Habari za Punde

SMZ Itawawezesha Mahujaji Wake Wote Kupata Chanjo ya Maradhi ya Covid 19.Ili Kwenda Kutekeleza Ibada ya Hijja Nchini Saud Arabia.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akitoa nasaha zake mara baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa ilioswaliwa leo katika Masjid Omar Bin Khatwaab Msumbiji Kwamabata  Jijini Zanzibar  ikiwa ni kawaida yake ya kujumuka na waumini Dini ya Kiislamu katika misikiti mbali mbali Nchini.

WAUMINI wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa nasaha zake mara baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa ilioswaliwa leo katika Masjid Omar Bin Khatwaab Msumbiji Kwamabata  Jijini Zanzibar  ikiwa ni kawaida yake ya kujumuka na waumini Dini ya Kiislamu wa miskiti mbali mbali Nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa  RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyiameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itawawezesha Mahujaji wake wote kupata chanjo ya maradhi ya COVID 19 ili kuweza kwenda kutekeleza  ibada ya Hijja nchini Saud Arabia mwaka huu.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Omar bin Khatab, Msumbiji kwa Mabata, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akitoa salamu zake hizo kwa waumini hao na wananchi kwa jumla, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba mwaka jana waumini hawakuweza kwenda kutekeleza ibada hiyo tukufu kutokana na kuwepo kwa maradhi hayo duniani lakini mwaka huu upo mwelekeo kwamba ibada ya hija inaweza kuruhusiwa lakini kwa masharti.

Hivyo, alieleza kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshajipanga kuwapatia Mahujaji wake wote chanjo hiyo itapatikana na kwa wale wote walioweka nia waendelee na maandalizi ya kwenda kufanya ibada ya Hijja mwaka huu.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mwelekeo kwamba chanjo hiyo itapatikana kwa uhakika na haitokuwa na kikwazo cha aina yoyote na wale wote wanaopaswa kupata huduma hiyo kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada hiyo tukufu watapatiwa.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuendeleza umoja na mshikamano na kueleza kwamba dini ya Kiislamu inawataka na kuwafunza waumini wake wote kuwa wamoja.

Alisema kwamba mifano mingi imetolewa katika hadithi za Mtume Mohamad (S.A.W), juu ya suala zima la umoja na kueleza kwamba kwa upande wa Zanzibar amani, utulivu na umoja vyote hivyo vipo na lililobaki hivi sasa ni kujitafutia maendeleo.

Aliongeza kwamba lililobaki hivi sasa ni kuhakikisha kila mtu anafanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo yanayohitajika huku akiahidi kwa upande wake kufanya yale yote aliyoyaahidi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kuomba ushirikiano ili kuleta maendeleo nchini.

Alisema kwamba pale panapokemewa watu hufanya hivyo kwa nia njema kabisa na hatafutwi mtu wa kulaumiwa bila sababu na hufanywa hivyo ili wanaofaidika wawe wengi na sio wachache.

Sambamba na hayo, Alhaj Rais Dk. Mwinyi alilipokea ombi la msiikiti huo la kuwapatia zulia jipya na kusema kuwa ombi hilo atalifanyia kazi kwa haraka na kuwaahidi kuwafanyia mengine zaidi kwani milango yake iko wazi.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Othman Othman Hussein aliyaeleza mafunzo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja.

Katika hotuba yake hiyo Sheikh Othaman alisisitiza haja ya kuimarisha na kuendeleza umoja miongoni mwa waislamu kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na neema kubwa katika wanaadamu ni kuwa wamoja.

Aidha, Sheikh Othman aliueleza kwamba msingi mwengine unaoimarisha umoja ni kuwa na subira jambo ambalo waumini walijifunza sana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh Othman alisisitiza subira na kutoa mifano ya aya za Qur-an tukufu pamoja na hadithi za Mtume Muhamad (S.A.W) zinazosisitiza suala zima la subira.

Nao waumini wa msikiti huo walieleza jinsi walivyofarajika kwa kusali pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi katika sala hiyo ya Ijumaa katika msikiti wao huo.

Pamoja na hayo, waumini hao walimueleza Alhaj Dk. Mwinyi ombi lao la kutaka kupatiwa zulia jipya la msikiti wao ili kuweza kufanya ipada zao ipasavyo, ombi ambalo Alhaj Dk. Mwinyi alilipokea na kulikubali mikono miwili.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.