfano tosha kupata jamii iliyoshikamana na kitabu cha Allah.

“ Jumuiya imefanya kazi kubwa na ya kujitolea tokea ilipoasisiwa kwake kitendo kinachoipa Serikali kuangalia namna ya kuunga mkono jitihada hizo”. Alisisitiza Mhe. Hemed Suleiman.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuahidi Uongozi wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran Zanzibar kwamba Serikali iko tayari kuwashawishi Waumini wenye Uwezo kutafuta njia ya kutanzua baadhi ya changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo likiwemo suala zima la Jengo la Afisi yao.

Akigusia suala la umuhimu wa kitabu cha Quran Mhe.Hemed amesema ipo haja ya kuendelea kuisoma zaidi Quran hasa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, ili kupata ujira mkubwa, akitolea mfano kuwa, mwenye kusoma quran, aajihakikishia uombezi siku ya kiama.

Amewausia  Wana Jumuiya na Walimu wa Vyuo vya Quran kwamba wasikate tamaa na mazingira magumu wanayofanyia Kazi kwani jukumu wanalolisimamia lina ujira mkubwa kwa Muumba wao ambaye hashindwi kuwashushia Rehema zake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi Wananchi na Waumini wenye uwezo kujitokeza katika kufanikisha mambo yenye kheir ikiwemo haya ya kusaidia nguvu za uhifadhi ya Quran kwa Vijana wao ambayo husaidia kupeleka mbele Uislamu.

Aliishauri Taasisi hiyo ijisogeze zaidi katika kuona malengo yake yanafikiwa na amekubali kuwa Mlezi wa Jumuiya hiyo katika azma ya kuona Maadili ya Kizazi cha sasa kupitia Kitabu Kitakatibu cha Quran yanaendelea kukua na kuimarika kila Mwaka.

Mapema akitoa Taarifa ya Jumuiya ya kuhifadhi Quran Zanzibar Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya Kiislamu Mwanazuoni Sheikh Suleiman Omar {Maalim Sule} alisema Jumuiya hiyo iliyoasisiwa Mnamo Mwaka 1992 hivi sasa imeshatimiza miaka 28.

Maalim Suleiman alisema lengo la Jumuiya hiyo ni kusimamia ujenzi wa Maadili mema katika Kizazi cha Kiislamu katika kujikita zaidi kwenye Uhifadhi ya Kitabu Kitakatifu cha Quran ambapo kwa sasa zaidi ya Wanafunzi 300 wameshafanikiwa kukihifadhi moyoni Kitabu hicho.

Alifahamisha kwamba Jumuiya ya kuhifadhi Quran katika malengo yake ya muda mrefu inaendelea na taratibu za kuitangaza Zanzibar Kimataifa jinsi ya kusimamia na kuendeleza Quran ili kuwa mwanga katika ardhi hii ya Mwenyezi Muungu.

Akitoa salamu Mmoja wa Waumini wanaoiunga mkono Jumuiya hiyo kwa kiwango kikubwa Mfanyabiashara Maarufu Nchini Sheikh Said Nasser Bopar alisema Waumini lazima washindane kwa nguvu na mali zao katika kuisimamia njia sahihi ya mwenyezi Mungu.

Sheikh Said Bopar aliwahakikishia Wanajumiya hiyo kwamba yeye kama mdau mkubwa wa Taasisi hiyo ya Kidini ataendelea kuiunga mkono Jumuiya hiyo ili ifanikiwe katika kufikia malengo yake.

Mashindano hayo Makuu ya kuhifadhi Quran ya Kitaifa huandaliwa na Jumuiya ya kuhifadhisha Quran Zanzibar kila Mwaka na kushirikisha Wanafunzi kutoka Mataifa ya Afrika Mashariki.

Lakini Mwaka huu Mashindano hayo yamejumuisha Wanafunzi  wa Zanzibar pekee kwa kuhifadhi Juzuu 30 yaliyoanzia mapema Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.

Matokeo ya Mashindano hayo ya kuhifadhi Quran yamemuwezesha Mwanafunzi Fahad Haji kushika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 99 akizawadiwa shilingi Milioni 5,000,000/- na zawadi maalum.

Mshindi wa Pili alikuwa Mwanafunzi Abdulnassir Mohamed Kombo aliyepata alama 98 akikabidhiwa shilingi Milioni 4,000,000/- taslim wakati mshindi wa Tatu Shamis Maalim aliyepata alama 98 na kuzawadiwa shilingi Milioni 3,000,000/-.

Mshindi wa Nne Mussa Hamad akifuatiwa na washindi wenzake hadi 16 wamezawadiwa shilingi Laki 800,000/- kila Mmoja na zawadi maalum.

Kwa upande wa Tashjii Tahqiq Mshindi wa kwanza alikuwa Mwanafunzi Rashid Hemed aliyeibuka na alama 100 na kuzawadiwa shilingi Milioni 2,500,000/- , Mshindi wa Pili Hamad Omar aliyezawadiwa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa kupata alama 98 na mshindi wa Tatu Mbarouk Mussa aliyepata alama 95.6 na kukabidhiwa shilingi Milioni 1,500,000/-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla Kati Kati, Kulia yake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran Zanzibar Maalim Suleiman Omar na Kushoto yake naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi wakifuatilia mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika Jaamiu Zinjibaar Mazizini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akimkabidhi Shilingi Milioni 5,000,000/- na zawadi Maalum Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya Kuhifadhi Quran Kitaifa Mwanafunzi Fahad Haji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya Kiuhifadhi Quran Zanzibar, kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na Ofisi ya Kadhi Mkuu wa Zanzibar mara baada ya kukamilika kwa Mashindano ya Kuhifadhi Quran.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.