Habari za Punde

Wanachama na Uongozi Umuhimu wa Kujenga Umoja na Kuondoa Ugomvi na Pamoja na Makundi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCMTaifa Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi na Mabalozi wa CCM wa Mkoa wa Magharibi Kichama, akiwa katika ziara yake ya kutowa shukrani kwa Wananchi, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Afisi ya CCM Mkoa Amaan Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu wa Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujenga Umoja na kuondokana na ugomvi pamoja na makundi.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika mkutano maalum wa shukrani kwa Viongozi wa ngazi mbali mbali za CCM na Jumuiya zake, uliofanyika katika Ukumbi  wa CCM Mkoa, uliopo Amani Jijini Zanzibar.

Amesema katika hali ilivyo hivi sasa ambapo baadhi ya Viongozi wa Majimbo (Wabunge na Wawakilishi)  wamegawika makundi, ni dhahri kuwa maendeleo yataweza kuchelewa.

Ametaka migogoro ndani ya chama hicho kusitishwa na kubainisha wajibu wa Viongozi na wanachama kushikamana ili kuijenga nchi.

Aidha, alisema uchaguzi wa chama hicho unatarajia kufanyika mwaka ujao wa 2022, hivyo akasisitiza na kuwataka wanachama kufuata misingi na taratibu za Chama katika kufanya kampeni, kuambatana na wakati uliopangwa pamoja na kusitiza haja ya kuondokana na fitna na majungu ambayo hatma yake ni kuleta mifarakano.

Rais Dk. Mwinyi aliwakumbusha  Mawaziri,  Wakuu wa Mikoa pmoja na  Wakuu wa Wilaya kutatua matatizo yanayowakabili wananchi katika maeneo yao badala ya kusubiri wananchi kuelekeza matatizo hayo kwa Rais, akibainisha haja ya kutekeleza ipasavyo wajibu wao.

Mapema, akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustapa, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa utekelezaji mwema wa majukumu yake na kusema hatua yake ya kumuamuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutoa taarifa ya hesabu za Serikali hadharani inathibitisha kwa kiasi gani alivyodhamiria kuwatumikia wananchi.

Nae, Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Kichama, Mgeni Mussa Haji  akitia taarifa ya kazi za Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake, alisema hali ay upinzani katika Mkoa huo iko chini, kwa kuzingatia Majimbo na wadi zote ziliomo katika Mkoa huo ziko chini ya hatamu ya CCM.

Alisema kuna mashirikiano ya karibu katika utendaji kazi kati ya Chama hicho na Serikali.

Aidha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Magharibi Mohamed Rajab Soud alisema jengo la Ofisi ya Chama hicho Mkoa, hailingani na hadhi ya chama hicho , hivyo Uongozi wa Mkoa huo umeazimia kupata eneo ili kujenga jengo jipya litakalokipa heshima chama.

Nao, baadhi ya Viongozi waliopata fursa hiyo, walieleza changamoto mbali mbali ziliomo katika Majimbo yao, ikiwemo ukosefu wa huduma za maji safi na salama, hususan katika majimbo ya Mwanakwereke, Mtoni pamoja na Welezo na kuilalamikia mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika upatikanaji wa huduma hiyo.

Aidha, walisema baadhi ya Majengo ya Chama katika Mkoa huo hayako katika hali nzuri, sambamba na kutokuwa na Hati miliki, hivyo wakauomba Uongozi wa CCM Taifa kufuatilia suala hilo, kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi.                        

Vile vile, waliomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuipanua Barabara ya Kinazini – Bububu ambayo walisema ni nyembamba na imekuwa chanzo cha kutokea kwa ajali.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.