RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyiameupongeza utayari wa uongozi wa Klabu ya Small Simba wa
kutaka kurejesha hadhi ya michezo hapa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Klabu ya Small Simba, ambayo hapo siku za nyuma iliweza kuwika katika mashindano ya mpira wa miguu ndani na nje ya Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa moja kati ya ahadi zake za katika Kampeni za Uchaguzi ilikuwa ni kurejesha hadhi ya michezo kama ilivyokuwa au zaidi ya ilivyokuwa katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane jambo ambalo litafanywa na wadau wa michezo na Serikali jukumu lake ni kuweka mazingira mazuri.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mafanikio katika sekta ya michezo hayawezi kupatikana iwapo hakutowekwa mazingira mazuri katika sekta hiyo, hivyo Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na wadau wote wenye azma ya kuiimarisha sekta ya michezo ili kuhakikisha inaimarika.
Alitoa pongezi kwa uongozi huo kutokana na mawazo yao ambayo yanaendana na yale ya Serikaliya kuanzia chini kwa kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana huko Fuoni Kibondeni ambalo ni jambo jema na aliliunga mkono huku akisisitiza kwamba nchi zote zilizofanikiwa katika soka duniani zimeanzia na vituo vya mafunzo na kuibua vipaji vya vijana wakiwa wadogo.
Alieleza kwamba kwa vile tayari timu hiyo imeshapatiwa eneo la kudumu la kufanyia shughuli zao, ni jambo jema ambapo hatua inayofuata ni kuhakikisha eneo hilo lina kuwa na miundombinu inayotakiwa hasa ikizingatiwa kwamba tayari wameshalifanyia upembuzi yakinifu.
Rais Dk. Mwinyi aliunga mkono maelezo ya uongozi huo kwamba michezo ni biashara na si burudani peke yake hivyo, ni vyema vilabu vyote vikaendeshwa kibiashara hatua ambayo itasaidia kutoa ajira pamoja na kuongeza ari ya vijana kujinga katika michezo.
Alisisitiza kwamba suala zima la matatizo katika michezo ikiwemo uongozi, uhaba wa walimu, tatizo la waamuzi, uadilifu katika vilabu na taasisi za michezo jambo ambalo ni sahihi lakini kwa vile wana azma ya kufungua ukurasa mpya ni lazima kujipanga kwa vipi matatizo hayo yatatatuliwa.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema kukawekwa utaratibu wa watu kuwajibika katika vilabu sambamba na kutafuta njia ya kutengeneza makocha kwa kufanya utaratibu wa kufundisha makocha hali ambayo itaondokana na uhaba wa walimu na kuupelekea mchezo huo kuimariska.
Akielezea kuhusu suala zima la udhamini, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba watu wengi waliokuwa wanadhamini michezo hapa Zanzibar waliwacha udhamini wao kutokana na kutokuwepo kwa uadilifu.
Alisema kwamba udhamini si msaada kwani hao wanaodhamini na wao huwa wanahitaji kutangazwa bidhaa zao hivyo, alieleza azma yake ya kufanya mkutano na Makampuni mbali mbali hapa nchini na kuyashawish ili kuonakwa utaratibu gani wanaweza kuidhamini ligi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwepo kwa mabadiliko kwa upande wa Mabaraza ya Michezo pamoja na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), ili kwenda kisasa zaidi ambapo tayari Wizara husika imeanza kulifanyia kazi suala hilo hivyo, hana shaka hilo litakaa vizuri kwani hatua zimeanza kuchukuliwa.
Rais Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa kurejeshwa kwa mashindano ya Ligi ya Muungano (Super League), na kuunga mkono wazo hilo huku akisisitiza kwamba ni vyema mashindano hayo yakarejeshwa ili iwe sehemu ya kuibua vipaji.
Sambamba na hayo, amepokea ombi lao na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha timu hiyo inaweza kujitegemea na iwe chanzo cha wao kujitegemea.
