Habari za Punde

Mbunge wa viti maalum Bi Asha Abdallah awafuta machozi wanawake

 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Asha Abdallah Juma, amewasihi Wananchi waliopata majanga ya kuungua moto nyumba zao kuendelea kuwa wavumilivu wakati Serikali na wadau wengine wakiendelea kutoa michango ya ya kuwasaidia.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT) Ghanima Sheha Mbwara wakati akikabidhi msaada wa Chakula kwa niaba ya Mbunge huyo na kuwaomba wawe wavumilivu ili wavuke salama katika kipindi kigumu cha majanga hayo.

Ghanima, akizungumza na wananchi hao huko katika Ukumbi wa makaazi ya kuhifadhi Wazee Sebleni, alisema msaada huo wa chakula umetolewa kwa lengo kuwasaidia familia zao kujikimu kimaisha.

"Ni kawaida UWT kujitoa katika kuwasaidia wanawake wenzao hasa katika wakati wanapopata maafa ya aina hii na maafa mengineo hivyo Mbunge huyu akiwa amechaguliwa na wanawake wenzake tena katika mkoa huu ameoguswa kwa kuwasaidia,"alisema

Alisema siku zote wanawake wanakuwa watu wa kuungana katika kusaidiana na kwamba hiyo ndio tabia yao hivyo kitendo cha Mbunge huyo wa viti maalamu kuwasaidia ni dhahiri imeonyesha dhana hiyo ya wanawake kuungana na kusaidiana wakati wa shida.

Kwa upande wao Wanawake hao waliopata majanga ya kuungua moto nyumba zao zilizopo Mji Mkongwe wamemshukuru Mbunge huiyo kwa msaada wa vyakula aliyowapatia kwa ajili ya kujikimu na familia zao.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Dorisi Rashid ambaye ni mmoja waliopata maafa hayo alisema  vyakula hivyo vitawasaidia kwa namna moja ama nyingine kutokana na kuwa mara nyingi majanga ya aina yoyote wanaoathirika zaidi ni  wanawake kwani wao ndio walezi wa familia zao.

"Sisi wanawake ndio tunakuwaga waathirika sana kwani sisi ndio walezi wa familia hizi baba anaweza kukimbia zake lakini mwanamke huwezi ukiangalia watoto kulea ni jukumu letu kuhakikisha watoto wanakula na wanakwenda shule hivyo msaada huu utatusaidia sana sitopata tabu kufikiria kupata mchele,sukari,mafuta ama maharage,"alisema  

Dorisi alisema mpaka sasa ni miezi miwili tangu kutokea kwa ajali hiyo ya moto ambapo miongoni mwa familia nane zimeathirika na ajali hiyo na wamepewa makazi ya kujihifadhi katika nyumba za kuwahifadhia wazee eneo la Sebuleni hivyo bado wanahitaji msaada zaidi.

Naye Maimuna Hassan Ame alisema anashukuru kwa kupata msaada huo wa vyakula ikiwemo mchele,mafuta,unga,sukari na maharage na kwamba ameonyesha dhamira yake ya kiungwana kama mwanamke mwenzao katika kuwasaidia wanawake wenzao.

"Tunashukuru kwa kupata msaada huu wa vyakula kwani mpaka sasa ni muda mrefu takribani miezi miwili tangia ajali hii ya kuunguliwa na nyumba zao itokee tunawaomba wanawake wenzetu nao wajitokeze watusaidie kama vyakula na ikiwezekana hata fedha za kujikimu kwani watoto zetu wanakwenda shule wanahitaji nauli na mambo mengine,"alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.