Habari za Punde

Mhe Hemed mgeni rasmi katika uzinduzi wa Vipindi vya kumbukumbu ya mambo ya kale vilivyopewa jina “SOGEA NIKUJUZE”

Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Mhe. Leila Mohamed Mussa akiwapongeza Vijana wa Kampuni ya Mavips Pictures katika hafla ya Uzinduzi wa Vipindi vya kumbukumbu ya mambo ya kale ambapo Makamu wa Pili Rais wa Zanzibar alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akihutubia hadhira iliofika katika hafla ya Uzinduzi wa Vipindi vya kumbukumbu ya mambo ya kale vilivyopewa jina “SOGEA NIKUJUZE” akiwahiza juu ya umhuimu wa kujifunza historia ya Zanzibar.
Mhe. Hemed akibofya kitufe maalum kushiria uzinduzi rasmi wa vipindi vya mambo ya kale vilivyoandaliwa na kampuni ya Mavips Pictures katika hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss AbdulWakili Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar akikabidhi vyeti pamoja na zawadi kwa washiriki waliosaidia kufanikisha hafla ya uzinduzi wa vipindi vilivyoandaliwa na Kampuni ya Mavips Pictures ambavyo vitarushwa hewani kwa Kushirkiana Mambo TV Swahili
 Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar akikabidhi vyeti pamoja na zawadi kwa washiriki waliosaidia kufanikisha hafla ya uzinduzi wa vipindi vilivyoandaliwa na Kampuni ya Mavips Pictures ambavyo vitarushwa hewani kwa Kushirkiana Mambo TV Swahili

                                                                     Picha na OMPR

Na Kassim Abdi , OMPR

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kuzipa Ushirikiano taasisi na kampuni binafsi zenye lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuiendeleza na kuitambulisha historia ya Zanzibar kwa lengo la kuimarisha utalii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed  Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati wa akizindua  vipindi vya  kumbukumbu ya mambo ya kale Zanzibar vilivyopewa jina (SOGEA NIKUJUZE) uzinduzi ambao uliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni  Jijini Zanzibar.

Mhe. Hemed aliwapongeza watayarishaji  wa  vipindi hivyo vilivyoandaliwa na kampuni ya Mavips Pictures kwa ushirikiano wa pamoja  na Mambo TV Swahili,  kwa kujitokeza kwao kuwa wa kwanza  kuja na wazo la kutayarisha vipindi maalum vya kuitambulisha historia ya Zanzibar ambavyo vina lenga zaidi kutoa Elimu na  kuelimisha jamii ya kizanzibari katika kujua mengi yaliyoizunguka jamii yao.

Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuitangaza historia ya Zanzibar , hivyo alitoa rai kwa  vyombo vyengine vya habari  kuiga mfanbo huo kwani historia ya Zanzibar ina uwanja mpana  kupitia Nyanja mbali mbali jambo ambalo linahitaji kazi na nguvu ya ziada ili kufahamu historia ya Zanzibar kwa ukamilifu wake.

Alieleza kuwa, Jumuiya na Taaisis binafsi zinapaswa kushiriki lengo likiwa ni kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha uendelezaji wa utalii wa ndani na nje akitolea mfano viongozi wa dini wana mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa kuizungumzia historia ya Zanzibar kwa kuinasibisha na dini ya kislamu.

“Utalii wa kidini ni mzuri ambapo watu mbali mbali hupenda kutembelea kwenye maeneo yanayohusina na dini zao” Alieleza Mhe. Hemed

Mhe. Hemed alisema Zanzibar ina maeneo mengi ya kihistoria ambayo yalikuwa ni sehemu ya uchumi wa nchi na kuelezaa kuwa historia ni roho ya taifa kwani inasadia kutengeneza njia sahihi za maisha na kujua wapi tunapoelekea.

Alisema Zanzibar imejaliwa kuwa na vivutio vyingi vya utalii kushinda nchi nyingi duniani lakini changamoto inayojitokeza baadhi ya historia hizo hazijulikani na wazawa jambo linalorejesha nyuma kukuza kasi ya uchumi na kujenga ustawi mzuri wa jamii.

Alifafanua kuwa, Uchumi wa Zanzibar ya kale ulikuwa na vyanzo vya kuaminika kutokana na miundombinu imara iliowekwa ikitolea mfano Rasi ya Mkumbuu iliyoko Pwani ya Magharibi ya Pemba kuanzia mapema mwa karne Kumi ilikuwa ni bandari iliyostawi ilikuwa ikitumika kusafirisha biashara zilizopelekwa nchi mbali mbali Barani Afrika, Uarabuni, India na Ghuba ya Uajemi.

Vile vile, Mhe. Hemed alisema Rasi ya Mkumbuu ilikuwa kituo muhimu cha kuendele dini na biashara zama hizo kabla la ujio wa utawala wa kwanza wa kigeni wa kireno uliotajwa katika rekodi za Oman ulioanzia karne ya nane.

Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa, uchunguzi wa Akiolojia uliofanyika kwenye mapango ya Fukuchani Mkoa wa Kasakazini Unguja pamoja na Kuumbi Jambiani umebaini kua Zanzibar katika karne ya kwanza ilikuwa tayari imeanzisha uhusiano wa kibiashara nan chi za Bara Arabu, India na Afrika kwani atu wake walianza kuishi katika visiwa hivyo kwa Zaidi ya miaka Elfu Ishirini (20) kabla ya kuzaliwa kwa Nabii Issa (AS).

“Kinachohitajika sasa ni kuanzisha fursa nyingi kwa wazanzibar katika kuitangaza Zaidi historia kwa lengo la kuhamasisha watalii wa ndani waweze kutembelea maeneo ya kihistoria kwa ajili ya kujifunza mambo mbali mbali” Alisema Makamu wa Pili

Aidha Mhe. Hemed alisema kuna haja kwa jamii kubadilisha mtazamo katika kuendeleza utalii wa ndani kwa kuondosha dhana ile ya kuwa maeneo ya kiutalii ni Mji Mkongwe , Jozani, kizimkazi na kwenye mashamba ya viungo, kwani kutegemea utalii wa hii kunapelekea kuporomoka kwa uchumi endapo kutatokea changamoto kama vile Covid 19 ilioikumba Dunia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzbar alitumia fursa hiyo kuiomba  Wizara ya Utalii na Mambo ya kale kuanzisha mbinu mbali mbali za kuhuwisha na kuendelea historia ya Zanzibar kama vile kuanzisha mashindano tofauti pamoja na  kutoa zawadi kwa watalii na kampuni zinazofanya vizuri katika kutangaza historia na Utalii wa  Zanzibar .

 “ Ni vyema kwa  wizara kuwaruhusu watu kufanya matukio mbali mbali katika maeneo ya kihistoria  akitolea mfano kuanzishwa  kwa shughuli za kimichezo na burudani, kushawishi kampuni kubwa za kurikodi filamu kuja kurikodi filamu zao pamoja na kurushu kufanyika kwa matukio muhimu ya kufunga ndoa” Alisema Makamu wa Pili

Nae, Waziri wa Utalii na mambo ya kale Mhe. Leila Mohamed Mussa aliwapongeza vijana wa Kampuni ya mavips Picture kwa kujitolea kwao na kuthamini azma ya serikali ya awamu ya nane katika kukuza sekta ya Utalii kwa kuendeleza historia ya Zanzibar kwa kufanya ubunifu wa kuaanda vipindi.

Alieleza kuwa, vijana hao wameonesha utayari kwani hadi sasa wamekwisha andaa vipindi vya kurushwa hewani kwa kipindi cha mwaka mzima jambo ambalo linaashiria kujipanga vyema katika kutoa elemu kupitia vipindi hivyo bila ya kusita.

Mhe. Leila alitumia fursa hiyo kwa kuwaomba vijana na kampuni nyengine kuiga mfano wa Kmapuni ya Mavips Pictures kwa kujitokeza kubuni vipindi kama hivyo ili kujenga miyo ya kizalendo katika kulitumikia taifa lao.

“Mhe. Mgeni Rasmi vijana hawa nawapongeza sana kwa uzalendo wao kwani walipo kuja Afisini kwangu kuniona hawakuonesha kuhitaji pesa bali uzalendo wao ndio umewasukuma kuaanda vipindi hivyo” Alisema Mhe. Leila

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mavips Pictures Bw. Mudrik Kassim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa vipindi vilivyoandaliwa vina lenga kutanua wigo kwa wenyeji na wageni kufuatilia historia ya Zanzibar.

Alisema kubuniwa kwa vipindi hivi vitasaidia kwa kisai kikubwa kutoa elimu ya kwa kuelimisha watu juu ya historia ya Zanzibar iliotokea karne nyingi zilizopita.

Mkurugenzi Mudrik alieleza kuwa kutangazwa kwa vipindi hivyo, kutatoa muwamko wa kuboresha miundombinu ya burudani ambapo utaratibu wa vipindi vitarushwa hewani kupitia Mambo TV Swahili kila siku ya Jumamosi wakati wa Saa mbili na Nusu Usiku (2:30) kuanzia Juni 12 mwaka huu.

Alieleza kwamba mbali na mafanikio walioyapata katika kutayarisha vipindi hivyo lakini walikabiliwa na changamoto ikiwemo ufinyu wa bajeti katika kuyafikia maeneo mengi ya kihistoria pamoja na ugumu wa kuyafikia maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na watu binafsi.

Mkurugenzi huyo wa Mavips Pictures aliomba serikali kupitia wizara ya Utalii na mambo ya kale kuwa muhimili wao kwa kuwapatia usimamizi kwa kuwaunga mkono kuweza kufanikisha malengo waliojipangia kwa kutangaza historia ya Zanzibar pamoja na vivutio vya utalii kwa wenyeji na wageni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.