“Mimi nina dhima na kwa vile nimetoa ahadi maana yake ni kwamba nitaulizwa baada ya miaka mitano, tuko wapi? hivyo, nyinyi ni wadau muhimu sana wa kunisaidia kutekeleza ahadi yangu...tukiwa na ‘academy’ kama hizi itakuwa sehemu moja nzuri ya kuanzia”, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Small Simba Suleiman Mahmoud Jabir alisema kuwa kuanguka kwa Klabu ya Small Simba kumetokana na kuangukwa kwa mpira wa miguu hapa Zanzibar na kupelekea kuondoka kwa ushabiki na upinzani wa mchezo huo.
Hivyo, waleileza azma ya kuirejesha hali hiyo katika mpira wa miguu hapa Zanzibar na kusema kuwa sifa na mazuri yote yaliyofanywa na Small Simba yalitokana na programu za vijana zilizokuwepo katika timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1970.
Alisema mpaka mwaka 1983 timu hiyo iliweza kupanda daraja na mwaka huo huo ilichukua ubingwa wa Zanzibar na kusema kwamba ili kufikia malengo mazuri katika michezo ni lazima kuwepo kwa nidhamu, ubunifu, mipango, kujituma, kujitolea, juhudi, ustahamilivu, dira na malengo yanayotekelezeka.
Mtendaji Mkuu
huyo aliongeza kuwa michezo imekuwa si
michezo tu bali ni biashara hivyo ni lazima kuwepo kwa rasili mali watu wenye
elimu ya kuendeleza hilo, rasilimali nyenzo, zinazoendana na viwango vinavyo pamoja
na rasilimali fedha.
Alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Serikali kwa kupatiwa eneo la michezo katika eneo la Fuoni Kibondeni ambolo litajumuisha michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, mpira wa mikono, tenis, kuogelea na michezo mengineyo.
Alisema kwamba mbali ya kuwepo kwa timu yao wa Small Simba pia, kutakuwa na kituo cha kuendelezavipajivyamichezokwavijanaambapotayarikituohichokimeshasajiliwarasmin.
Aidha, alsiema kuwa tayari wana mpango wa program yao hiyo, wameshaandika Mtaala maalum wa Small Simba ambao utaanzia miaka 8 hadi 20 huku uongozi huo wakiomba kupatiwa udhamini na Serikali kwa kuweza kulijenga kwani lengo lao ni kuliendesha kibiashara na kimasoko ambalo litatoa ajira mia moja, litachangia pato la Serikali pamoja na kupata michango mengine kadhaa.
Alifahamisha kuwa hali ya michezo hapa nchini haipo katika hali ya kufurahisha na kwa upande wa uongozi huo ulieleza kwamba bado kunachanga moto kadhaa katika soka hapa Zanzibar ikiwemo hali ya uwamuzi, uadilifu katika fedha hasa katika masuala ya kupatikana udhamini wa kudumu.
Alisema kuwa ni vyema jamii ikaelewa kwamba michezo hivi sasa ni zaidi ya kucheza hivyo, walieleza haja ya kuwepo kwa viongozi wenye elimu na umahiri wa kuendesha michezo hatua ambayo pia, itasaidia kupata udhamini wa uhakika wa ligi ya Zanzibar.
Aidha,uongozi huo uliomba kurejeshwa kwa kombe la Muungano (Super league) ambalo lilikuwa likileta raha, burudani na ushidhani kati ya timu za Tanzania Bara na Zanzibar ambapo pia, ilikuwa ni fursa njema kwa walimu hasa wanaofundisha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Star) kuwaona wachezaji wa Zanzibar na uwezo wao ili kuweza kujumuishwa katika timu hiyo.
Alisema kwamba hivi sasa kumekuwepo na manung’uniko kwamba wachezaji wa Zanzibar hawaonekani katika timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Star) labda wawe wanachezea timu za Yanga, Simba, Azam au timu nyengine kutoka Tanzania Bara, hiyo ni kutokana na kutoonekana uwezo wao.
Uongozi huo pia, ulitumia fursa hiyo kumuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba timu yao iko tayari kusaidia katika kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment